Wilaya ya Tanga Yaendelea Kung’ara Mbio za Mwenge Kitaifa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Jakaya Mrisho akiwa katika picha ya pamoja na washindi wa Mbio za Mwenge 2013 Kikanda na Kitaifa. Wa pili kushoto ni Mratibu wa Mwenye Wilaya ya Tanga Bw. Hanafi Bakari Massudi akiwa na kombe la Ushindi
Mhe. Kikwete akihutubia wananchi siku ya kilele cha maadhimisho ya Mbio za Mwenge 2013  katika Uwanja wa Samora mjini Iringa 
Baadhi ya wananchi waliofika katika maadhimisho ya Mbio za Mwenge katika Uwanja wa  Samora mjini Iringa

Maadhimisho ya mbio za Mwenge 2013 yalipambwa na washindi wa mbio za mwenge Kikanda na Kitaifa. Wilaya ya Tanga imeendelea kutwaa kombe la mshindi wa kwanza Kikanda ( yenye mikoa ya Tanga, Morogoro, Iringa, Tabora, Njombe, Shinyanga na Simiyu)  na mshindi wa pili Kitaifa na hii ni mara ya pili kwa Wilaya ya Tanga kunyakua kikombe cha ushindi wa Mbio za Mwenge.

Sherehe hizo zilizofana zilihudhuriwa na maelfu ya wakazi wa Iringa na wawakilishi wa kitaifa kutoka Mikoa na Wilaya mbalimbali na kusindikizwa na burudani za vikundi mbalimbali vya ngoma za asili, kwaya na Bongo fleva. Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Mhe. Dkt Jakaya Mrisho Kikwete.

Akifafanua umuhimu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Rais Kikwete alivipongeza vyombo vya Habari kwa kufikisha ujumbe wa Mwenge kwa wananchi .

“Bila vyombo vya habari wapotoshaji hawakosekani, na wasiopenda Mwenge pia wapo, hawawezi kukosekana”

Amewapongeza watanzania wanaokataa ushawishi wa kugawanya kwa misingi ya dini, siasa na mambo mengine.

Alisema dhambi kubwa ya kubaguana kwa misingi yoyote ile ni kupotea kwa amani na kwamba amani ikipotea watu watatumia muda mwingi kujihami badala ya kufanya shughuli zao za maendeleo.

Amesisitiza kuwa  serikali yake itaendelea kukemea vitendo vyote vya kuvuruga amani na watakaohusika watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Akizungumzia umuhimu wa siku ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere amesema, kilele cha maadhimisho ya Mbio za Mwenge kimefanywa kuwa siku ya kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere tangu afariki miaka 14 iliyopita.

Ametoa wito kwa  watanzania wote bila kujali itikadi zao  kuwa wana wajibu wa kuyakumbuka mema yote yaliyofanywa na baba wa Taifa, mafundisho yake na urithi kwa Taifa hili.“Nia ya maadhimisho haya, watu wasimsahau kiongozi huyu maalumu katika historia ya nchi; tunahitaji kumkumbuka hasa wakati huu wa mchakato wa Katiba,” alisema.

 




Written by

0 comments: