Kilindi kuinua pato la wananchi kwa kilimo cha maembe ya kisasa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kilindi mkoani Tanga Daudi Mayeji amesema kuwa Halmashauri yake imejipanga kuongeza pato la Mwananchi mmoja mmoja  kutoka Tsh 800,000  hadi 1,500,000/- kwa mwaka kufikia mwaka 2015 kwa kuanzisha kilimo maalumu cha maembe ya kisasa yatakayokuwa yakisafirishwa nje ya nchi.

Mayeji  aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wilayani Handeni katika mahojiano maalum na waandishi wa habari mara baada ya kuwasilisha mpango mkakati wa Halmashauri yake wa  program ya tekeleza sasa kwa matokeo makubwa (BRN) katika kikao cha kazi kilichojumuisha watendaji wa sekretarieti ya mkoa, wakuu wa wilaya,Makatibu tawala,Wakurugenzi, maofisa tarafa na watendaji wa Halmashauri kilicholenga  kuharakisha utekelezaji wa mpango wa BRN.

Alisema kuwa Halmashauri yake imetenga ekari 100 katika kijiji cha Mvungwe ambazo zimekwishapimwa na tayari wamekwishaunda ushirika wa wanachama watakaojihusisha na kilimo hicho ambao pia wamekwishauombea uanachama katika umoja wa kitaifa wa wakulima wa maembe “Mango growers” ambao husaidia kutafuta masoko ya maembe nje ya nchi na kuuza zaidi katika nchi za mashariki ya kati.

Aliongeza kuwa kwa mujibu wa “Mango growers” mahitaji ya maembe katika soko la nje ni makubwa sana kuliko uzalishaji  na hivyo hali hiyo inatoa uhakika wa soko kwa wakulima hao ambapo kwa muda mfupi wa kati ya miaka miwili  hadi mitatu watashuhudia mabadiliko chanya ya vipato vyao kupitia mradi huo ambao utawekewa miundombinu yote muhimu kama barabara,ofisi na maghala na hivyo kuufanya kufikika kwa urahisi .

Aidha alifafanua kuwa kila mwanachama wa ushirika huo amepatiwa ekari moja ambayo itamwezesha kupata Tsh 250,000 kwa kila mwembe mmoja.Wanachama hao wametakiwa tu kuchangia nguvu ya kusafisha mashamba yao na kulipia ada ya uanachama ili kujenga hisia ya umiliki na kisha Halmashauri kuwagawia bure miche ya miembe ya kisasa ambayo iliinunua kutoka chuo kikuu cha kilimo cha Sokoine (SUA) sambamba na kutoa utaalamu wa kuipanda na kuitunza kupitia maafisa ugani wa Halmashauri.


Mkurugenzi Mtendaji (W) Kilindi Daudi Mayeji akijibu maswali ya waandishi wa Habari nje ya ukumbi wa Hill town view hotel mjini Handeni mara baada ya kikao kazi cha BRN.

kikundi cha  sanaa na maonesho cha Mgambo JKT cha Handeni kikitumbuiza kabla ya kuanza kwa kikao kazi katika ukumbi wa Hill Town view Hotel.
Baadhi ya Wenyeviti wa Halmashauri za wilaya na miji mkoani Tanga wakifuatilia taarifa zilizowasilishwa katika kikao kazi cha kuharakisha BRN. 



Written by

0 comments: