Mkuu wa Mkoa Tanga awataka Wanawake Wilayani Korogwe kuwashitaki Wanaume Walevi



Wanawake Wilayani Korogwe wametakiwa kuwashitaki  kwa viongozi waume zao ambao wana tabia ya kuuza chakula cha familia na kutumia pesa hizo kwa ajili ya ulevi badala ya kuihudumia familia.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe.  Chiku Gallawa wakati wa  mkutano wa hadhara wa wananchi wa kijiji cha Mafureta kilichopo Korogwe vijijini  ambapo aliwataka wanawake kutowaonea huruma  wanaume wenye kasumba ya kuziterekeza familia kutokana na ulevi.
 
Mhe. Gallawa  alionekana kukerwa na maisha duni ya wakazi hao licha ya kuzunguukwa na mazingira mazuri ya kilimo na kutaka kujua kulikoni, aliwapasha wananchi hao kuwa ardhi ni mali na kwamba hawakustahili  kuwepo kwenye lindi la umaskini.
Hata hivyo idadi kubwa ya watu waliyokuja kumsikiliza Mkuu huyo wa Mkoa walikuwa katika hali ya ulevi huku  watoto waliyokuwepo kutokuwa na  viatu wala nguo zenye kuleta matumaini ya maisha bora kwa  mtanzania jambo lililomchefua sana .
“Akinamama toeni taarifa kwenye vyombo vya sheria kwa wababa wanaouza vyakula  na kwenda kulewa  pombe ama kuongeza nyumba ndogo  huku watoto hawana viatu wala vifaa vya shule” alisema Gallawa.
Kwa upande mwingine aliwataka wananchi kuachana na kilimo cha mazoea  ambacho alisema kuwa  hakiwezi kuwaletea mabadiliko  mazuri ya  kimaisha kwa kuwa hakina tija wala muelekeo.
Awali Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Lucas Mweri  wakati akijibu hoja ya  Mkuu wa Mkoa kuhusu mradi wa kijiji hicho, alieleza kuwa kijiji cha Mafureta ni miongoni mwa vijiji vilivyopata  fedha kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na kwamba zaidi ya tsh, million 300 zilitolewa kuiimarisha.
Mweri alieleza kuwa jumla ya tsh million 300 zilitolewa kwenye skimu ya Mafureta kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu na kuboresha thamani ya zao la mpunga na kwamba watakopeshwa pembejeo kwa kulipa wakati wa mazao pamoja na mkakati  wa barabara ya uhakika.

Naye Mbunge wa jimbo la Korogwe vijiji, Stivin Ngonyani (Profesa Majimarefu) aliwataka wananchi hao kuchangia mambo ya maendeleo yao badala ya kuchanga fedha kwa ajili ya kuleta waganga wa jadi ambao hatima yake ni kusababisha migogoro na jamii kutengana.

 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Korogwe Vijijini Bw. Lucas Mweri akijibu hoja ya mradi wa kilimo cha umwagiliaji kijijini hapo

Umati wa wanakijiji waliofika katika mkutano wa hadhara wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa

Baadhi ya watoto waliofika kwenye mkutano wa hadhara wengi wao wakiwa hawana viatu


Written by

0 comments: