Halmashauri Muheza Kuongeza Ukusanyaji Mapato ya Ndani
Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Muheza, Bw. Ibrahim Matovu
HALMASHAURI ya Wilaya ya Muheza
inatarajia kukusanya Shilingi Bilioni 1 katika mwaka wa fedha ujao wa 2013/2014
kutoka katika vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwemo mabango ya matangazo ya
biashara pamoja na minara ya mawasiliano ya simu za mkononi.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Muheza, Ibrahim Matovu wakati akijibu maswali ya
wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa(LAAC)
ilipofika kwa mahojiano mjini humo hivi karibuni
Alisema katika kuhakikisha
makusanyo hayo yanapatikana tayari Halmashauri imetuma timu ya wataalam kupita
katika maeneo mbalimbali ya mjini na vijijini wilayani humo kwa ajili ya
kuhakiki aina tofauti za mabango ya matangazo zilizopo ili waweze kuyawekea
viwango vya tozo.
Matovu alisema lengo ni kupunguza
changamoto zinazowakabili hivi sasa katika ukusanyaji wa mapato ya halmashauri
ili hatimaye waweze kufikia lengo lao hilo katika mwaka wa fedha ujao.
“Tumefanikiwa kuongeza kiwango cha
makusanyo kila mwaka na hivi sasa kwa mwaka huu wa 2012/2013 tumekusanya kiasi
cha sh. Milioni 856 kiwango ambacho kimevuka lengo letu la makusanyo tulilokuwa
tumelikadiria awali’, alisema na kuongeza.
“Makisio yetu katika bajeti ya
mwaka ujao wa fedha ambayo tayari tumeanza maandalizi ni kukusanya sh. Bilioni
moja na tunaamini tutafikia lengo hili kwasababu tumejipanga vizuri na
tunaboresha mifumo ya ukusanyaji ikiwemo kuwafuta mawakala wanaoshindwa kufikisha
malengo ya makusanyo ”,alisema.
Awali wajumbe wa kamati hiyo
akiwemo Kangi Ligora alihoji kutaka kujua mfumo wanaotumia katika ukusanyaji wa
mapato kutoka katika baadhi ya vyanzo hasa Mabango ya matangazo na Minara ya
mawasiliano ya simu.
“Nataka kujua hapa Muheza kama
mnakusanya fedha kutoka katika mabango yote ya matangazo yaliyopo kwasababu
uzoefu uliopo katika halmashauri nyingi hawakusanyi na hatua hii inakosesha
halmashauri nyingi mapato kwa madai kwamba wamiliki wengi wa mabango hayo hawajulikani
walipo “ alisema.
“Ushauri wangu katika hili
nawatuma kwamba katengenezeni mgogoro na wenye mabango hasa kwa kuanza
kuyang’oa hayo mabango yao badala ya kuyawekea alama ya x ...naamini kwa
kufanya hivyo ndipo mtaweza kuwapata wamiliki wake na watawalipa fedha
yenu”,alishauri.
Kwa upande wake Mbunge wa viti
maalum Vijana kutoka Zanzibar, Tauhida Galoss aliitaka halmashauri hiyo kwenda
kujifunza namna bora ya ukusanyaji wa mapato katika mabango ya matangazo katika
manispaa ya Ilala iliyoko jijini Dar es salaam ambao alidai wamefanikiwa sana
katika suala hilo.
Akifunga mjadala wa hoja hiyo,
Mwenyekiti wa kamati hiyo ya LAAC, Rajabu Mbarouk aliipongeza halmashauri hiyo
kwa kuendelea kuongeza kiwango cha ukusanyaji wa mapato ya ndani kila mwaka na kuwataka
waongeze juhudi katika ukusanyaji kodi itokanayo na chanzo cha Mrabaha wa
minara ya mawasiliano ya simu.
“Katika hili la kodi ya minara ya
simu za mkononi naomba nalo mwende mkajifunze katika halmashauri ya wilaya ya
Kilindi kwasababu wao wamepambana na sasa wanapata mrahaba wao kutoka kwa
kampuni zote za simu za mkononi zenye minara ndai ya wilaya hiyo”, alisema. Habari na Anna Makange- Habari Leo
0 comments: