Uwekezaji Kwenye Kilimo cha Maembe Kunufaisha Wakazi wa Wilaya ya Kilindi



Wakazi wa Kilindi wanatarajia kunufaika na kilimo cha maembe mafupi yanayozalisha maembe mengi, makubwa na kwa wakati mfupi na lengo likiwa ni kulipatia zao hilo dhamani. Awali Wilaya ya Kilindi imekuwa yenye mafanikio makubwa katika uzalishaji wa maembe ya asili lakini kuna changamoto ya matumizi ya sayansi katika kilimo.

 Akizungumza na timu ya uandaaji wa Makala ya maeneo ya Uwekezaji katika Mkoa wa Tanga, Mhe. Seleman Salum Liwowa ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kilindi amesema kuwa, baada ya kuona fursa ya ardhi yao yenye kustawisha maembe kwa wingi, waliamua kubuni mradi wa maembe mafupi ili kunufaisha wananchi wengi zaidi.

“Kwa sasa tumetenga eneo la Sangeni lenye hekali 960 na tumeanza kumpatia kila mkulima aliye kwenye kikundi cha ushirika hekali 1 , miche kwa ajili ya zoezi hilo na tayari tumeshaotesha miche kwa ajili ya shamba la mfano ” alisisitiza afisa mipango wa Halmashauri ya Kilindi Bw. Simon  Vedastus Mzee.

Vilevile imeelezwa kuwa lipo soko la kutosha kwani maembe ya Kilindi yanapendwa sana na soko kubwa linapatikana upande wa Mashariki ya Kati. Miundo mbinu mizuri imesaidia wanunuzi kufika katika Wilaya ya Kilindi kwani kuna barabara nzuri zinazofikika kwa urahisi ,nishati ya umeme na mawasiliano.

Mhe. Liwowa anatoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje kufika katika Wilaya yake na kushirikiana na Wakazi wa Kilindi kulipatia zao hili dhamani kwa kujenga viwanda ambayo vitaweza kusindika maembe na kutengeneza juice na kuleta utaalamu na vifaa vya kisasa ili kurahishisha ukulima wa zao la embe.

Wilaya ya Kilindi ipo ndani ya mwinuko na ina hali nzuri yenye ubaridi, mvua za wastani, udongo wenye rutuba na upatikanaji wa maji na madini mbalimbali. Pia uwekezaji unaweza kufanyika katika uzalishaji wa viungo, utalii katika maeneo ya milima ya Nguu, Mlima wa Kilindi na poli la Handeni.

Kwa taarifa zaidi juu ya fursa za uwekeza katika wilaya ya Kilindi tembelea tovuti ya Mkoa wa Tanga www.tanga.go.tz kisha chagua wilaya ya Kilindi na pia unakaribishwa kwenye Jukwaa la Uwekezaji kanda ya Kaskazini litakalofanyika katika Mkoa wa Tanga septemba 26-21 mwaka huu. Kushiriki Jukwaa la Uwekezaji tembelea tovuti ya uwekezaji www.investnorthernzone.go.tz na jaza form maalumu.



Mhe. Seleman Salum Liwowa ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kilindi 

 Muonekano wa baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Kilindi
Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi


Written by

0 comments: