Serikali Kuanzisha Mfumo Wa Kudhibiti Matumizi Ya Fedha Sekta Ya Afya .


Dkt Anna Nswilla akiwasilisha mada jinsi mfumo wa utoaji ripoti Sekta ya Afya unavyofanya kazi katika Mkoa wa Tanga
Katibu wa Afya Mkoa Tanga Bw. Patric Mchami akisisitiza umuhimu wa matumizi ya mfumo wa HRIS katika sekta ya afya

Serikali ipo mbioni kuondoa urasimu wa matumizi ya fedha kwa kufunga mfumo maalum ulioboreshwa utakaoonesha kwa pamoja kiasi,matumizi  bakaa na kutoa ripoti  ili   kudhibiti matumizi ya fedha katika sekta ya afya  na hivyo kuondokana na tatizo la matumizi yasiyomo kwenye mpango wa bajeti husika.

Hayo yamesemwa na Mratibu wa Huduma za Afya  ngazi ya Halmashauri katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dkt Anna Nswilla wakati wa kikao cha kuweka mikakati ya kuboresha sekta ya afya kwa mwaka 2014/2015 kilichofanyika mwishoni mwa wiki wilayani Lushoto kwa kuwahusisha wadau wa sekta ya afya wakiwemo waganga wakuu wa wilaya zote za mkoa wa Tanga.

Dkt.Nswilla alisema mfumo huo ambao utafanya kazi kwa pamoja na mfumo wa sasa wa ‘epicor’ ambao pia madaktari watafungiwa katika ofisi zao ili kujua kiasi cha fedha kilichoingia utaondoa tatizo la kutokutumia fedha kwa wakati kwa sababu utawalazimisha kutumia fedha na kutoa ripoti kwa mujibu wa mpango uliopo na hivyo kuzuia matumizi yasiyo rasmi.

Aidha  Dkt Nswilla aliwataka Madaktari  wa Wilaya kupanga mipango ya bajeti inayoendana na mahitaji ya jamii wanazozihudumia huku akiwasisitiza kutoa ushauri wa kitaalamu na kufanya kazi kwa weledi na kwa  mujibu wa taaluma  ili kuboresha sekta ya afya nchini.

Katika hatua nyingine Katibu wa afya Mkoa wa Tanga Patric Mchami aliwataka Madaktari hao kutumia mfumo wa taarifa za watumishi ‘HRIS’ ili kujua idadi,mahitaji na upungufu wa watumishi katika wilaya zao jambo litakaloisaidia wizara kujua taarifa za watumishi wake na hivyo kuelekeza nguvu kuliko na watumishi wachache.

Mchami pia aliwataka Madaktari kuwajali watumishi wakada hiyo ngazi ya  chini kwa kuwapatia motisha ikiwemo kuwalipa stahili zao kwa wakati na kutoa kipaumbele kwa madeni yao kila fedha inapopatikana.

Mkutano huo uliofanyika kwa siku mbili ulizijumuisha  ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa,Waganga Wakuu wa Wilaya,Wenyeviti wa Bodi ya Afya na Wadau wa Sekta ya Afya kama,WHO, MSD,kfw, WEI na Giz. Habari & Picha na Fatina Mfalingundi, Afisa Habari Halmashauri ya Wilaya Korogwe
 

Written by

0 comments: