Mamlaka ya Vitambulisho Vya Taifa (NIDA) Umezindua Rasmi Zoezi La Utambuzi Na Usajili Wa Watu Katika Mkoa Wa Tanga

 
Joseph Makani, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho (NIDA) akizungumza wakati wa uzinduzi. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Chiku Gallawa ,  Katibu Tawala Mkoa wa Tanga Bw.Salum Mohamed Chima (Alhaj) na Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mhe. Halima Dendego

WAKUU wa Wilaya, Wakurugenzi, Watendaji katika ngazi zote Tarafa, Kata, Mitaa, Vijiji na Vitongoji, Viongozi wa Dini na Viongozi wa Vyama vya Siasa wameagizwa kuonyesha ushirikiano  katika kuhakikisha jukumu la utambuzi na usajili wa watu linaenda sawasawa na maagizo ya Serikali .
Msisitizo huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Chiku Gallawa ambaye ameahidi kutoa ushirikiano wakati akizindua rasmi zoezi la utambuzi na usajili wa watu uliofanyika mapema leo asubuhi katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
 Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho( NIDA) Bw. Joseph Makani amewataka wakazi wa Tanga kujitokeza na kutoa ushirikiano katika zoezi zima kwani zoezi  hilo Mkoani Tanga ni utekelezaji wa Mpango wa Usajili wa Wakazi waishio Kihalali Nchini kwa lengo la kuwapatia vitambulisho vya Taifa kwa hadhi ya raia, Wageni wakazi na Wakimbizi.
“Fichueni wale ambao hawastahili kupata vitambulisho vya uraia kwa kutoa taarifa katika ofisi za uhamiaji na polisi ili taifa lisije likaingia katika hatari ya kuwasajili wageni kama raia”amesisitiza Makani.
 Zoezi la Utambuzi na Usajili Mkoani Tanga linategemea kuanza Oktoba 12 mwaka huu. Wananchi wanaombwa kuhakikisha wanajisajili kwa wenyeviti wa mitaa ili kurahisisha zoezi hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Chiku Gallawa akizindua rasmi zoezi la utambuzi na usajili wa watu
 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga Bw. Salum Mohamed Chima ( Alhaji) akizunguza muda mchache kabla ya uzinduzi
Baadhi ya viongozi wawakilishi kutoka katika Wilaya za Tanga wakati wa uzinduzi


Written by

1 comment:

  1. Mimi shabiri Hemedi Bakari mzaliwa wa Tanga, jina langu la la NIDA limekisewa, nataka kurekebisha ila sijui niende wapi

    ReplyDelete