Blog ya Mkoa wa Tanga, itakupatia habari mbalimbali, kuhusu Mkoa wetu
Makao Makuu ya Mkoa wa Tanga

Mahakama Tanga Yazindua Bodi Mpya Ya Parole


 Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Magalula Said Magalula amewataka wajumbe wa Bodi ya Paroli Mkoa  kutenda kazi kwa kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa ili kutenda haki na kuepuka ushawishi wa namna yeyote katika kupokea na kuomba rushwa.

Hayo yamesemwa mapema siku ya alhamisi ya machi 12 mwaka huu wakati wa uzindua rasmi Bodi ya Parole Mkoa tukio lililofanyika katika ofisi za Magereza Mkoa.

 Lengo la Bodi hii ni  kuwajadili  wafungwa wenye sifa  za kuweza kuachiliwa huru baada ya kutimiza vigezo ambavyo vimeainishwa kwenye  sheria namba 25  ya Paroli ya mwaka 1994 na kufanyiwa mabadiliko mwaka 2002.

Sheria husika imeweza kuanisha ni aina gani ya makosa ambayo mfungwa anaweza kupata fursa ya kuingia kwenye mpango wa Paroli . Pamoja na makosa hayo mfungwa hawezi kuingizwa kwenye utaratibu wa Paroli endapo amepatikana na kosa la unyanyanyi wa siraha, madawa ya kulevya, kulawiti, kubaka na mauaji ya kukusudia.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa sheria ya parole tangu utekelezaji wake mwaka 2003, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tanga Kamishina Agustino Mboje amesema tayari wafungwa 331 wameshaachiliwa huru kwa utaratibu wa parole, wafungwa 305 wamemaliza vifungo vyao salama na wafungwa 26 bado wanaendelea na vifungo vyao kwa utaratibu huu.

Licha ya kuwepo na mpango huu wa kupunguza msongamano wa wafungwa gerezani lakini bado wafungwa wengi wameshindwa kunufaika na utaratibu wa Paroli kutokana na kutotimiza masharti ya parole.

Sababu kubwa ni ukosefu wa nakala za hukumu kwa wakati na ukosefu wa elimu ya kutosha  kwa wanajamii kuhusu sheria hii na hivyo kupelekea maafisa wa Paroli  kuwa na ugumu wa kupata taarifa muhimu zinazowahusu wafungwa wananotarajiwa kunufaika na mpango huu.

 Maafisa wa Magereza wakimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Magalula Said Magalula
Mkuu wa Mkoa wa Tanga akisaini kitabu cha wageni
Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tanga Kam. Augostino Mboje akitoa taarifa ya utekelezaji wa sheria ya Parole katika Mkoa wa Tanga
Baadhi ya wajumbe na Maafisa wa magereza wakati wa uzinduzi



Read more

Mkoa Wa Tanga Kuwa Mwenyeji Wa Maadhimisho Ya Siku Ya Utepe Mweupe Kitaifa Machi 15

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Magalula S. Magalula akizungumza  na Waandishi wa Habari  Leo Ofisini kwake 
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Tanga Bw. Ramadhani Kaswa  (Kushoto ) na baadhi ya Waandishi wakati wa mkutano
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakati wa mkutano

Taarifa zaidi

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga kwa niaba ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Muungano wa Utepe Mweupe wa Uzazi Salama Tanzania inapenda kuwatangazia Wananchi  kuwa Mkoa wa Tanga unatarajia kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya Siku ya Utepe Mweupe Kitaifa itakayofanyika Machi 15, Mwaka huu.

Siku ya Utepe Mweupe ni mwendelezo wa juhudi za Serikali katika kupunguza  na kutokomeza kabisa vifo vya akina mama na watoto wachanga.Maadhimisho haya ambayo hufanyika  Machi 15 kila mwaka yana lengo la kuwakumbuka na kuwaenzi wanawake waliopoteza maisha kutokana na matatizo ya uzazi.

Siku hii pia hutumika kujadili mikakati ya kuzuia vifo vingine visitokee. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “WAJIBIKA MAMA NA MTOTO MCHANGA AISHI”.  Kauli mbiu hii inalenga kuhamasisha uwajibikaji wa kila mmoja wetu kuanzia mama mjamzito nwenyewe na familia yake,  jamii na uongozi katika kuhakikisha kuwa hakuna mama wala mtoto mchanga anayepoteza maisha kutokana na sababau ambazo zingeweza kuzuilika.

Aidha, kutakuwepo na shughuli mbalimbali ambazo zitaambatana na maadhimisho haya katika wiki ya kuelekea siku yenyewe ambazo ni pamoja na uchangiaji damu salama, kushiriki katika zoezi la sauti ya jamii,kushiriki katika matembezi ya mshikamano na mkutano siku ya kilele.

 Asilimia 75 ya vifo vingi nchini vinatokana na kutoka damu kwa wingi, maambukizi, shinikizo la damu na utoaji mimba. Wanawake 24 wanafariki kila siku na wengine hupata ulemavu wa kudumu.

Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kuweka mikakati madhubuti ili kupunguza vifo vya mama na mtoto. Kwanza imeelekeza nguvu zake katika kutoa elimu ya uzazi salama na pia imeelekeza Halmashauri zote Mkoani kuwa na kipengele mahususi cha bajeti kinacholenga kuhakikisha kuwa huduma za dharura za uzazi zinapatikana karibu na akina mama na watoto.

Kutokana na juhudi za serikali na wadau mbalimbali, matunda yameshaanza kuonekana miongoni mwetu. Kwa mfano katika Mkoa wa Tanga vifo vya mama na mtoto vimepungua kutoka idadi ya akina mama 101 kati ya wakina mama 45,256 waliojifungua kwa mwaka 2013 hadi kufikia idadi ya akinamama 69 kati ya wakina mama 47,692 waliojifungua kwa mwaka 2014 na idadi ya watoto 429 kati ya watoto 44,852 waliozaliwa  kwa mwaka 2013.   Serikali inaendelea na mapambano kuhakikisha afya ya mama na mtoto iko salama.

Kupunguza vifo vya mama na mtoto vinavyotokana na matatizo wakati wa kujifungua ni  moja ya malengo 8 ya Milenia. Hili ni lengo namba tano ambalo linalenga kupunguza vifo vya akina mama vinavyoyokana na matatizo wakati wa kujifungua kwa asilimia sabini na tano (75%) ifikapo mwaka 2015.

Nawashukuru na kuwapongeza wenzetu wa Utepe Mweupe na wadau wengine kwa kujikita katika kampeni ya uhamasishaji ili kupunguza na kutokomeza vifo vya mama na mtoto.

Napenda kutoa wito kwa wananchi kuhakikisha kuwa kila mmoja anatekeleza wajibu wake ili kuokoa maisha ya mama na mtoto. Pia naviomba vyombo vya habari kuungana na makundi mengine katika jamii kuwa sauti ya akina mama ili kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Kwa pamoja tunaweza kuzuia vifo vya mama na watoto wachanga

“Wajibika Mama na Mtoto Mchanga Waishi”





Read more

Wakuu Wapya Wa Wilaya Mkoani Tanga Waapishwa Leo

Mhe. Magalula Said Magalula akimwapisha Mhe. Husna Rajab Msangi kuwa  Mkuu wa Wilaya ya Handeni .


Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Magalula Said Magalula amewaapishwa leo Wakuu Wapya wa Wilaya ambao ni Mhe. Husna Rajab Msangi, Mkuu wa Wilaya ya Handeni na Mhe. Mariam M. Juma , Mkuu wa Wilaya ya Lushoto wakati wa hafla fupi iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga .

Mhe. Magalula ameonya tabia ya umangimeza na kuwaasa Wakuu hao wapya kuwa njia pekee ya kumwahakikishia Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete ,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa hajakosea kuwateua ni kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii.

Aidha kwa upande wao, Wakuu hao wameomba ushirikiano kutoka kwa viongozi wa Wilaya wanakotoka na Mkoa ili waweze kutekeleza majukumu yao vizuri.

               Mhe Magalula Said Magalula akimwapisha Mhe. Mariam M. Juma kuwa  Mkuu wa Wilaya ya Lushoto .
Baadhi  ya waalikwa wakati wa kiapo

Picha ya pamoja ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Katibu Tawala wa Mkoa Bw. Mohamed Chima ( wa kwanza kushoto kwa waliokaa), wakuu wa Wilaya Wapya , Viongozi Maalumu na  Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Wilaya




Read more

Utepe Mweupe Wakutana Na Waandishi Wa Habari Mkoani Tanga

Bi Rose Mlay, Mratibu wa Muungano wa Utepe Mweupe akitoa mada . Kulia ni Bw. Kenneth Simbaya , Mmoja wa wakufunzi kwenye warsha.


“Mama akiwa salama Taifa liko salama, Mama anapokufa na Taifa linakufa” Hayo ni baadhi ya maneno ambayo waliaswa waandishi wa habari kwenye warsha ya Waandishi wa habari iliyoandaliwa na Muungano wa Utepe Mweupe iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa  Kituo cha Walemavu ( YDCP)

Waandishi  wa Habari kutoka vyombo vya Habari Mkoani Tanga walipata wasaa wa  kuongeza uelewa wa masuala ya Vifo vya Mama na Mtoto. Akizungumza kwa hisia kali, Bi Rose Mlay  ambaye ni Mratibu wa Muungano wa Utepe Mweupe aliwaomba waandishi wa habari kuungana na makundi mengine katika jamii kupaza sauti  kwa niaba ya akina mama ili kupunguza vifo vya mama na mtoto.

“Sababu za vifo vya mama na mtoto hazichagui zinaweza kutokea kwa mama yeyote awe tajiri ama maskini. Mama anahitaji kituo cha afya kilichokaribu na chenye huduma nzuri , vifaa na wataalamu. Jamani Tuwajibike ili mama aishi”

Naye Bw. Kenneth Simbaya , mmoja wa wakufunzi kwenye warsha hiyo alitoa wito kwa waandishi  wa habari kuona umuhimu wa kuandika makala na habari za vifo vya akina mama na watoto ili jamii husika na serikali ilichukulie suala hilo kwa uzito mkubwa.

Warsha ya waandishi wa habari iliyoamdaliwa na Muungano wa Utepe Mweupe ni maandalizi ya maadhimisho ya siku ya Utepe Mweupe yenye kauli mbiu “Wajibika  Mama Aishi”yatakayofanyika kitaifa Machi 15 katika Mkoa wa Tanga.

 Bw. Hassan Hashim, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Tanga  ambaye pia ni Mwakilishi wa Channel Ten akichangia mada wakati wa Warsha
Bw.  John Semkande, mwakilishi kutoka Pangani Fm akitoa ushuhuda ni kwa jinsi gani amekuwa akitimiza wajibu wake ili kuhakikisha anaokoa maisha ya mama na mtoto 



Read more