Mkuu wa Mkoa wa Tanga Afungua Jengo la Maabara ya Kompyuta katika Shule ya Seminari Livingstone Muheza


Mhe. Chiku Gallawa , Mkuu wa Mkoa wa Tanga akifanya ufunguzi wa maabara ya Kompyuta katika Shule ya Seminari ya Livingstone iliyopo Wilayani Muheza Mkoa wa Tanga.
Mhe. Gallawa akitumia moja ya Kompyuta za maabara  mara baada ya uzinduzi. Wanaoangalia ni viongozi wa juu wa Wilaya ya Muheza na uongozi wa shule.
Ukaguzi wa majengo ya shule mara baada ya uzinduzi. Kulia ni Meneja wa shule Mch. Andrew Park
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Seminari ya Livingstone wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Tanga (  hayupo pichani)
Majengo ya madarasa ya shule ya Livingstone.


Jengo la maabara ya kompyuta la Shule ya Secondari ya Livingstone lililoanza kujengwa mwezi Agosti na kukamilika Januari mwaka huu limezinduliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Chiku Gallawa na lipo tayari kutumika. 

Mradi huo ambao umfadhiliwa na wahisani kutoka Umoja wa Wamishonari wa Afrika Mashariki kutoka  Korea na  Marekani, umegharimu kiasi cha fedha ya Marekani 87,000/= ambayo ni sawa sawa na shilingi za 149,000,000/=  za Kitanzania ikiwa ni fedha ya ujenzi na ununuzi wa Kompyuta 40, viti na madawati.

Akizungumza na Uongozi wa shule  ya Seminari ya Livingstone pamoja na wanafunzi , Mhe Gallawa ameupongeza uongozi wa shule hiyo kwa kuona umuhimu wa kujenga maabara hiyo ambayo itamwezesha mwanafunzi mmoja mmoja kujifunza kwa vitendo.
“Jiepusheni na makundi ya vijana waalioharibikiwa hasa mnapokwenda likizo na muache kujiingiza katika suala zima la mahusiano ya kimapenzi kwani litawapotezea muda na litawaharibia katika masomo yenu” Mhe. Gallawa alimewaasa wanafunzi.

Pamoja na kazi nzuri iliyofanywa na Uongozi wa shule hiyo wa ujenzi wa maabara ya Kompyuta, Mhe. Gallawa ameusisitizia uongozi  kutekeleza agizo la serikali la ujenzi wa maabara tatu za sayansi ambazo  ni za masomo ya Fizikia,Biolojia na Kemia.

Naye  Mkuu wa Shule ya Seminari ya Livingstone Mch.  Jonathani Mwamboza wakati akisoma taarifa fupi ya maendeleo ya shule hiyo amesema kuwa matazamio  ya shule yao  ni vijana kupata ufahamu wa hali ya juu pamoja na malezi mazuri yatakayowajengea uadilifu wa hali ya juu katika jamii na taifa kwa ujumla.

“Mhe. Mkuu wa Mkoa, kama inavyoonekana, shule yetu imeanzishwa ikiwa na miundombinu yenye kuwezesha utoaji wa Elimu bora na kujenga matumaini ya matokeo makubwa sasa”amesisitiza Mch. Mwamboza.  Shule ya Seminari ya Livingstone ilianzishwa mwaka 2012 na mpaka sasa ina kidato pili na idadi ya wanafunzi 225. Matarajio ya baadaye ni kuwa na kidato cha tano na sita  kwa wanafunzi wa sayansi na pia kuwa na chuo cha masomo ya sayansi ( science college)


Written by

0 comments: