TASAF II ilivyogeuza changamoto ya uhaba wa chakula kuwa fursa ya uchumi na maendeleo kwa wakazi wa korogwe vijijini





Mzee Rajabu Kufa  mlemavu wa macho na mkazi wa kijiji cha Kwetonge kilichopo kata ya Mashewa mmoja wa wakazi wa Korogwe ambao wamenufaika  na mradi wa TASAF II wa ufugaji ng’ombe kupitia kikundi  cha Jipemoyo

Watu wengi duniani huziona changamoto zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku kuwa ni vikwazo vya kutofikia malengo waliyojiwekea au wanayopaswa kuyafikia kama binadamu.Ni watu wachache sana wenye ujasiri wa uthubutu katika maisha yao,hata ikawapelekea wenye busara kutengeneza msemo wa “uoga wako ndiyo umasikini wako” wakilenga  kuwatia watu moyo na kuwataka kuthubutu hasa katika masuala yenye changamoto.

Korogwe vijijini yenye ukubwa wa kilomita za mraba 3544,kata 20,vijiji 122,vitongoji 610 na jumla ya Wakaazi 242,038 kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2012 ni moja ya jamii iliyojipatia manufaa kwa kutumia hekima za msemo huo.Korogwe ambayo kilimo ndiyo njia kuu ya wakaazi wake kujipatia chakula na kipato kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia 2010 imekuwa ikipata mvua za kubahatisha jambo lililopelekea kukabiliwa na uhaba wa chakula kwa baadhi ya maeneo na maeneo mengine kukumbwa na njaa hata kupelekea Serikali kupeleka chakula cha msaada.

Pamoja na kukabiliwa na changamoto hiyo wakaazi hao hawakukaa na kuiangalia njaa ikiharibu maisha yao,badala yake kwa kutumia fursa zilizopo kama Mfuko wa maendeleo ya Jamii (TASAF II) iliyokuwa ikitekeleza program zake wilayani humo waliiona ni nafasi nyingine ya kujipatia maendeleo endelevu,wakaonesha uhitaji wao,wakathubutu na kwa kushirikiana vyema na Wataalamu wa kada mbalimbali katika Halmashauri, leo hii Wananchi hao  wanajivunia mafanikio yao.

Edward Lukinisha ambaye ni mratibu wa Mfuko wa maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya wilaya ya Korogwe anaeleza kwa kina jinsi jamii ya wanakorogwe ilivyofaidika na changamoto ya uhaba wa chakula kwa kuigeuza kuwa fursa ya kiuchumi,na kwamba sasa Wananchi hao wanayo miradi inayowaingizia kipato na kuwahudumia kila siku hata wameondokana kabisa na changamoto ya uhaba wa chakula.

“Korogwe ilipotangazwa kuwa ni moja ya wilaya zinazokabiliwa na uhaba wa chakula,TASAF kama Mfuko wa kusaidia jamii katika fedha za bajeti kuanzia mwaka 2010 tulikaa na baadhi ya vijiji na kuwataka waibue miradi ambayo si tu ingekidhi haja ya kumaliza uhaba wa chakula kwa wakati huo,bali pia ingekuwa ni miradi endelevu hata kwa vizazi vijavyo” alisema Lukinisha.

Anafafanua kuwa uibuaji wa miradi hiyo iliyogawanyika katika Sekta kuu tatu za mawasiliano,kilimo na ufugaji uliolenga kukabiliana na uhaba wa chakula ulikuwa katika sura mbili,miradi ambayo ingeinufaisha jamii moja kwa moja na miradi ya vikundi.Katika miradi ya jamii iliwapasa  wanajamii wenyewe kuibua miradi endelevu ambayo ingeinufaisha jamii nzima na kisha kubainisha kaya zizoathiriwa zaidi na uhaba wa chakula, hivyo wale wenye uwezo wa kufanya kazi katika kaya hizo ndiyo ambao wangefanya kazi ya ujenzi wa mradi wa jamii na kulipwa ujira ambao ungewasaidia kupata chakula kwa wakati huo,na wakati huo huo jamii nayo ingenufaika kwa kupata mradi endelevu.

Moja ya miradi iliyojengwa wilayani humo kutokana na changamoto hiyo ni barabara ya  kijiji cha Changarikwa kilichopo kata ya Magamba Kwalukonge.Barabara hiyo ilichimbwa kwa urefu wa km 5.5 na upana wa mita 4.5 kwa gharama ya Tsh ml 32 zilizotolewa kwa Wananchi hao kama ujira. 

Rukia Hamisi aliyekuwa mmoja wa washiriki katika ujenzi wa mradi huo anasema barabara hiyo ilianza kuchimbwa mwaka 2010 na kukamilika 2011,ambapo wataalamu wa Halmashauri walipima na kutoa ushauri na wao Wananchi walichimba kwa ujira wa Tsh 3000 kwa kutwa.Fedha ambayo anasema ndiyo ilikuwa ikimsaidia kununua chakula kwa ajili ya familia yake.

 “Barabara hii licha ya kuwa sasa inatusaidia sana kwa usafirishaji wa mazao yetu,lakini wakati wa kuitengeneza ilitusaidia sana kwani tulioichimba tulilipwa na fedha ile tuliitumia kwa kununua chakula kwani hatukupata kabisa mazao kwa mwaka ule.”Anasema Rukia.
Naye bi.Ndatima Shemshi anaongeza kuwa hapo mwanzo walitembea umbali mrefu kwa miguu kwani ilikuwa ni vigumu kwa magari kufika kijijini kwao,lakini sasa magari yanaingia hadi kijijini na kubeba mazao yao kama mahindi na ngwasha ambayo hununuliwa sana na Wakenya kwa ajili ya kutengenezea biskuti. Hata hivyo mama huyo ana ombi maalum kwa wadau wenye uwezo kuwekeza zaidi katika barabara hiyo ili iweze kutokezea kitongoji cha Mlembule katika Mamlaka ya Mji mdogo wa Mombo ambako ndipo kuliko na barabara kuu inayounganisha nchi za Afrika Mashariki kupitia Arusha.

Sekta ya mawasiliano inapewa nafasi pia katika kijiji cha Makumba  ambapo wanakijiji hao kwa pamoja wanaamua kujenga kivuko kitakachounganisha kijiji chao na kijiji cha Kazita.Wanakijiji hao wa Makumba wanapata msukumo wa kujenga kivuko hiki ili kuisaidia jamii  kubwa ya wenzao waishio katika kijiji cha kazita katika vitongoji vya Magunga na Mtemiroda huku huduma zote muhimu za kijamii zikipatikana kijiji cha Makumba.

Afisa Mtendaji wa kijiji cha Makumba Petro Harawa anasema kimsingi vijiji hivyo viwili ni kama kijiji kimoja cha watu 3069 huku 800 kati yao wanaoishi Kazita wakitenganishwa na bonde korofi hasa nyakati za mvua,hivyo kama kijiji waliona ni vyema kujenga kivuko kitakachowaunganisha nyakati zote na ndipo TASAF II ilipowapatia ml 28 na kuanza ujenzi wa kivuko hicho Mei 2012.
 
Oddos Komba Mwanakijiji wa Kazita pamoja na kushukuru kwa kuondokana na njaa pia anasifu jitihada za Serikali za kuimarisha miundombinu ya mawasiliano na uchukuzi vijijini kwa kuielezea kadhia waliyokuwa wakiipata hapo awali hasa nyakati za masika huku akitolea mfano wa mwaka 2006  pale wanafunzi wa kijiji cha kazita waliposhindwa kufanya mtihani wa darasa la nne kutokana na mvua kubwa kusababisha mahali hapo kutokupitika na kukifikia kijiji cha Makumba ambako ndiko kuliko na shule.

Sambamba na mawasiliano miradi mingine iliyokusudiwa kuinufaisha jamii nzima ni ile ya Sekta ya kilimo, ambayo ni ujenzi wa mifereji ya umwagiliaji.Katika utekelezaji wa kusudio hilo vijiji vinne ambavyo ni Chekelei, Mazinde Mheza,Mazinde Goha na Makangara Songea vilinufaika nayo.

Michael Cassian ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya mradi wa mfereji wa umwagiliaji kijiji cha Chekelei anasema kuwa wao walipatiwa ml 31 ambazo zimeweza  kuchimba na kujenga mfereji wenye urefu wa mita 200 pamoja na vigawa maji nane.Mradi huo ulioanza kujengwa mwaka 2011 ulikamilika 2012 na tayari Wakulima wameanza kutumia katika msimu huu wa kilimo wakiwa na matumaini ya kuongeza uzalishaji wa mpunga mara dufu kwa sababu sasa hivi maji yanafika mashambani kwa uhakika na kwa kipimo kinachotakiwa.

Wakati Chekelei wakisubiri mavuno, kijiji cha Mazinde Goha wao wanajivunia mavuno ya matunda aina ya matikiti maji tani sita katika msimu wa kwanza kabisa April 2012 mara tu baada ya kukamilika kwa mradi wao Januari 2012, na sasa wanajipanga kufanya kilimo cha pilipilihoho,vitunguu , nyanya na mbogamboga kwa kipindi cha kiangazi.

Iddi Uledi Mwenyekiti wa kikundi hicho kiitwacho Songambele anasema walipatiwa ml 8.9 za kuchimba kisima na ununuzi wa mipira yenye uwezo wa kuhudumia ekari 15 za shamba ambazo walipewa na kijiji,lakini mpaka sasa wametumia ekari nne tu huku wakiendelea na juhudi za kufyeka pori lililobaki ili waweze kunufaika zaidi 

Katika harakati hizo za kuwapunguzia Wananchi makali yatokanayo na uhaba wa chakula TASAF II iliwekeza pia katika sekta ya mifugo huku wanufaika wakishuhudia ya kwamba wamepata faraja kubwa kwa kupata miradi ya ufugaji ng’ombe na mbuzi kwani mbali ya kuwapatia kipato pia imeimarisha afya zao kwa kunywa maziwa kila siku.

Miradi hiyo ya ufugaji ilitolewa kwa vikundi vya watu kumi na nne na kumi na tano kwa vigezo vya kuathiriwa na uhaba wa chakula na kuwa katika makundi maalumu ambayo ni walemavu,wajane na wagane, na kwa kuzingatia uwiano wa jinsia.

Rajabu Kufa ni mlemavu wa macho na mkazi wa kijiji cha Kwetonge kilichopo kata ya Mashewa anasema yeye amenufaika na mradi wa TASAF II wa ufugaji ng’ombe kupitia kikundi chao cha Jipemoyo.Anasema ng’ombe wake aliyempa jina la Sara amekuwa mkombozi mkubwa sana kwake hasa kwa kuzingatia hali yake isiyomwezesha kufanya kazi nyigine ngumu.

“Ng’ombe huyu ananisaidia sana kwani napata lita nne kila siku ambazo naziuza kwenye kituo cha maziwa kilichopo hapa kijijini kwetu,napata pesa za kujikimu mahitaji yangu kutokana na ng’ombe huyu,hivyo imenisaidia kuondokana na tatizo la kuombaomba na kuwa na uhakika wa kupata chakula kila siku”.Anasema Kufa.

Mzee huyu anakiri kuwa hawezi kumhudumia ng’ombe wake yeye mwenyewe,lakini ng’ombe huyo wa asili aliyeboreshwa ili kutoa maziwa ana afya njema sana.Kufa anasema ng’ombe huyo  huhudumiwa na mtoto wake ambaye humkatia majani ya kutosha kwa siku nzima kila asubuhi kabla ya kwenda kwenye shughuli zake.  

Anaongeza kuwa kijana wake ana furaha sana kumhudumia ng’ombe huyo kwani amempunguzia majukumu ya kumgharamia yeye kifedha.Mzee Kufa anaishukuru Serikali kwa kuleta mradi wa TASAF kwa wahitaji kama yeye na kusema kwake yeye hakika Serikali imemjali sana,pia anaishukuru Jamii ya kijiji chake kwa kuuona uhitaji wake  na kumchagua kupewa ng’ombe huyo.

Naye Bi. Stara Ponda mjane aishie katika kijiji hicho cha Kwetonge anasema mbali ya ng’ombe wake kuimarisha afya ya familia yake wakiwemo watoto ambao ni wajukuu zake anaowalea kwa kunywa maziwa lakini pia ng’ombe huyo humsaidia kupata mahitaji  ya shule ya watoto  kwa kuuza maziwa kila siku.
Wakati Wananchi hao wakifurahia ufumbuzi wa tatizo la uhaba wa chakula na kujipatia miradi ya maendeleo, Afisa Kilimo na Ushirika wa Halmashauri ya wilaya ya Korogwe Kakulu Lugembe anakiri kuwa katika kipindi cha mitatu  maeneo mengi ya Halmashauri yamepitia kipindi kigumu cha upungufu wa chakula hata kupelekea Serikali kuleta chakula cha msaada.

“Novemba 2012 Halmashauri ilipokea tani 111.8 za mahindi ya msaada toka Serikalini na kugawa katika vijiji 60 vya Kata 12 na Machi 2013 ilipokea tani 350.6 na kugawa katika vijiji 63 vya kata 12” anasema Lugembe.

Hata hivyo anasifu jitihada zilizochukuliwa na TASAF II kwani zilisisimua uwajibikaji kwa kuwa suala la upungufu wa chakula husababishwa na mambo mengi ikiwemo uvivu wa mtu husika,majanga kama  mafuriko na mabadiliko ya tabianchi.Anaielezea hali ya chakula kwa mwaka huu kuwa ina ishara njema kwani hali ya mazao mashambani ni nzuri ukiachilia mbali kata nne tu za Mashewa,Mkomazi,Mkalamo na Mazinde. 

Lugembe anawapongeza zaidi Wananchi waliochagua ujenzi wa mifereji ya umwagiliaji kwa kueleza kuwa kwa sasa kilimo cha uhakika na tija ni cha umwagiliaji kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa yasiyotabirika.Anaeleza kuwa hata Halmashauri imeelekeza nguvu zake katika ujenzi wa skimu za umwagiliaji ikiwemo ya Kwemkumbo katika mamlaka ya mji mdogo Mombo na katika bonde la Mkomazi ambazo zinatarajiwa kukamilika mwaka 2014.

Anatoa wito kwa Wananchi kutumia kanuni bora za kilimo kwa mazao yote,kulima mazao mbadala yanayostahimili ukame kama mtama,muhogo na viazi vitamu na zao la biashara la alizeti kwa maeneo yasiyo na mvua za kutosha.Anasisitiza zaidi Wananchi kutumia chakula kwa uangalifu,kujiwekea akiba na kuacha uuzaji holela ili kuepuka upungufu wa chakula mara kwa mara.           


Written by

0 comments: