Mkoa wa Tanga wazindua Mpango wa Uwiano wa Maendeleo wa miaka Mitano 2011/2012- 2015/2016

Mkuu wa Mkoa wa Tanga ,Mhe. Chiku Gallawa akizindua rasmi mpango huo. Kushoto ni katibu Tawala Mkoa wa Tanga Bw. Benedict Ole Kuyan.
 

Mpango wa Uwiano wa Maendeleo wa Mkoa wa Tanga ni mpango ambao umeandaliwa kimkakati baada ya kuchambua hali halisi ya maisha ya Wakazi wa Mkoa wa Tanga na kuwashirikisha  wadau wa maendeleo ambao wako tayari kushirikiana na Serikali katika kutumia rasilimali zilizopo katika kuinua kipato cha mwananchi mmoja mmoja ha hatimaye kuinua uchumi na maendeleo  ya Mkoa wa Tanga.

Akizindua mpango huo wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri cha Mkoa jana, Mkuu wa Mkoa wa Tanga ,Mhe. Chiku Gallawa  amesema kuwa mpango huu una lengo la kubadili hali ya uchumi wa Mkoa wa tanga ili Mkoa uweze kuwa  na kipato cha kati ifikapo 2015 ( pato  la wastani la Mkazi wa Tanga kuwa dola 3000).

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Tanga Bw. Benedict Ole Kuyan akitoa salamu zake ameushukuru uongozi wa SULGO-GIZ Dar es salaamu na Tanga kwa ushirikiano mkubwa unaouonyesha katika kuwezesha uandaaji wa mpango huu.

Mpango huu wa uwiano wa Mkoa wa Tanga umejikita katika kutekeleza vipaumbele vichache ambavyo vitakuwa chachu ya kukuza uchumi katika Mkoa wa Tanga. Vipaumbele hivyo ni pamoja  na Kilimo, Mifugo na Ushirika, Mali asili na Utalii, Viwanda na Biashara na Miundombinu.

Katika kuleta matokeo makubwa ndani ya muda mfupi nazo sekta za huduma za jamii ( Afya, Elimu na Maji) zimepewa umuhimu bila kuacha nyuma masuala ya Utawala Bora, Uwazi na Uwajibikaji, Rasilimali watu, na Teknolojia ya Habari na Mawsiliano.

Mkoa wa Tanga ni Mkoa wenye fursa nyingi ikiwemo uwepo wa ardhi ya kutosha yenye rutuba kwa ajili ya kilimo cha mazao mbalimbali ya chakula na biashara, mvua za kutosha, vivutio mbalimbali kama fukwe , malighafi za kutosha na madini.


Written by

0 comments: