Viongozi wa Dini Mkoani Tanga waaswa Kuhubiri Upendo na Kupigania Amani.



Wahitimu wa mafunzo ya lugha ya Kiingereza na Kompyuta ambao ni viongozi wa dini ya Kikristo na Dini ya Kiislamu wameaswa  kuihubiri Amani ili kuupatia Mkoa wa Tanga fursa ya kukua kiuchumi. Hayo yamesemwa na Mgeni rasmi Mhe. Chiku Gallawa, Mkuu wa Mkoa wa Tanga wakati wa mahafali  katika chuo cha Mafunzo cha Novelty Jijini Tanga.

Akizungumza wakati wa  mahafali  amesisitiza “ Viongozi wa Dini msichoke  kukemea vitendo vya uvunjifu wa amani kwani bila amani hatutakuwa na maendeleo na hakuna atakayepona endapo amani itatoweka Mkoani na Nchini kwetu”

Mhe. Gallawa pia ametoa wito kwa viongozi  wa dini na wananchi  kwa ujumla kutokubali kugeuzwa watumwa katika nchi yao wenyewe bali  kupinga  kwa nguvu hoja za wale wote wanaonekana kuwa na nia  ya kuvuruga amani.

Aidha  Mhe  Gallawa amekipongeza chuo cha mafunzo cha Novelty kwa jitihada walizozionyesha kwa kuamua kudhamini mafunzo ya Kompyuta na kiingereza  na kuyatoa bure kwa viongozi wa dini ya kikristo  na dini ya kiislamu. Chuo cha mafunzo Novety kimeanziswhwa mwaka 1998 na kimeendelea kutoa mafunzo mbalimbali kwa vijana yakiwemo mafunzo ya Elimu ya Ukimwi, madhara ya madawa ya kulevya, kozi ya kiingereza , Kompyuta n.k

Nao viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu ( Wahitimu) wakitoa risala yao kwa mgeni rasmi wameonyesha furaha yao kwa kupata mafunzo hayo na kukiri kuwa sasa wana fursa nzuri ya kuweza kusoma na kuongeza elimu ya dini zao kwa kutumia vitabu vya lugha ya kiingereza na Kompyuta. Jumla ya Viongozi wa Dini 43 walianza mafunzo hayo June 15, 2013 na wamehitimu Viongozi 30 na wengine 13 wameshindwa kuhitimu kutokana na sababu mbalimbali.

Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Tanga Bw. Bernard P. Marcelline akitoa utambulisho wa viongozi wa Mkoa wakati wa mahafali
 Mkuu wa Mkoa Chiku Gallawa Mhe. Chiku Gallawa akikabidhi vyeti kwa wahitimu

Picha ya pamoja ya Mkuu wa Mkoa akiwa na viongozi wa dini kimkoa
 ( waliokaa) na viongozi wa dini wa dini ya Kikristo na Kiislamu
 ( wahitimu wakiwa na vyeti vyao )




Written by

0 comments: