Madaktari Mkoani Tanga Wapania Kutokomeza Vifo Vitokanavyo Na Uzazi

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt Asha Mahita akieleza mkakati wa kukabiliana na upungufu wa damu kwa wajumbe 
Mratibu wa afya ya mama na mtoto Mkoa wa Tanga Dorothy Lema akionesha hali ya vifo vya kina mama tangu mwaka 2010 -2013
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Pangani Dkt Dennis Ngaromba akichangia mjadala jinsi ya kukabiliana na vifo vitokanavyo na uzazi .Habari & picha na Fatna Mfalingundi- Afisa Habari Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe.
Madaktari Mkoani Tanga kwa pamoja wameazimia kuchukua hatua za tahadhari  ikiwemo kubuni njia mbadala  zitakazowezesha kuokoa maisha ya mama na mtoto  pindi wanakapokumbana na vikwazo vya dharura wakati wa mama kujifungua ili kufikia lengo la nne la dunia  la kukabiliana na vifo vya uzazi,watoto wachanga na walio chini ya umri wa miaka mitano.
Madaktari hao walifikia hatua hiyo mwishoni mwa wiki wakati wa kikao  cha pamoja cha Sekta ya Afya kilichofanyika Wilayani Lushoto na kuwajumuisha ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa, Waganga Wakuu wa Wilaya ,Wenyeviti wa Bodi za Afya, Wadau wa Sekta ya Afya wakiwemo MSD,NHIF,WHO,kfw,WEI na GIZ kwa lengo la kujadili changamoto na mikakati ya kuboresha Sekta ya Afya kwa mwaka 2014/2015.
Akitoa maelezo kuhusu kukabiliana na changamoto ya upungufu wa damu salama katika benki za damu ambayo ilitajwa kuwa ni miongoni mwa sababu kubwa zinazopelekea vifo vingi vya wajawazito, Mganga Mkuu wa Mkoa wa  Tanga Dkt Asha Mahita, alisema kuwa miongoni mwa mikakati waliyojiwekea ni pamoja na kuifanya hospitali ya Mkoa wa Tanga ya Bombo kuwa kituo cha kusambaza damu kwa hospitali za Wilaya badala ya kila wilaya kuomba na  kusubiri damu kutoka hospitali ya rufaa ya KCMC.
“Tumeshaiandikia  Wizara kuiombea hospitali ya Mkoa ya Bombo kuwa kituo cha kusambaza damu kwa Halmashauri zake, tunaamini kwa kufanya hivyo tunaweza kupunguza tatizo la upungufu wa damu na vifo vya kinamama”.Alisema Dkt Mahita.
Akichangia mjadala  Mganga Mkuu wa Wilaya ya Pangani Dkt Dennis Ngaromba, aliwashauri madaktari wenzake kuachana na rufaa za ghafla na kuwataka  kuwafuatilia wajawazito wanaowapatia rufaa ya kwenda kujifungulia mahali kwingine kwa kuanzisha utaratibu wa kujaza fomu tatu ambayo moja itabaki mahali alipofungulia kadi,nyingine itakwenda alikopewa rufaa na nyingine kubaki katika ofisi za kijiji au mtaa ambapo utaratibu huo utakwenda sambamba na mawasiliano ya simu lengo likiwa ni kutoa historia ya Mjamzito ili hatua stahiki za haraka zichukuliwe.
“Pangani tumeweza kupunguza  vifo vya uzazi  kwa kuachana na rufaa za fumanizi na tumeweka utaratibu wa kuwatambua wanaofariki kutokana na uzazi kwa kuzishirikisha vyema ofisi za Serikali za vijiji”.Aliongeza Dkt Ngaromba.
 
Awali akiwasilisha mada Mratibu wa Afya ya Mama na Mtoto Mkoa wa Tanga Dorothy Lema, alisema kuwa hali ya vifo vya uzazi pamoja na watoto wachanga nchini Tanzania bado siyo nzuri,kwani inakadiriwa kuwa wanawake 8000 hupoteza maisha kila mwaka hapa nchini,huku Tanga peke yake wanawake 225 walipoteza maisha mwaka 2013.  
 
 


Written by

0 comments: