Watakiwa kutumia muda vizuri na kutenda kwa haki
Mkuu wa mkoa wa Tanga, Chiku Gallawa amewataka wanasiasa na
watendaji wa serikali katika ngazi mbalimbali mkoani hapa kuacha tabia ya
kufanya kazi zao kwa mazoea badala yake watumie muda vizuri na kuhakikisha
wanamtendea haki kila mtu wanayemhudumia bila kujali alivyo.
Ametoa mwito huo mwishoni mwa wiki wakati akifunga mkutano wa
pamoja (Inter Council Meeting) uliojumuisha wakuu wa wilaya, makatibu tawala,
wenyeviti wa halmshauri, wakurugenzi watendaji, maofisa mipango, utumishi na
maofisa tarafa kutoka wilaya zote nane zinazounda mkoa huo.
Lengo la mkutano huo maalum wa kazi uliofanyika kwa siku mbili
wilayani Handeni lilikuwa ni kuwaleta pamoja watendaji hao kubadilishana
uzoefu, kuondoa tofauti na kujengana ili waweze kuwa timu moja katika
utendajikazi itakayoharakisha maendeleo mkoani humo.
“Ndugu zangu tumepewa dhamana kubwa ya kuongoza wakazi wa Tanga
kwahiyo kila mmoja wetu mahali alipo yampasa kujitambua na kubadilisha mazoea
mabaya kwa kuamua mwaka huu kutenda kwa haki na kutumia muda wa kazi vizuri kwa
ajili ya kuleta mabadiliko chanya ya kijamii na kiuchumi yatakayomfanya kila
mwananchi kufurahia maisha alipo”, alisema na kuongeza.
“Ni vema tukaona mbali tukaongeza ubunifu na pia tufikirie zaidi
na kujaribu kutumia kwa hekima fursa zilizopo pamoja na rasilimali fedha
tunazopewa na serikali kwa ajili ya kuondoa kero zinazowakabili wananchi ili
wapate maendeleo ya kweli”.
Akizungumzia hali ya Usalama na Amani iliyopo sasa alisema kuna
haja kwa wao kuendelea kuwashauri na kuwasaidia wananchi kwa kuwapa miongozo
itakayowawezesha kufanya shughuli zao za kilimo na ufugaji kwa tija ili
wajikwamue ki uchumi badala ya kuwatelekeza.
“Naomba tusijaribu kutengeneza “gap” kubwa kati ya wananchi walionacho
na wale wasionacho hii ni mbaya sana kwa kuwa uzoefu unaonesha hiyo ni miongoni
mwa sababu zinazochochea wananchi kuleta machafuko kwenye jamii.
“Siku zote mahali
penye njaa na maradhi hapana utulivu kwa hivyo ni jukumu letu sisi viongozi
hapa kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na maendeleo yatakayosababisha
afurahie maisha na ndipo tutaweza wote kuishi mahali penye amani na utulivu”,
alisema Mh.Gallawa.
Aidha, akizungumzia namna ya kuwezesha wananchi ki uchumi
aliwataka wakurugenzi watendaji wa halmashauri zote 11 za mkoani humo
kuhakikisha wanatenga asilimia 10 ya makusanyo yao kwa ajili ya kuviwezesha
mitaji vikundi vya vijana na wanawake.
“Wakurugenzi acheni kupata kigugumizi wakati wa kutoa ile
asilimia 5 kwa ajili ya mfuko wa vijana na ile 5 nyingine ya wanawake hiyo ni
haki yao kwa mujibu wa sheria kadhalika na ile ruzuku kutoka serikalini kwa
ajili ya vijiji nayo wapeni wapange shughuli zao za kuwakwamua kiuchumi acheni
kuzipangia matumizi mengine ya ofisi”, alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya
Korogwe Lucas Mweri akiwasilisha mpango mkakati wa Halmashauri yake kuhusiana
na utekelezaji wa BRN.
0 comments: