Kilindi kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani zao la mahindi
Katika kukabiliana na tatizo la njaa pamoja na ulanguzi wa mazao
ya nafaka unaofanywa na wafanyabishasha walanguzi Halmashauri ya wilaya ya
Kilindi imeanza mchakato wa ujenzi wa viwanda vya kusindika mazao ya Mahindi na
Mtama ili kuyaongezea thamani.
Hayo yamebainishwa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi Mtendaji wa
halmshauri hiyo, Daudi Mayeji wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa
miradi ya kuleta matokeo makubwa sasa wakati wa mkutano wa pamoja (Inter
Council Meeting) wa siku mbili uliofanyika wilayani handeni na kujumuisha
viongozi wa kisiasa na watendaji wa ngazi ya mkoa na halmashauri.
Alisema hatua hiyo itapunguza tatizo la njaa linalozikabili kaya
kila mwaka, itaongeza kipato cha mkulima kutokana na kuongezeka kwa thamani ya
bidhaa za unga wa mahindi na mtama sokoni ambao utakasindikwa viwandani na
wakulima.
“Mradi huu umetokana na uchunguzi wetu tuliofanya na kubaini
kwamba wakati wa mavuno wakulima wanapata mengi lakini yanachukuliwa kwa bei
ndogo na wafanyabishara walanguzi kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania na nje ya
nchi na hivyo baada ya muda mfupi wao hubaki maskini wa kuomba chakula cha
msaada”, alisema na kuongeza.
“Kwa hiyo tukaona tuwe na viwanda vya kusindiaka na kufungasha
unga wa mahindi na mtama ambavyo vitasimamiwa na wakulima wenyewe kupitia chama
chao cha ushirika lengo la halmashauri ni kuhakikisha mkulima wa kilindi
anapata tija kupitia shughuli zake hizo”.
Alisema ili kuhakikisha uzalishaji wa kutosha wa mazao hayo
tayari wameanzaisha program maalum ya kuwafundisha wakulima hao mbinu za kisasa
za uzalishaji wa mazao hayo na kwamba tayari wakulima wa kata ya Songe
wametenga eneo la ujenzi wa kiwanda chao.
“Mradi huu utakwenda kwa awamu na tayari tumehamasisha wakulima
wanajiunga kwenye vyama vya ushirika kwa kutoa viingilio na hisa na
tumeshatembelewa na taasisi za fedha ambapo kwa kuanzia kata ya Songe wamepata
wazalishaji ambao wataleta mashine yenye uwezo wa kusindika tani 20 za mahindi
kwa siku”, alisema.
Mayeji alisema mashine moja ina thamani ya sh. Milioni 200 na
inaundwa na sehemu kuu nne ambazo ni kwa ajili ya kusafisha nafaka, kukoboa,
kusagwa na kisha kufungashwa katika vifungashio maalum na kwamba katika
kufanikisha kiwanda hicho cha awali halmashauri imechangia kiasi cha sh.
Milioni 93 kwa ajili ya ununuzi wa mitambo.
0 comments: