Waganga Wakuu Wa Hospitali Za Wilaya Wakumbushwa Kuendelea Kutoa Elimu Ya Mfuko Wa Bima Ya Afya
Wakurugenzi na Waganga wakuu wa hospitali za Wilaya Mkoani
Tanga, wametakiwa kupita kila kijiji na kitongoji kutoa elimu ya
kujiunga na mfuko wa bima ya afya ili
kuiwezesha Serikali kufikia malengo
iliyojiwekea.
Akifungua kikao cha kujadili mpango wa mfuko wa Afya ya jamii na kusaini mkataba
wa uhamasishaji wa CHF kwa Wilaya ya Lushoto na Muheza jana, Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Salim Mohammed Chima alisema elimu ya mfuko wa afya ya jamii
inahitajika na kuwataka viongozi wenye dhamana kuacha kujifungia maofisini.
Alisema viongozi wengi wamekuwa wakishindwa kutekeleza wajibu wao wakiwemo
watu wenye dhamana kushindwa
kuhamasisha jamii kujiunga na
mifuko wa bima ya afya ya jamii.
“Leo nawafungulia kikao chenu wenyewe cha kujadili na kuweka mikakati ya jamii
kujiunga na mfuko wa afya ya jamii---baada ya hapa kila mmoja ahakikishe
anatimiza wajibu wake” alisisitiza Chima
“Tumekuwa
tukikemea tabia ya wakuu wa idara
na viongozi wenye dhamana kujifungia maofisini na kushindwa kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa mikataba ya utumishi
wa umma” alisema
Alisema tabia ya viongozi kujifungia maofisini na kuacha kutekeleza wajibu wao
ataikomesha ikiwemo utoro pamoja na muda wa kuingia na kutoka kazini na hivyo
kutoa agizo la kila mmoja kujua wajibu wake katika kazi.
Awali akizungumza katika kikao hicho, Mganga Mkuu wa Mkoa, Asha Mahita, alipinga
vikali ukosefu wa madawa katika hospitali zake na kuwabebesha mzigo waganga wa
hospitali za Wilaya kwa uzembe wa kuacha kuagizia dawa.
Alisema malalamiko yanayotoka kwa wananchi juu ya ukosefu wa madawa ni uzembe wa
waganga wakuu wa hospitali na hivyo kutoa wito kwa kila mmoja kuhakikisha
kituo chake kinakuwa na dawa za kutosha ili kuondosha malalamiko kutoka kwa wananchi.
“Hakuna ukosefu wa madawa hospitalini na ikotokea ni waganga wakuu wa hospitali
kufanya uzembe wa kuacha kuagizia-----dawa zipo za kutosha na hili
nitalishughulikia mimi mwenyewe” alisema na kuongeza
“Tena natoa wito kwa wananchi popote katika Mkoa huu mgonjwa aendapo hospitali na
kuelezwa kuwa hakuna dawa awasiliane na ofisi yangu au mimi mwenyewe
nitalivalia njuga ” alisema Mahita
0 comments: