Halmashauri ya Jiji la Tanga yaadhimisha siku ya Serikali za Mitaa kwa Amani na Uwajibikaji


Mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Serikali za Mitaa Bw.  Mzamilu Semdoe Naibu Meya wa Jiji la Tanga ( katikati ) wakiyapokea maandamano yaliyofanywa na wakazi wa Jiji la Tanga ( hawapo pichani). Kushoto ni Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Bi. Juliana Malange



Halmashauri ya Jiji la Tanga imeadhimisha siku ya Serikali za Mitaa kwa maonesho ya shughuli mbalimbali zinazotendeka katika Halmashauri hiyo. Kila Idara imepata fursa ya kuelezea shughuli zinazotendeka na ni kwa jinsi gani wananchi hushiriki katika shughuli hizo. Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ni Naibu Meya wa Jiji la Tanga Bw. Mzamilu Semdoe. Kauli mbiu ya Siku ya Serikali za Mitaa mwaka huu inasema “ Amani, Uadilifu na Uwajibikaji kwa wote ni nyenzo muhimu katika Mchakato wa Katiba na Ustawi wa Serikali za Mitaa”

 Siku ya Serikali ya Mitaa  ni siku ambayo huadhimishwa tarehe moja (1) Julai kila mwaka. Lengo kuu ni kuwafanya wananchi kukumbuka na kusherehekea upelekaji wa madaraka kwa wananchi na mafanikio yaliyopatikana kutokana na utekelezaji wa majukumu mbalimbali yaliyofanywa na Serikali za Mitaa na hivyo kuchochea ari ya wananchi kufungamana na Serikali zao ambazo ndizo ishara za wao kupewa madaraka ya kuamua kupanga na kushughulikia maendeleao yao .
 Sherehe hizi zilianza kuadhimishwa tarehe mosi Julai mwaka 2005 katika Mkoa wa Dar es salaam na mwaka huu maadhimisho yanafanyika katika Mkoa wa Morogoro. Utoaji wa madaraka kwa serikali za Mitaa unatokana na Katiba ya jamhuri ya Muungan wa Tanzania ( Ibara ya 145 na 146) na huongozwa na sheria za Serikali za Mitaa za mwaka 1982 sheria no 7,8,9,10 na 11 na sheria no 3 ya mwaka 1983.
Dira ya jiji la Tanga ni kuboresha maisha ya wakazi wa Jiji la Tanga kwa kutumia rasilimali endelevu zilizopo chini ya misingi ya Utawala Bora. Malengo yake makuu ni Kuimarisha na kuboresha utoaji na upatikanaji wa huduma bora za kijamii,  ujenzi wa miundombinu ya Kiuchumi na kijamii, kuboresha mipango na matumizi bora ya ardhi na pia kupunguza maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa wakazi wake.
Kwa upande wa utawala bora, Jiji la Tanga linajivunia kushughulikia kero na malalamiko mbalimbali ya wananchi kwa kupitia fursa ya kufungua milango ya wananchi kufika katika ofisi ya Mstahiki Meya na Mkurgenzi wa Jiji.
Katika siku hii muhimu Jiji la Tanga linatambua umuhimu wa wadau mbalimbali katika Maendeleo ya Jiji. Katika kupambana na gonjwa hatari la UKIMWI, jiji limeendelea kutoa elimu ya juu ya kujikinga na kujilinda na maambukizi ya UKIMWI na pia kuzidi kutoa ushauri nasaha na dawa za kupunguza makali ya UKIMWI kwa walioathirika.
Vilevile Jiji la Tanga limeendelea kuwalipia ada wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu au waliopoteza wazazi wao. Jiji la Tanga ni Jiji lenye fursa nyingi ambazo hutumika kwa ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Jiji na Mkoa kwa ujumla.



 



Wakazi wa Jiji la Tanga wakiwa kwenye maandamano ya Amani kuelekea katika Uwanja wa Tangamano kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Serikali za Mita
Bw. Mkombozi Juma  Afisa Takwimu wa Jiji la Tanga akitoa maelezo mbele ya Mgeni rasmi Naibu Meya Bw.Mzamilu Semdoe juu ya majukumu ya idara ya Mipango ambayo hufanya kazi ya kutafsiri sera mbalimbali za Jiji.
Wakazi wa Tanga wakipata maelezo kutoka idara mbalimbali kuhusiana na shughuli zinazotendeka
 
Mratibu wa Kitendo cha Afya Ngamiani Upande wa akina mama na watoto Bi. Sara Fubusi akitoa maelezo juu namna ya kufunga kizazi kwa upande wa wanaume. Amehamasisha wanaume kuwa mstari wa mbele kufunga uzazi na si kuwaachia akina mama tu
 Bi Rox- Anna Jacob Usiri ambaye ni Fundi Umeme kutoka katika Shule ya sekondari yaTanga Ufundi akitoa maelezo juu ya utendaji kazi wa mfumo wa umeme
Mwanafunzi Augustino M. Kato wa kidato cha sita kutoka Shule ya Sekondari Usagara akitoe maelezo juu ya utalamu wa kilimo bora na magonjwa ya mifugo
 

Afisa Nyuki Bi. Neema John Kiketero akitoa ufafanuzi juu ya ufugaji nyuki na faida ya asali kwa afya ya binadamu


Written by

0 comments: