TASAF II ilivyogeuza changamoto ya uhaba wa chakula kuwa fursa ya uchumi na maendeleo kwa wakazi wa korogwe vijijini
Mzee Rajabu Kufa mlemavu wa
macho na mkazi wa kijiji cha Kwetonge kilichopo kata ya Mashewa mmoja wa wakazi wa Korogwe ambao wamenufaika na mradi wa TASAF II wa ufugaji ng’ombe kupitia kikundi cha
Jipemoyo
Watu wengi duniani
huziona changamoto zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku kuwa ni vikwazo
vya kutofikia malengo waliyojiwekea au wanayopaswa kuyafikia kama binadamu.Ni
watu wachache sana wenye ujasiri wa uthubutu katika maisha yao,hata
ikawapelekea wenye busara kutengeneza msemo wa “uoga wako ndiyo umasikini wako”
wakilenga kuwatia watu moyo na kuwataka kuthubutu
hasa katika masuala yenye changamoto.
Korogwe vijijini yenye
ukubwa wa kilomita za mraba 3544,kata 20,vijiji 122,vitongoji 610 na jumla ya
Wakaazi 242,038 kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2012 ni moja ya jamii iliyojipatia
manufaa kwa kutumia hekima za msemo huo.Korogwe ambayo kilimo ndiyo njia kuu ya
wakaazi wake kujipatia chakula na kipato kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia
2010 imekuwa ikipata mvua za kubahatisha jambo lililopelekea kukabiliwa na
uhaba wa chakula kwa baadhi ya maeneo na maeneo mengine kukumbwa na njaa hata
kupelekea Serikali kupeleka chakula cha msaada.
Pamoja na kukabiliwa na
changamoto hiyo wakaazi hao hawakukaa na kuiangalia njaa ikiharibu maisha yao,badala
yake kwa kutumia fursa zilizopo kama Mfuko wa maendeleo ya Jamii (TASAF II) iliyokuwa
ikitekeleza program zake wilayani humo waliiona ni nafasi nyingine ya kujipatia
maendeleo endelevu,wakaonesha uhitaji wao,wakathubutu na kwa kushirikiana vyema
na Wataalamu wa kada mbalimbali katika Halmashauri, leo hii Wananchi hao wanajivunia mafanikio yao.
Edward Lukinisha ambaye
ni mratibu wa Mfuko wa maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya wilaya ya
Korogwe anaeleza kwa kina jinsi jamii ya wanakorogwe ilivyofaidika na
changamoto ya uhaba wa chakula kwa kuigeuza kuwa fursa ya kiuchumi,na kwamba
sasa Wananchi hao wanayo miradi inayowaingizia kipato na kuwahudumia kila siku
hata wameondokana kabisa na changamoto ya uhaba wa chakula.
“Korogwe ilipotangazwa
kuwa ni moja ya wilaya zinazokabiliwa na uhaba wa chakula,TASAF kama Mfuko wa
kusaidia jamii katika fedha za bajeti kuanzia mwaka 2010 tulikaa na baadhi ya
vijiji na kuwataka waibue miradi ambayo si tu ingekidhi haja ya kumaliza uhaba
wa chakula kwa wakati huo,bali pia ingekuwa ni miradi endelevu hata kwa vizazi
vijavyo” alisema Lukinisha.
Anafafanua kuwa uibuaji
wa miradi hiyo iliyogawanyika katika Sekta kuu tatu za mawasiliano,kilimo na
ufugaji uliolenga kukabiliana na uhaba wa chakula ulikuwa katika sura
mbili,miradi ambayo ingeinufaisha jamii moja kwa moja na miradi ya vikundi.Katika
miradi ya jamii iliwapasa wanajamii wenyewe
kuibua miradi endelevu ambayo ingeinufaisha jamii nzima na kisha kubainisha
kaya zizoathiriwa zaidi na uhaba wa chakula, hivyo wale wenye uwezo wa kufanya
kazi katika kaya hizo ndiyo ambao wangefanya kazi ya ujenzi wa mradi wa jamii
na kulipwa ujira ambao ungewasaidia kupata chakula kwa wakati huo,na wakati huo
huo jamii nayo ingenufaika kwa kupata mradi endelevu.
Moja
ya miradi iliyojengwa wilayani humo kutokana na changamoto hiyo ni barabara ya kijiji cha Changarikwa kilichopo kata ya Magamba
Kwalukonge.Barabara hiyo ilichimbwa kwa urefu wa km 5.5 na upana wa mita 4.5
kwa gharama ya Tsh ml 32 zilizotolewa kwa Wananchi hao kama ujira.
Rukia Hamisi aliyekuwa
mmoja wa washiriki katika ujenzi wa mradi huo anasema barabara hiyo ilianza
kuchimbwa mwaka 2010 na kukamilika 2011,ambapo wataalamu wa Halmashauri
walipima na kutoa ushauri na wao Wananchi walichimba kwa ujira wa Tsh 3000 kwa
kutwa.Fedha ambayo anasema ndiyo ilikuwa ikimsaidia kununua chakula kwa ajili
ya familia yake.
“Barabara hii licha ya kuwa sasa inatusaidia
sana kwa usafirishaji wa mazao yetu,lakini wakati wa kuitengeneza ilitusaidia
sana kwani tulioichimba tulilipwa na fedha ile tuliitumia kwa kununua chakula
kwani hatukupata kabisa mazao kwa mwaka ule.”Anasema Rukia.
Naye bi.Ndatima Shemshi
anaongeza kuwa hapo mwanzo walitembea umbali mrefu kwa miguu kwani ilikuwa ni
vigumu kwa magari kufika kijijini kwao,lakini sasa magari yanaingia hadi
kijijini na kubeba mazao yao kama mahindi na ngwasha ambayo hununuliwa sana na
Wakenya kwa ajili ya kutengenezea biskuti. Hata hivyo mama huyo ana ombi maalum
kwa wadau wenye uwezo kuwekeza zaidi katika barabara hiyo ili iweze kutokezea
kitongoji cha Mlembule katika Mamlaka ya Mji mdogo wa Mombo ambako ndipo kuliko
na barabara kuu inayounganisha nchi za Afrika Mashariki kupitia Arusha.
Sekta ya mawasiliano
inapewa nafasi pia katika kijiji cha Makumba ambapo wanakijiji hao kwa pamoja wanaamua
kujenga kivuko kitakachounganisha kijiji chao na kijiji cha Kazita.Wanakijiji
hao wa Makumba wanapata msukumo wa kujenga kivuko hiki ili kuisaidia jamii kubwa ya wenzao waishio katika kijiji cha
kazita katika vitongoji vya
Magunga na Mtemiroda huku huduma zote muhimu za kijamii zikipatikana kijiji cha
Makumba.
Afisa Mtendaji wa kijiji
cha Makumba Petro Harawa anasema kimsingi vijiji hivyo viwili ni kama kijiji
kimoja cha watu 3069 huku 800 kati yao wanaoishi Kazita wakitenganishwa na
bonde korofi hasa nyakati za mvua,hivyo kama kijiji waliona ni vyema kujenga
kivuko kitakachowaunganisha nyakati zote na ndipo TASAF II ilipowapatia ml 28
na kuanza ujenzi wa kivuko hicho Mei 2012.
Oddos Komba Mwanakijiji wa
Kazita pamoja na kushukuru kwa kuondokana na njaa pia anasifu jitihada za
Serikali za kuimarisha miundombinu ya mawasiliano na uchukuzi vijijini kwa kuielezea
kadhia waliyokuwa wakiipata hapo awali hasa nyakati za masika huku akitolea
mfano wa mwaka 2006 pale wanafunzi wa
kijiji cha kazita waliposhindwa kufanya mtihani wa darasa la nne kutokana na
mvua kubwa kusababisha mahali hapo kutokupitika na kukifikia kijiji cha Makumba
ambako ndiko kuliko na shule.
Sambamba na mawasiliano miradi
mingine iliyokusudiwa kuinufaisha jamii nzima ni ile ya Sekta ya kilimo, ambayo
ni ujenzi wa mifereji ya umwagiliaji.Katika utekelezaji wa kusudio hilo vijiji
vinne ambavyo ni Chekelei, Mazinde Mheza,Mazinde Goha na Makangara Songea
vilinufaika nayo.
Michael Cassian ambaye ni
Mwenyekiti wa kamati ya mradi wa mfereji wa umwagiliaji kijiji cha Chekelei
anasema kuwa wao walipatiwa ml 31 ambazo zimeweza kuchimba na kujenga mfereji wenye urefu wa
mita 200 pamoja na vigawa maji nane.Mradi huo ulioanza kujengwa mwaka 2011
ulikamilika 2012 na tayari Wakulima wameanza kutumia katika msimu huu wa kilimo
wakiwa na matumaini ya kuongeza uzalishaji wa mpunga mara dufu kwa sababu sasa hivi
maji yanafika mashambani kwa uhakika na kwa kipimo kinachotakiwa.
Wakati Chekelei
wakisubiri mavuno, kijiji cha Mazinde Goha wao wanajivunia mavuno ya matunda
aina ya matikiti maji tani sita katika msimu wa kwanza kabisa April 2012 mara
tu baada ya kukamilika kwa mradi wao Januari 2012, na sasa wanajipanga kufanya
kilimo cha pilipilihoho,vitunguu , nyanya na mbogamboga kwa kipindi cha
kiangazi.
Iddi Uledi Mwenyekiti wa
kikundi hicho kiitwacho Songambele anasema walipatiwa ml 8.9 za kuchimba kisima
na ununuzi wa mipira yenye uwezo wa kuhudumia ekari 15 za shamba ambazo walipewa
na kijiji,lakini mpaka sasa wametumia ekari nne tu huku wakiendelea na juhudi
za kufyeka pori lililobaki ili waweze kunufaika zaidi
Katika harakati hizo za
kuwapunguzia Wananchi makali yatokanayo na uhaba wa chakula TASAF II iliwekeza
pia katika sekta ya mifugo huku wanufaika wakishuhudia ya kwamba wamepata
faraja kubwa kwa kupata miradi ya ufugaji ng’ombe na mbuzi kwani mbali ya
kuwapatia kipato pia imeimarisha afya zao kwa kunywa maziwa kila siku.
Miradi hiyo ya ufugaji
ilitolewa kwa vikundi vya watu kumi na nne na kumi na tano kwa vigezo vya
kuathiriwa na uhaba wa chakula na kuwa katika makundi maalumu ambayo ni
walemavu,wajane na wagane, na kwa kuzingatia uwiano wa jinsia.
Rajabu Kufa ni mlemavu wa
macho na mkazi wa kijiji cha Kwetonge kilichopo kata ya Mashewa anasema yeye
amenufaika na mradi wa TASAF II wa ufugaji ng’ombe kupitia kikundi chao cha
Jipemoyo.Anasema ng’ombe wake aliyempa jina la Sara amekuwa mkombozi mkubwa
sana kwake hasa kwa kuzingatia hali yake isiyomwezesha kufanya kazi nyigine
ngumu.
“Ng’ombe huyu ananisaidia
sana kwani napata lita nne kila siku ambazo naziuza kwenye kituo cha maziwa
kilichopo hapa kijijini kwetu,napata pesa za kujikimu mahitaji yangu kutokana
na ng’ombe huyu,hivyo imenisaidia kuondokana na tatizo la kuombaomba na kuwa na
uhakika wa kupata chakula kila siku”.Anasema Kufa.
Mzee huyu anakiri kuwa hawezi
kumhudumia ng’ombe wake yeye mwenyewe,lakini ng’ombe huyo wa asili
aliyeboreshwa ili kutoa maziwa ana afya njema sana.Kufa anasema ng’ombe huyo huhudumiwa na mtoto wake ambaye humkatia
majani ya kutosha kwa siku nzima kila asubuhi kabla ya kwenda kwenye shughuli
zake.
Anaongeza kuwa kijana
wake ana furaha sana kumhudumia ng’ombe huyo kwani amempunguzia majukumu ya
kumgharamia yeye kifedha.Mzee Kufa anaishukuru Serikali kwa kuleta mradi wa TASAF
kwa wahitaji kama yeye na kusema kwake yeye hakika Serikali imemjali sana,pia
anaishukuru Jamii ya kijiji chake kwa kuuona uhitaji wake na kumchagua kupewa ng’ombe huyo.
Naye Bi. Stara Ponda
mjane aishie katika kijiji hicho cha Kwetonge anasema mbali ya ng’ombe wake
kuimarisha afya ya familia yake wakiwemo watoto ambao ni wajukuu zake anaowalea
kwa kunywa maziwa lakini pia ng’ombe huyo humsaidia kupata mahitaji ya shule ya watoto kwa kuuza maziwa kila siku.
Wakati Wananchi hao
wakifurahia ufumbuzi wa tatizo la uhaba wa chakula na kujipatia miradi ya
maendeleo, Afisa Kilimo na Ushirika wa Halmashauri ya wilaya ya Korogwe Kakulu
Lugembe anakiri kuwa katika kipindi cha mitatu maeneo mengi ya Halmashauri yamepitia kipindi
kigumu cha upungufu wa chakula hata kupelekea Serikali kuleta chakula cha
msaada.
“Novemba 2012 Halmashauri
ilipokea tani 111.8 za mahindi ya msaada toka Serikalini na kugawa katika
vijiji 60 vya Kata 12 na Machi 2013 ilipokea tani 350.6 na kugawa katika vijiji
63 vya kata 12” anasema Lugembe.
Hata hivyo anasifu
jitihada zilizochukuliwa na TASAF II kwani zilisisimua uwajibikaji kwa kuwa
suala la upungufu wa chakula husababishwa na mambo mengi ikiwemo uvivu wa mtu
husika,majanga kama mafuriko na
mabadiliko ya tabianchi.Anaielezea hali ya chakula kwa mwaka huu kuwa ina
ishara njema kwani hali ya mazao mashambani ni nzuri ukiachilia mbali kata nne
tu za Mashewa,Mkomazi,Mkalamo na Mazinde.
Lugembe anawapongeza
zaidi Wananchi waliochagua ujenzi wa mifereji ya umwagiliaji kwa kueleza kuwa
kwa sasa kilimo cha uhakika na tija ni cha umwagiliaji kutokana na mabadiliko
ya hali ya hewa yasiyotabirika.Anaeleza kuwa hata Halmashauri imeelekeza nguvu
zake katika ujenzi wa skimu za umwagiliaji ikiwemo ya Kwemkumbo katika mamlaka
ya mji mdogo Mombo na katika bonde la Mkomazi ambazo zinatarajiwa kukamilika
mwaka 2014.
Anatoa wito kwa Wananchi
kutumia kanuni bora za kilimo kwa mazao yote,kulima mazao mbadala
yanayostahimili ukame kama mtama,muhogo na viazi vitamu na zao la biashara la alizeti
kwa maeneo yasiyo na mvua za kutosha.Anasisitiza zaidi Wananchi kutumia chakula
kwa uangalifu,kujiwekea akiba na kuacha uuzaji holela ili kuepuka upungufu wa
chakula mara kwa mara.
0 comments: