RC na RAS nchini kujengewa uwezo


 Wakuu wa Mikoa nchini wameaswa kufahamiana  kama viongozi ili kubadilishana uzoefu wa kujenga mtandao wa mawasiliano na mahusiano kwa ajili ya kupashana habari na kushauriana.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ally Idd wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Wakuu wa Mikoa (RC) na Makatibu Tawala Mikoa (RAS) nchini leo jijini Dar es salaam.
“Jengeni mshikamano wa mahusiano katika utendaji kazi wenu mkiimarisha maelewano miongoni mwenu mtarahisisha utendaji na kuepuka migogoro isiyo ya lazima” alisema Balozi Seif.
Balozi Seif aliendelea kusema, “Tumieni nafasi hii kufahamiana muweze kujenga mtandao wa mahusiano, mawasiliano mkiimarisha mashirikiano ili kuleta maendeleo katika maeneo yenu ya kazi kwa manufaa ya wananchi”.
Balozi Seif alisema kuwa kila kazi inachangamoto zake, katika kutekeleza majukumu yao vizuri na kubainisha kuwa viongozi hawa baadhi yao wamekuwa na misuguano ya hapa na pale ambayo husababishwa na mawasiliano yasiyoridhisha.
Balozi Seif alisisitiza kuwa dawa ya misuguano hiyo itapatikana kupitia mafunzo hayo ya siku tatu ambapo viongozi hao watakumbushwa mengi waliyoyasahau, watapata mengi ya kujifunza, kujikumbusha na kujinoa ili kuhuisha uhai wa utekelezaji wa majukumu yao ambao utaleta mshikamano na umoja miogoni mwa watendaji hao.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Hawa Ghasia alipokuwa akimkaribisha Mgeni Rasmi alisema kuwa mafunzo hayo yataimarisha mahusiano na mawasiliano ya viongozi hao katika kutekeleza majukumu yao ili yapate tija iliyokusudiwa.
Waziri Ghasia amewaasa viongozi hao kuwa wasipofanya kazi kama timu hawawezi kupata tija katika maeneo yao ya kazi hasa katika kuwaletea maendeleo wananchi wanaowaongoza na nchi  kwa ujumla.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wakuu wa Mikoa ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro akimshukuru  na kumhakikishia Mgeni Rasmi Balozi Seif kuwa wanamatumaini makubwa kuimarisha mahusiano kati yao vilevile na wanasiasa wote na kuahidi kuwa watatoa huduma bora zaidi.  
 Aidha, mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma viongozi wao hawatashiriki mkutano huo kwa kuwa kwa sasa wapo kwenye ratiba ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete katika mikoa hiyo.
Wakuu wa mikoa hiyo waunganishwa kupata mfunzo kama hayo na Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa mikoa ya Zanzibar ambayo itapangwa kufanyika hapo baadaye ambapo Serkali ya Mapinduzi imeahidi kushirikiana na Tasisi ya Uongozi kutoa mafunzo hayo.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Taasisi  ya Uongozi kwa lengo la kuwawezesha viongozi hao kufahamu kwa kina umuhimu wa mawasiliano bora baina ya viongozi wa kisiasa na watendaji Wakuu wa ngazi ya Mkoa ili kuimarisha utoaji bora wa huduma  kwa wananchi.
Habari & picha na Eleuteri Mangi-MAELEZO








Written by

0 comments: