Waganga Wakuu Wa Hospitali Za Wilaya Wakumbushwa Kuendelea Kutoa Elimu Ya Mfuko Wa Bima Ya Afya



Wakurugenzi  na Waganga wakuu wa hospitali za Wilaya Mkoani Tanga,  wametakiwa kupita kila  kijiji na kitongoji kutoa elimu ya  kujiunga  na mfuko wa bima ya afya ili kuiwezesha Serikali kufikia  malengo iliyojiwekea.

 Akifungua kikao cha  kujadili mpango  wa mfuko wa Afya ya jamii na kusaini mkataba wa uhamasishaji  wa CHF kwa Wilaya  ya Lushoto na Muheza jana, Katibu Tawala  Mkoa wa Tanga,  Salim Mohammed Chima  alisema elimu ya mfuko wa afya ya jamii inahitajika na  kuwataka viongozi wenye  dhamana kuacha  kujifungia  maofisini.

 Alisema viongozi  wengi wamekuwa  wakishindwa kutekeleza wajibu wao wakiwemo watu wenye  dhamana kushindwa  kuhamasisha jamii kujiunga  na mifuko wa bima  ya afya ya jamii.  

 “Leo nawafungulia  kikao chenu wenyewe  cha kujadili na kuweka mikakati ya jamii kujiunga na mfuko  wa afya ya  jamii---baada ya hapa kila mmoja ahakikishe anatimiza wajibu  wake” alisisitiza Chima

  “Tumekuwa  tukikemea tabia ya wakuu wa  idara na viongozi wenye dhamana kujifungia maofisini na  kushindwa kutekeleza  wajibu wao kwa mujibu wa mikataba ya utumishi wa umma”  alisema

 Alisema tabia ya  viongozi kujifungia  maofisini na kuacha kutekeleza wajibu wao ataikomesha   ikiwemo utoro   pamoja  na muda wa kuingia na kutoka kazini na hivyo kutoa agizo la  kila mmoja kujua  wajibu wake katika kazi.

 Awali akizungumza  katika kikao hicho,  Mganga Mkuu wa Mkoa, Asha Mahita, alipinga vikali ukosefu wa  madawa katika  hospitali zake na kuwabebesha mzigo waganga wa hospitali za  Wilaya kwa uzembe  wa kuacha kuagizia dawa.

 Alisema malalamiko  yanayotoka kwa  wananchi juu ya ukosefu wa madawa ni uzembe wa waganga wakuu  wa hospitali na  hivyo kutoa wito kwa kila mmoja kuhakikisha kituo chake   kinakuwa na dawa za  kutosha ili kuondosha malalamiko kutoka kwa  wananchi.

 “Hakuna ukosefu  wa madawa hospitalini  na ikotokea ni waganga wakuu wa hospitali kufanya uzembe wa  kuacha  kuagizia-----dawa zipo za kutosha na hili nitalishughulikia  mimi mwenyewe”  alisema na kuongeza  

 “Tena natoa wito  kwa wananchi popote  katika Mkoa huu mgonjwa aendapo hospitali na kuelezwa kuwa  hakuna dawa  awasiliane na ofisi yangu au mimi mwenyewe nitalivalia njuga  ” alisema Mahita  

 Kwa kauli hiyo,  Mahita aliwataka  waganga wakuu wa hospitali za Wilaya  kuhakikisha vituo vyao  havipungukiwi na  madawa na kudai kuwa hakuna upungufu huo na yoyote ambaye  atafanya uzembe  atamchukulia hatua. Habari & picha na  Salim Mohammed, Mwananchi 



Written by

0 comments: