Mkoa Wa Tanga Kuwa Mwenyeji Wa Maadhimisho Ya Siku Ya Utepe Mweupe Kitaifa Machi 15

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Magalula S. Magalula akizungumza  na Waandishi wa Habari  Leo Ofisini kwake 
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Tanga Bw. Ramadhani Kaswa  (Kushoto ) na baadhi ya Waandishi wakati wa mkutano
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakati wa mkutano

Taarifa zaidi

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga kwa niaba ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Muungano wa Utepe Mweupe wa Uzazi Salama Tanzania inapenda kuwatangazia Wananchi  kuwa Mkoa wa Tanga unatarajia kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya Siku ya Utepe Mweupe Kitaifa itakayofanyika Machi 15, Mwaka huu.

Siku ya Utepe Mweupe ni mwendelezo wa juhudi za Serikali katika kupunguza  na kutokomeza kabisa vifo vya akina mama na watoto wachanga.Maadhimisho haya ambayo hufanyika  Machi 15 kila mwaka yana lengo la kuwakumbuka na kuwaenzi wanawake waliopoteza maisha kutokana na matatizo ya uzazi.

Siku hii pia hutumika kujadili mikakati ya kuzuia vifo vingine visitokee. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “WAJIBIKA MAMA NA MTOTO MCHANGA AISHI”.  Kauli mbiu hii inalenga kuhamasisha uwajibikaji wa kila mmoja wetu kuanzia mama mjamzito nwenyewe na familia yake,  jamii na uongozi katika kuhakikisha kuwa hakuna mama wala mtoto mchanga anayepoteza maisha kutokana na sababau ambazo zingeweza kuzuilika.

Aidha, kutakuwepo na shughuli mbalimbali ambazo zitaambatana na maadhimisho haya katika wiki ya kuelekea siku yenyewe ambazo ni pamoja na uchangiaji damu salama, kushiriki katika zoezi la sauti ya jamii,kushiriki katika matembezi ya mshikamano na mkutano siku ya kilele.

 Asilimia 75 ya vifo vingi nchini vinatokana na kutoka damu kwa wingi, maambukizi, shinikizo la damu na utoaji mimba. Wanawake 24 wanafariki kila siku na wengine hupata ulemavu wa kudumu.

Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kuweka mikakati madhubuti ili kupunguza vifo vya mama na mtoto. Kwanza imeelekeza nguvu zake katika kutoa elimu ya uzazi salama na pia imeelekeza Halmashauri zote Mkoani kuwa na kipengele mahususi cha bajeti kinacholenga kuhakikisha kuwa huduma za dharura za uzazi zinapatikana karibu na akina mama na watoto.

Kutokana na juhudi za serikali na wadau mbalimbali, matunda yameshaanza kuonekana miongoni mwetu. Kwa mfano katika Mkoa wa Tanga vifo vya mama na mtoto vimepungua kutoka idadi ya akina mama 101 kati ya wakina mama 45,256 waliojifungua kwa mwaka 2013 hadi kufikia idadi ya akinamama 69 kati ya wakina mama 47,692 waliojifungua kwa mwaka 2014 na idadi ya watoto 429 kati ya watoto 44,852 waliozaliwa  kwa mwaka 2013.   Serikali inaendelea na mapambano kuhakikisha afya ya mama na mtoto iko salama.

Kupunguza vifo vya mama na mtoto vinavyotokana na matatizo wakati wa kujifungua ni  moja ya malengo 8 ya Milenia. Hili ni lengo namba tano ambalo linalenga kupunguza vifo vya akina mama vinavyoyokana na matatizo wakati wa kujifungua kwa asilimia sabini na tano (75%) ifikapo mwaka 2015.

Nawashukuru na kuwapongeza wenzetu wa Utepe Mweupe na wadau wengine kwa kujikita katika kampeni ya uhamasishaji ili kupunguza na kutokomeza vifo vya mama na mtoto.

Napenda kutoa wito kwa wananchi kuhakikisha kuwa kila mmoja anatekeleza wajibu wake ili kuokoa maisha ya mama na mtoto. Pia naviomba vyombo vya habari kuungana na makundi mengine katika jamii kuwa sauti ya akina mama ili kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Kwa pamoja tunaweza kuzuia vifo vya mama na watoto wachanga

“Wajibika Mama na Mtoto Mchanga Waishi”





Written by

0 comments: