Mashindano Ya SHIMUTA 2014 Yafunguliwa Rasmi Jijini Tanga

 
Mkuu wa Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga Mhe.Subira Mgalu amezionya timu ambazo zinashiriki kwenye michuano ya Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma na Kampuni Binafsi Nchini (SHIMUTA) kuacha kuchukua wachezaji ambao sio wafanyakazi  kwani kufanya hivyo kunapunguza ladha ya mashindano hayo.                                

Mgalu aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizundua mashindano ya Shimuta yanayofanyika kwenye viwanja vya Mkwakwani vilivyopo katika Jiji la Tanga na kushirikisha wanamichezo wapatao 500 kutoka mashirika na makampuni mbalimbali hapa nchini.                                                                                      

Alisema kuwa michezo hujenga undugu na furaha baina ya wanamichezo hivyo kuwaingiza wachezaji ambao sio wafanyakazi kwenye mashindano hayo wataondoa maana halisi ya mashindano hayo jambo ambalo linaweza kuwafanya kushindwa kufikia malengo yao waliojiwekea. 

  “Mashindano haya ni ya wanamichezo wafanyakazi…kuna wale wanamichezo ambao sio wafanyakazi ambao wanajulikana kama mamluki au wavamizi kwamba hapa sio mahala pao nawasihi tuchezeshe wafanyakazi halisi ili mshindi apatikane kihalali na sio vyenginevyo….. kwa sababu ni hatari sana kumleta mwanamichezo ambaye sio mfanyakazi kwenye michezo hii anaweza kuvunjika mguu au akifa kwa mfano hatuombei itokee hiyo itakuwaje “Alisema DC Mgalu. 

Aidha alizitaka timu hizo kuacha kuwatumia wachezaji wa aina hiyo kwani wana madhara makubwa hasa pale yanapokuwa yakijitokeza kwa kuzitaka timu zenye utamaduni huo kuhakikisha wanaondokana nao. 

Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya alionekana kukerekwa na baadhi ya menejimenti za Taasisi,Mashirika na makampuni mbalimbali kuwa na utashi wa kutokupenda michezo na wengine kwa kisingizio cha ukosefu wa fedha kuacha kufanya hivyo badala yake wamuunge mkono Rais Jakaya Kikwete katika jitihada zake za kuinua na kuendeleza michezo hapa nchini. 

Akizungumzia waamuzi wanaochezesha mashindano hayo, Mgalu aliwataka kuchezesha kwa haki bila upendeleo kwa kufuata sheria za mchezo husika ili mshindi aweze kupatikana kihalali kwa sababu wakienda kunyume chake wanaweza kusababisha tafrani na manung’uniko kwa baadhi ya timu shiriki. 

Hali kadhalika aliwataka kuhakikisha wanakuwa na nidhamu ya hali ya juu wakati wote wa mashindano ikiwemo kukubaliana na matokeo pindi watakapojikuta wamefungwa wakati wa mashindano hayo. 

Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha Mkuu huyo wa Wilaya, Mwenyekiti wa Shimuta, Khamis Mkanachi alisema kuwa mashindano hayo msimu huu yanashirikisha timu 20 pungufu ya 22 zilizoshiriki mwaka jana mkoani Dodoma ingawa walijiwekea lengo la kuwa na timu 25 hadi 30 mwaka huu . 

Alisema kuwa kupungua kwa idadi ya timu shiriki kunatokana na baadhi ya mashirika kubinafsishwa hali ambayo imepelekea timu nyingi kushindwa kupata nafasi ya kupeleka washiriki wake lakini pamoja na kuwepo hali hiyo shirikisho hilo limendelea na jitihada za ziada kuhakikisha idadi ya timu hizo haipungui bali kuongezeka. 

Aidha alizitaja timu hizo kuwa ni  Shirika la Utangazaji  Tanzania (TBC),Chuo Kikuu Huria(OUT),Chuo cha Elimu ya Biashara(CBE),Kampasi za Mbeya na Dar es Salaam na Mwanza,Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO),Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), ChuoKikuuchaArdhi.

Timu nyengine ambazo zinashiriki mashindano hayo ni Hifadhi ya Taifa Tanzania(TANAPA), Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini(IRDP),Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma(CDA),Chuo Kikuu cha Mzumbe,Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi(MOCU),Chuo kkikuu cha Muhimbili cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS),Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM).

Wengine ambao watashiriki kwenye mashindano hayo ni Baraza la Hifadhi na Usimamizi na Mazingira (NEMC),Shirika la Mzinga,Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Arusha (AICC), Wenyeji wa Mashindano hayo,TANGA CEMENT na Timu mpya kwenye shirikisho hilo ya Bohari ya Madawa(Medical Stores Department(MSD).


  Mhe. Subira Mgalu akifungua rasmi mashindano hayo
 Wakati Mhe. Mgalu akisalimiana na wachezaji wa timu shiriki

Mashindano yalifunguliwa kwa muziki wa kizazi kipya  ujulikanao kama "Kwaito"


Written by

0 comments: