Blog ya Mkoa wa Tanga, itakupatia habari mbalimbali, kuhusu Mkoa wetu
Makao Makuu ya Mkoa wa Tanga

Tangazo Ukosefu Wa Muda Wa Maji Jijini Tanga


TANGAZO
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Tanga (TANGA UWASA) inawatangazia wakazi wa jiji la Tanga kuwa kutakuwa na ukosefu wa maji siku ya Alhamisi ya Tarehe 16/4/2015. Hii inatokana na TANESCO kufanya ukarabati wa nguzo katika maeneo ya mitambo ya maji Pande.

Wananchi mnashauriwa kuhifadhi maji ya kutosha. Huduma inatarajiwa kurejea kama kawaida siku ya Ijumaa tarehe 17/4/2015.

Mamlaka inaomba radhi kwa usumbufu utakaojitokeza.


Imetolewa na ofisi ya uhusiano
Tanga uwasa
14/04/2015


Read more

Mkuu Wa Mkoa Wa Tanga Azindua Mpango Mkakati Wa Miaka Mitano Wa Ukimwi Katika Mkoa Wa Tanga Wakati Wa Kikao Cha RCC


Mhe. Magalula Said Magalula , Mkuu wa Mkoa wa Tanga akikata utepe uliofungwa kwenye kitabu kuashiria  uzinduzi wa Mpango wa Miaka mitano wa Ukimwi katika Mkoa wa Tanga wakati wa kikao cha Ushauri cha Mkoa wa Tanga (RCC) kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga mwishoni mwa wiki.

Mada mbalimbali ziliwasilishwa na kujadiliwa katika kikao hicho zikiwemo mada juu ya Taarifa ya upatikananji maji katika Mkoa wa Tanga, taarifa ya Bima ya Afya, taarifa ya hali ya bandari ya Tanga, taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya 2014/2015 na mapenekezo ya bajeti ya mwaka 2015/2016.

Wajumbe walipata nafasi ya kujadiliana jinsi ya kuboresha huduma na vilevile mikakati juu ya kukabiliana na baadhi ya changamoto. Naye Mkuu wa mkoa ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kikao alitoa maelekezo juu ya nini kifanyike ili huduma za wananchi ziweze kuboreshwa. 

    Baadhi ya Wajumbe na waalikwa wakisikiliza mijadala mbalimbali



      Baadhi ya waandishi wa habari wakisikiliza kwa makini



Read more

Jikumbushe Wiki Ya Utepe Mweupe Iliyofanyika Kitaifa Mkoani Tanga

Mkoa wa Tanga umekuwa mwenyeji wa maadhimisho ya Kitaifa ya Utepe Mweupe wa Uzazi salama  yaliyofanyika Machi 15 mwaka huu. Wiki ya Utepe mweupe ilianza tarehe 10 ambapo iliambatana na shughuli mbalimbali zilizolenga kuhakikisha vifo vya mama na mtoto vinavyozuilika vinatokomezwa.

Katika Kupata sauti za Wananchi, Wakazi wa Wilaya tano za Mkoa wa Tanga ambazo ni Kilindi, Handeni, Korogwe, Muheza na Jiji la Tanga walipata fursa ya kutoa maoni yao wakiwawakilisha Watanzania  jinsi gani huduma za afya ziboreshwe  kwa lengo la kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Uhamasishaji wa wananchi ulifanyika kupitia vyombo mbalimbali ya habari. Pichani Bi. Agness Mbwana ambaye ni Mratibu wa Utepe Mweupe Mkoa wa Tanga akizungumza  na wananchi juu ya ushiriki wao katika maadhimisho hayo kupitia radio ya Breeze Fm iliyoko Tanga 
Dr Herriet Mwakilishi kutokaChama cha madaktari Wanawake Tanzania  ( MEWATA )  akifafanua kuhusu dalili za awali za ugonjwa wa saratani ya matiti  na huduma za upimaji wakati wa wiki ya  maadhimisho ya Utepe Mweupe Mkoani kupitia radio ya Breeze Fm
 Vikao vya maandalizi ya Utepe Mweupe viliendelea katika ukumbi mdogo wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga ili kufanikisha zoezi  la maadhimisho kitaifa. Wa pili kulia ni Mganga Mkuu wa mkoa wa Tanga Dr Asha Mahita akifafanua jambo wakati wa kikao
Baadhi ya wajumbe wa vikao vya maandalizi
 Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Magalula Said Magalula akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini  kwake siku mbili kabla ya Kilele cha Maadhimsho  ili kuutaarifu umma kuwa Mkoa ulijiandaa vyema na maandalizi yalikamilika tayari kwa maadhimisho ya siku ya Utepe Mweupe kitaifa Mkoani Tanga
Baadhi ya waandishi wakati wa mkutano
Zoezi la Upimaji wa dalili za awali ya saratani ya matiti liliiendelea . Pichani akinamama wakisubiri kumwona mtalaamu


Read more

Bodi Ya Barabara Mkoa wa Tanga Yaonya Uharibifu Wa Barabara


Wajumbe wa Bodi ya Barabara Mkoa wa Tanga  wamesikitiswa na baadhi ya tabia za Wakazi wa Tanga ambao kwa makusudi kabisa wamekuwa wakifanya uharibifu katika barabara hasa zile zenye lami. Hayo yamebainika katika kikao cha pili  cha bodi ya barabara kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mku wa Tanga siku ya alhamisi ya Machi 2015 kuanzia saa tatu asubuhi.

Akifungua kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Tanga, magalula Said Magalula amesema lengo la kikao cha bodi ya barabaraa ni wadau kupata habari sahihi ya uboreshaji wa barabara katika kupunguza umaskini na kuleta maendeleo kwa wananchi.

“ Tukiweka maazimio mazuri yanayotekelezeka  barabara zetu zinaweza kuwa katika mazingira mazuri na kuhudumia ipasavyo “alisisitiza Magalula

Pia Mhe. Magalula alielekeza Wakurugenzi wa Halmashauri za tanga kuhakikisha wanatoa  elimu kwa wananchi juu ya kutumia vivuko vilivyowekwa barabarani rasmi kwa ajili ya kuvusha mifugo.


Kikao kiliazimia  kuhakikisha uboreshaji katika kudhibiti uzito na mifugo kutembea barabarani.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga , Mhe Magalula Said Magalula akifungua rasmi kikao cha Bodi ya barabara
Meneja wa TANROADS Mhandisi Alfred Ndumbaro Akitoa taarifa ya hali ya barabara katika Mkoa wa Tanga
 Mbunge wa jimbo la  Tanga Mhe Omari Nundu akichangia mada wakati wa Kikao
Baadhi ya wajumbe wa bodi ya Barabara na waalikwa




Read more