Semina ya UKIMWI kwa makundi maalumu yalenga Uhamasishaji wa Elimu kwa Jamii
Washiriki wa semina ya masuala ya UKIMWI kutoka
makundi ya Wanahabari, Vijana na Viongozi wa dini wakisikiliza moja ya maada
zilizowasilishwa.
Ni jambo lisilopingika
kuwa kundi la wanahabari, Vijana na Viongozi wa dini ni makundi yenye nafasi
muhimu sana katika jamii hususani katika
kufikisha ujumbe husika.
Umuhimu huu ndio
uliopelekea Mratibu wa Masuala ya UKIMWI wa Jiji la Tanga Bw. Moses Kisibo
kuona umuhimu wa kuyakutanisha makundi haya ili kuyapatia elimu juu ya Ugonjwa
wa hatari wa UKIMWI na baadaye makundi haya kujipanga kwa pamoja na kuazimia ni
nini kifanyike ili haya makundi yakawe chachu ya kutoa elimu kwa jamii juu ya
kupunguza maambukizi mapya ya UKIMWI.
Semina ya UKIMWI kwa
makundi maalumu imefanyika mwanzoni mwa wiki katika ukumbi wa mikutano wa ofisi
za Mipango miji ambapo makundi haya yameaswa kuepuka unyanyapaa wa wagonjwa wa
UKIMWI kwa kuendelea kuwahudumia kwa upendo.
Aidha elimu imetolewa kuwa
ni vyema kupata elimu kutoka kwa wataalamu
kuhusu taratibu sahihi za kumhudumia mgonjwa wa UKIMWI ili kuepuka maambikizi
wakati wa kumhudumia mgonjwa.
Akizungumzia tabia na
mazingira hatarishi kwa maambukizi ya UKIMWI, mwezeshaji wa elimu ihusuyo
UKIMWI Bw.Desideri Joseph amebainisha kuwa ngono isiyo salama, kuwa na wapenzi wengi,mila
potofu, ukosefu wa elimu na na upataji habari, ukosefu wa upatikanaji huduma ya
afya, ukosefu wa ajira na tabia ya kunywa pombe kupita kiasi ni miongoni mwa
mazingira hatarishi.
Hata hivyo makundi haya
maalumu ya wanahabari, Vijana na Viongozi wa dini wameamua kujiwekea mikakati
na maazimio ni kwa jinsi gani yangetumia nafasi yaliyonayo katika jamii ili
kutoa elimu juu ya ugonjwa wa UKIMWI kwa lengo la kupunguza maambukizi.
Wanahabari walikubaliana
kutumia kalamu zao na kuelekeza nguvu zao katika kuandaa machapisho na vipindi
vya radio na televisheni ambavyo vitalenga mahusus i elimu jinsi ya kujikinga
na maambukizi mapya ya huu ugonjwa hatari, elimu ya jinsi ya kuishi bila
kujinyanyapaa wala kuwanyanyapaa wengine na pia kuitaarifu jamii juu ya tafiti
mpya juu ya ugonjwa wa UKIMWI.
Nalo kundi la vijana limeona
ni muda mwafaka wa wao kutumia elimu waliyoipata juu ya masuala ya UKIMWI na kuazimia
kuipeleka kwa jamii hasa kwa kupitia mabaraza ya vijana.
Vilevile Viongozi wa dini
nao hawakubaki nyuma bali wameweka azmio la kutumia majukwaa ya Misikiti na
Makanisa kupasha habari na kutoa elimu
ya UMIKWI kwa waumini wao.
Ni wito kwa kila mmoja kuamua kuacha vitendo hatarishi
vitakavyopelekea kupata maambukizi mapya ya UKIMWI kwani ugonjwa huu hatari
hauchagui elimu, cheo, Umri wala Imani ya mtu. Imethibitika kuwa kinga pekee ya
kuepuka maambukizi haya ni kuacha ngono
kabisa kwa wale ambao hawako kwenye ndoa na pia walioko kwenye ndoa kuendelea
kuwa waaminifu kwa wapenzi wao.
Mratibu wa Masuala ya UKIMWI wa Jiji la Tanga Bw.
Moses Kisibo akifafanua jambo wakati wa semina
Kundi la wanahabari kutoka vyombo vya habari mbalimbali
wakijadiliana ni nini kifanyike ili
kuweza kuielemisha jamii juu ya masuala yahusuyo UKIMWI.
Kundi la Vijana wakijadiliana ni nini kifanyike ili kuweza kuielemisha
jamii juu ya masuala yahusuyo UKIMWI
Kundi la Viongozi wa dini wakijadiliana ni nini kifanyike ili kuweza kuielemisha
jamii juu ya masuala yahusuyo UKIMWI
jamii inatakiwa kubadili tabia juu ya ugonjwa wa UKIMWI badala ya kusubili Serikali na kuilaumu, kwani ugonjwa wa UKIMWI, unahitaji mikakati kuanzia ngazi ya mtu binafsi, familia, kaya makundi ya kijamii ndio serikali kuwekea mkazo katika mikakati hiyo
ReplyDeleteMOSES KISIBO
BOX 178
TANGA JIJI