RC Tanga Ashauri Chanjo Ya Surua Na Rubella Kwa Watoto Haina Madhara Kwa Binadamu Ni Kinga Kwa Afya Bora
Mkoa wa Tanga kama ilivyo kwa Mikoa mingine ya Tanzania
iko kwenye maandalizi ya kampeni shirikishi ya chanjo ya Surua na Rubella. Maandalizi hayo ni pamoja na kuelimisha na kuhamasisha wakazi wote wa Tanga kwa ngazi ya Mkoa,
Wilaya,Tarafa, Kata,Vitongoji na vijiji kujitokeza kwa wingi na kuwapeleka
watoto wao katika vituo vya afya tarehe 18 hadi 24 Oktoba ili kupata chanjo ya magonjwa hatari ya Surua
na Rubella.
Sambamba na chanjo ya Surua na Rubella kwa watoto wenye
umri wa miezi tisa (9) na chini ya miaka 15, zoezi hilo la chanjo linalenga
kutoa vidonge vya vitamin A kwa watoto wote wenye umri wa miezi 6 mpaka miezi
59 , dawa za minyoo, kwa watoto wote wenye umri wa miezi 12 hadi miezi 59 na dawa za matende na mabusha kwa watoto miaka mitano (5) na kuendelea .
Akizungumza wakati wa kufungua kikao cha wadau wa afya
(PHC) kilichofanyika leo katika ukumbi
wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Chiku Gallawa, Mkuu wa Mkoa
wa Tanga ametoa wito kwa wadau wote wa Afya Mkoani Tanga kuweka jitihada za
kuhakikisha Mkoa wa Tanga unaendelea kufanya vizuri katika zoezi la Chanjo.
Mkoa wa Tanga ambao
kwa takribani miaka mitatu mfululizo umeendelea kufanya vizuri katika utoaji
chanjo kwa ngazi ya kitaifa kwa kushika nafasi ya kwanza, umejiwekea mikakati
mizuri ya kutoa elimu na hamasa kwa wazazi kuhakikisha wanawapatia watoto wao
chanjo muhimu.
“Ndugu washiriki, nashauri tujipange kutoa elimu na
hamasa kwa wananchi wetu walio katika maeneo yetu ili waweze kujitokeza kwa
wingi katika zoezi la Chanjo. Jitihada ziwekwe katika kuwaelimisha kuwa chanjo
hizi hazina madhara yeyote kwa binadamu badala yake ni kinga kwao.”amesisitiza
Mhe. Gallawa.
Naye mwakilishi kutoka Wizara ya Ustawi wa Jamii Dr.
Maduhu amesema Wizara yake imejipanga vyema katika kusambaza vifaa tiba na
elimu kwa wahudumu ili kuhakikisha zoezi hilo linaenda vizuri.
Kampeni ya chanjo kitaifa itaanza rasmi tarehe 18 hadi 25, Octoba na kauli mbiu ya mwaka huu ni “Linda , Okoa Maisha Zuia Ulemavu – Kamilisha Chanjo”
Dr. Maduhu Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii akieleza juu ya jinsi wizara yake ilivyojiandaa kukamilisha zoezi la chanjo Mkoani Tanga. kulia ni Mkuu wa Mkoa wa tanga Mhe. Chiku Gallawa na Katibu Tawala Mkoa Bw. Salum Mohamed Chima.
Baadhi ya wajumbe wa kikao wakisiliza kwa makini
0 comments: