Lushoto waandaa mwarobaini wa kudhibiti Wafanyabiashara Walanguzi wa Viazi.


Halmashauri  ya wilaya ya Lushoto imeanza mchakato wa ujenzi wa vituo viwili kwa ajili ya kufanya mnada wa wazi wa zao la viazi mviringo ili kudhibiti wachuuzi na wafanyabishara walanguzi.

Hatua hiyo inalengwa kudhibiti wizi unaofanywa sasa na wafanyabishara wanaofika wilayani humo na kuwarubuni wakulima kwa kununua zao hilo kwa bei ndogo au likiwa shambani kabla ya kuvunwa n hivyo kusababisha waendelee kuwa maskini.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Jumanne Shauri ameyasema hayo  mwishoni mwa wiki katika mahojiano maalum na kusema utekelezaji wa mradi huo unalenga kuwawezesha wakulima wa viazi na mboga mboga kupata matokeo ya haraka na yenye kuleta tija katika shughuli zao hizo ili wajikwamue ki uchumi.

“Lengo la mradi huu ni kuongeza thamani kwa zao la viazi mviringo na mboga kwa hiyo tunajenga vituo vya  kukusanya na kuchambulia viazi kulingana na aina na ukubwa katika maeneo mawili ya Maringo Lukozi na Lushoto mjini ambako kila moja litakuwa na “cold room” kwa ajili ya kuvihifadhi kabla ya kununuliwa”, alisema na kuongeza.

“Tutatumia wakulima watakaokwenda kutafuta mazao na kuyakusanya katika vituo maalum na baada ya kufikishwa hapo vituoni mnada wa hadhara utafanywa kwa bei watakayokubaliana wakulima na sio kutoa uhuru kama ilivyo sasa ya kati ya sh. 5,000 na 6,000 kwa debe ambayo ki msingi haina maslahi kwa mkulima”,alisema.

Akizungumzia mnada huo wa viazi katika vituo hivyo alisema utaendeshwa na wakulima wenyewe wa viazi mviringo na mboga mboga kupitia vyama vyao badala ya kutumia wachuuzi na walanguzi kama wanavyofana hivi sasa.

“Lengo ni kumsaidia mkulima kukuza kipato chake kutoka wastani wa sh. 1,026,000 ya sasa kwa mkazi wa Tanga hadi kufikia wastani wa sh. 1,500, 000 ifikapo mwaka 2015 na hili tunaamini litafikiwa kwasababu limo katika vipaumbele vya mpango wa uwiano wa miaka mitano wa mkoa”, alisema.

Aidha, alisema katika kutekeleza mradi huo chama hicho cha wakulima kinashirikiana na shirika la Oxfam Tanzania, wizara ya kilimo ambayo imewapatia sh. Milioni 200 kwa ajili ya kujenga vyumba vya kuhifadhia, halmashauri sh. Milioni 32 kwa ajili ya kujenga vituo vya kukusanyia mazao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Lushoto Jumanne Shauri akitoa ufafanuzi wa mpango mkakati wa Halmashauri yake kwa waandishi wa Habari mara baada ya kumalizika kwa kikao kazi hicho.


Written by

0 comments: