Semina ya UKIMWI kwa makundi maalumu yalenga Uhamasishaji wa Elimu kwa Jamii


Washiriki wa semina ya masuala ya UKIMWI kutoka makundi ya Wanahabari, Vijana na Viongozi wa dini wakisikiliza moja ya maada zilizowasilishwa.

Ni jambo lisilopingika kuwa kundi la wanahabari, Vijana na Viongozi wa dini ni makundi yenye nafasi muhimu sana katika jamii  hususani katika kufikisha ujumbe husika.

Umuhimu huu ndio uliopelekea Mratibu wa Masuala ya UKIMWI wa Jiji la Tanga Bw. Moses Kisibo kuona umuhimu wa kuyakutanisha makundi haya ili kuyapatia elimu juu ya Ugonjwa wa hatari wa UKIMWI na baadaye makundi haya kujipanga kwa pamoja na kuazimia ni nini kifanyike ili haya makundi yakawe chachu ya kutoa elimu kwa jamii juu ya kupunguza maambukizi mapya ya UKIMWI.

Semina ya UKIMWI kwa makundi maalumu imefanyika mwanzoni mwa wiki katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Mipango miji ambapo makundi haya yameaswa kuepuka unyanyapaa wa wagonjwa wa UKIMWI kwa kuendelea kuwahudumia kwa upendo.
Aidha elimu imetolewa kuwa ni vyema kupata elimu kutoka  kwa wataalamu kuhusu taratibu sahihi za kumhudumia mgonjwa wa UKIMWI ili kuepuka maambikizi wakati wa kumhudumia mgonjwa.

Akizungumzia tabia na mazingira hatarishi kwa maambukizi ya UKIMWI, mwezeshaji wa elimu ihusuyo UKIMWI Bw.Desideri Joseph amebainisha kuwa ngono isiyo salama, kuwa na wapenzi wengi,mila potofu, ukosefu wa elimu na na upataji habari, ukosefu wa upatikanaji huduma ya afya, ukosefu wa ajira na tabia ya kunywa pombe kupita kiasi ni miongoni mwa mazingira hatarishi.

Hata hivyo makundi haya maalumu ya wanahabari, Vijana na Viongozi wa dini wameamua kujiwekea mikakati na maazimio ni kwa jinsi gani yangetumia nafasi yaliyonayo katika jamii ili kutoa elimu juu ya ugonjwa wa UKIMWI kwa lengo la kupunguza maambukizi.

Wanahabari walikubaliana kutumia kalamu zao na kuelekeza nguvu zao katika kuandaa machapisho na vipindi vya radio na televisheni ambavyo vitalenga mahusus i elimu jinsi ya kujikinga na maambukizi mapya ya huu ugonjwa hatari, elimu ya jinsi ya kuishi bila kujinyanyapaa wala kuwanyanyapaa wengine na pia kuitaarifu jamii juu ya tafiti mpya juu ya ugonjwa wa UKIMWI.

Nalo kundi la vijana limeona ni muda mwafaka wa wao kutumia elimu waliyoipata  juu ya masuala ya UKIMWI na kuazimia kuipeleka kwa jamii hasa kwa kupitia mabaraza ya vijana.

Vilevile Viongozi wa dini nao hawakubaki nyuma bali wameweka azmio la kutumia majukwaa ya Misikiti na Makanisa kupasha habari  na kutoa elimu ya UMIKWI kwa waumini wao. 

Ni wito kwa  kila mmoja kuamua kuacha vitendo hatarishi vitakavyopelekea kupata maambukizi mapya ya UKIMWI kwani ugonjwa huu hatari hauchagui elimu, cheo, Umri wala Imani ya mtu. Imethibitika kuwa kinga pekee ya kuepuka maambukizi haya  ni kuacha ngono kabisa kwa wale ambao hawako kwenye ndoa na pia walioko kwenye ndoa kuendelea kuwa waaminifu kwa wapenzi wao.

 Mratibu wa Masuala ya UKIMWI wa Jiji la Tanga Bw. Moses Kisibo akifafanua jambo wakati wa semina
Kundi la wanahabari kutoka vyombo vya habari mbalimbali wakijadiliana  ni nini kifanyike ili kuweza kuielemisha jamii juu ya masuala yahusuyo UKIMWI.

Kundi la Vijana wakijadiliana  ni nini kifanyike ili kuweza kuielemisha jamii juu ya masuala yahusuyo UKIMWI
Kundi la Viongozi wa dini wakijadiliana  ni nini kifanyike ili kuweza kuielemisha jamii juu ya masuala yahusuyo UKIMWI


Written by

1 comment:

  1. jamii inatakiwa kubadili tabia juu ya ugonjwa wa UKIMWI badala ya kusubili Serikali na kuilaumu, kwani ugonjwa wa UKIMWI, unahitaji mikakati kuanzia ngazi ya mtu binafsi, familia, kaya makundi ya kijamii ndio serikali kuwekea mkazo katika mikakati hiyo

    MOSES KISIBO
    BOX 178
    TANGA JIJI

    ReplyDelete