Hotuba ya Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete , Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa Bungeni kuhusu Jumuiya ya Afrika Mashariki, Novemba7, 2013 Dodoma


Mheshimiwa Anne Makinda, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
 Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa Mizengo Pinda, Waziri Mkuu;
Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri;
Mheshimiwa Freeman Mbowe, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni;
Waheshimiwa Wabunge;
Mabibi na Mabwana;

          Nakushukuru sana Mheshimiwa Spika kwa kukubali ombi langu na kutenga muda wenu ili niweze kuzungumza na Wabunge wa Bunge lako Tukufu kuhusu masuala muhimu kwa uhai, ustawi na maendeleo ya nchi yetu na watu wake.
Mheshimiwa Spika;
          Nimeambiwa kuwa taarifa ilipotolewa kuwa ninaomba kuja kuzungumza na Waheshimiwa Wabunge, kumekuwepo na dhana mbalimbali.  Wapo waliodhani kuwa nakuja kuzungumzia mchakato wa kuunda Katiba mpya na hasa matukio ya wiki chache zilizopita.   Wapo waliodhani nakuja kuzungumzia “Operesheni Tokomeza”.  Tena wapo waliokwenda mbali na kufikiria kuwa nakuja kuwakaripia Waheshimiwa Wabunge waliotoa maoni yao kuelezea kasoro zilizojitokeza katika utekelezaji wa Operesheni hii muhimu. Na wapo pia waliodhani ninakuja kuzungumzia ushiriki wa majeshi yetu ya Tanzania katika Jeshi la Kulinda Amani la Umoja wa Mataifa nchini Kongo.

Mheshimiwa Spika;
          Hayo si makusudio yangu.  Kinachonileta mbele ya Bunge lako Tukufu ni kuzungumzia Jumuiya ya Afrika Mashariki na mustakabali wa Tanzania katika Jumuiya hiyo.  Lakini, kwa sababu ya umuhimu wa masuala hayo niliyoyataja na rai niliyopewa kuwa niyasemee japo kidogo.  Nimeona ni vyema nifanye hivyo.
Mheshimiwa Spika;
  Kuhusu mchakato wa Katiba mpya, napenda kusema kuwa tumefikia hatua nzuri katika utekelezaji wake.  Kama mjuavyo Tume ya Mabadiliko ya Katiba imekamilisha, kwa mafanikio, hatua ya mwanzo ya kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu Katiba wanayoitaka.  Pia walishatoa Rasimu ya Kwanza ya Katiba na kukamilisha mchakato wa Mabaraza ya Katiba.  Kinachosubiriwa kwa hamu na sisi wote, ni Rasimu ya Pili ya Katiba ambayo inatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 15 Desemba 2013 au kabla ya hapo.
Mheshimiwa Spika;
          Kwa upande wa Bunge lako Tukufu, tunategemea kupata mambo mawili kutoka kwenu yatakayowezesha mchakato kutekelezwa vizuri katika hatua zinazofuata.  Jambo la kwanza ni kutungwa kwa Sheria ya Kura ya Maoni na pili kufanyika kwa marekebisho ya nyongeza ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kuhusu Bunge Maalum ili kuboresha utekelezaji wake.  Baada ya Bunge kukamilisha kazi yake hiyo itafuatia uteuzi wa Wajumbe wa Bunge Maalum ili kazi ya kujadili Rasimu ya Pili ya Katiba ifanyike na kutupatia Rasimu ya Mwisho. Rasimu ambayo ikikubaliwa na wananchi katika Kura ya Maoni itakayofanyika wakati wo wote mwakani, tutakuwa tumepata Katiba Mpya.  Hivi sasa katika Serikali tunaendelea kufanya tafakuri na tunachukua hatua za kuwezesha Bunge Maalum na Kura ya Maoni kufanyika kwa mafanikio.

Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika;
          Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge wa Bunge lako Tukufu kuwa sikukasirishwa na maoni yao kuhusu madai ya kuwepo kasoro katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza. Shabaha ya Operesheni hii ni kuokoa maliasili za misitu na wanyamapori dhidi ya uvunaji haramu ambao umefikia kiwango kinachotishia kutoweka kwa raslimali hizo.  Kwa kweli hali inatisha.  Miti inakwisha na ndovu na faru wanaangamia. 

Mheshimiwa Spika;
          Wakati, tunapata Uhuru Tanzania ilikuwa na ndovu waliokadiriwa kuwa takribani 350,000.  Lakini, kwa sababu ya ujangili uliokithiri katika miaka ya 1970 na 1980  ilipofika mwaka 1989 kulikuwa na ndovu wapatao 55,000 tu.  Ilipofikia hali hiyo Serikali ikaanzisha Operesheni Uhai iliyohusisha Jeshi la Ulinzi na kuongozwa na Meja Jenerali  John Walden (ambaye sasa ni marehemu) kuendesha mapambano dhidi ya majangili. Kutokana na hatua hiyo na uamuzi wa Shirika linalosimamia biashara ya wanyama walioko kwenye hatari ya kutoweka (CITES) kupiga marufuku biashara ya pembe za ndovu duniani, idadi ya ndovu nchini iliongezeka na kufikia 110,000 mwaka 2009.

Tumewaomba Fankfurt Zoological Society ambao ni wabia wetu katika uhifadhi wa wanyama pori kwa miaka mingi wafanye sensa maalum ya ndovu katika Hifadhi ya Selous na kote nchini ili tujue hali halisi ikoje.  Kazi hiyo inaendelea hivi sasa.

Mheshimiwa Spika; 
  Baada ya mwaka 2009 kumezuka wimbi jipya, tena la nguvu kubwa, la kuua ndovu na faru nchini na kwingineko katika Bara la Afrika ambako wanyama hao wapo.  Idadi kubwa ya meno ya ndovu yaliyokamatwa na yanaoendelea kukamatwa nchini na kwingineko duniani inathibitisha ukweli huo.  Kwa mfano, kati ya mwaka 2010 na Septemba, 2013, hapa nchini, kwa jitihada zetu vipande 3,899 vya pembe za ndovu vyenye uzito wa kilo 11,212 na vipande 22 vya pembe za ndovu zilizochakatwa zenye uzito wa kilo 3,978 vilikamatwa.  Aidha, katika kipindi hicho vipande 4,692 vya pembe za ndovu vilivyotokea Tanzania vyenye uzito wa kilo 17,797 vilikamatwa nje ya nchi.     

Mheshimiwa Spika;
          Kama nilivyokwisha sema hapo awali matatizo ya kuuawa kwa wingi kwa ndovu na faru lipo pia katika nchi nyingine Afrika zenye wanyama hao.   Nchi za Gabon, Kenya, Afrika ya Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Uganda, Zimbabwe, Zambia na nyinginezo nazo zinakabiliwa na matatizo kama yetu.  Tatizo limekuwa kubwa kiasi cha kuifanya Jumuiya ya Kimataifa kushtuka na kuamua kuingilia kati kwa namna mbili.  Kwanza kuunga mkono juhudi za uhifadhi wa ndovu na faru katika nchi zenye wanyama hao.  Na, pili, kuchukua hatua thabiti kudhibiti biashara ya meno ya ndovu duniani.  Ni ukweli ulio wazi kuwa kama hakutakuwepo na wanunuzi wa meno ya ndovu na faru hakuna ndovu au faru atakayeuawa.
Mheshimiwa Spika;
 Kutokana na ukweli ulivyo uamuzi wetu wa kuendesha Operesheni Tokomeza ni sahihi kabisa.  Manufaa yaliyopatikana baada ya Operesheni Uhai ya mwaka 1989 yanatupa imani kuwa na safari hii pia tutafanikiwa.  Tusipochukua hatua kama hii sasa ni sawa na kuwapa kibali majangili waendelee kumaliza ndovu na faru nchini.  Hakika wanyama hao watakwisha.  Itakuwa ni aibu kubwa kwetu na historia itatuhukumu vibaya.

Mheshimiwa Spika;
          Tumeyasikia maelezo ya Wabunge kuhusu kasoro mbalimbali zilizojitokeza katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza.  Nawaahidi kuwa tutayafanyia kazi.  Serikali imeahirisha kwa muda Operesheni hii ili kujipa muda wa kurekebisha kasoro hizo na kujipanga upya.  Watendaji wasiokuwa waadilifu na wale wasiokuwa waaminifu wataondolewa.  Halikadhalika, kasoro za kimfumo nazo zitasahihishwa ili tutakapoanza upya Operesheni itekelezwe kwa mafanikio yaliyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika;
          Miongoni mwa mambo yaliyozungumzwa kwa uchungu ni ukamataji wa mifugo iliyokutwa kwenye mapori ya hifadhi za wanyama na vitendo vibaya walivyofanyiwa wenye mifugo na mifugo yenyewe.  Narudia kusisitiza kuwa taarifa zote hizo zitafanyiwa kazi na waliohusika watachukuliwa hatua zipasazo.  Pamoja na hayo, napenda kuwakumbusha ninyi watunga sheria wetu kuwa sheria ya hifadhi za wanyamapori hairuhusu mifugo kuchungwa katika maeneo ya hifadhi. 

Naomba tuwakumbushe wananchi tunaowaongoza wajiepushe na kufanya hivyo.  Ni uvunjifu wa Sheria za nchi.  Naomba pia, wananchi waelimishwe ili wajue kuwa wakifanya hivyo na kukutwa katika maeneo hayo na mifugo yao kuna adhabu iliyotamkwa kwenye sheria.   Hivyo tusiwalaumu wala kuwaona maafisa wanyamapori kuwa ni watu wabaya.  Wanatekeleza Sheria iliyotungwa na Bunge hili.  Pale wanapotenda visivyo tuseme, watawajibishwa ipasavyo.

Jeshi la Umoja wa Mataifa Kongo
Mheshimiwa Spika;
          Mapema mwaka huu (2013) Umoja wa Mataifa uliomba nchi yetu ichangie kikosi kimoja cha wanajeshi katika Brigedi Maalum iliyoundwa na Umoja huo kuongeza nguvu ya kudhibiti waasi Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.  Lengo la msingi ni kuiwezesha nchi hiyo kupata amani ya kudumu ambayo imekosekana kwa muda mrefu kutokana na kuibuka kwa uasi mara kwa mara.

Mheshimiwa Spika;
          Tulikubali, kwani hata kabla ya kuombwa na Umoja wa Mataifa tulishakubali maombi kama hayo yaliyotolewa kwenye Mkutano wa Nchi za Maziwa Makuu.  Ni miezi saba (tangu Aprili) sasa tangu wanajeshi wetu waende Kongo na wamekuwa wanatekeleza majukumu yao vizuri tena kwa weledi na nidhamu ya hali ya juu.  Sifa hiyo kwa wanajeshi wetu imekuwa inatolewa na viongozi wa juu wa Umoja wa Mataifa, viongozi wa juu wa Jeshi la Umoja wa Mataifa Kongo (MONUSCO) na viongozi wa juu wa Serikali ya Kongo.

Mheshimiwa Spika;
          Majeshi ya Umoja wa Mataifa hupewa majukumu na mamlaka ya namna mbili.  Yapo yanayopewa jukumu la kulinda amani tu.  Wanajeshi wake huwa hawapewi majukumu ya kimapigano na hata pale wanaposhambuliwa wanatakiwa kujihami tu.  Kwa kawaida majeshi yenye jukumu hili hupelekwa mahali ambapo kumekuwepo na makubaliano ya kuacha mapigano.  Wanapelekwa kusaidia kuona Mkataba unatekelezwa ipasavyo. 

Aina ya pili ni ile ya majeshi yanayopelekwa mahali ambapo hakuna amani hivyo wanapewa jukumu la kuchukua hatua za kufanya amani ipatikane.  Majeshi haya hupewa mamlaka ya kutumia nguvu ya kijeshi dhidi ya wanaosababisha amani ikosekane kama ni lazima kufanya hivyo.  Maana yake ni kwamba wanayo ruhusa kuingia katika mapigano dhidi ya watu au vikundi vinavyovuruga amani.  Tofauti na wenzao wa kundi la kwanza, wanajeshi wa kundi la pili wako kwenye hatari zaidi ya kupoteza maisha au kujeruhiwa kuliko wenzao ingawaje wapo wengi nao wameuawa na kujeruhiwa.

Mheshimiwa Spika; 
Wanajeshi wetu wamekwenda Kongo chini ya utaratibu huu wa pili ambao unahusu kuingia kwenye mapigano dhidi ya waasi kama hapana budi kufanya hivyo.   Wametekeleza majukumu yao vyema na kwa ujasiri mkubwa na weledi wa hali ya juu. Bahati mbaya tumepoteza vijana wetu watatu shupavu.  Daima tutawakumbuka na tutawaenzi ipasavyo mashujaa wetu hawa.  Tuzidi kuwaombea kwa Mola awape mapumziko mema.  Ameen.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Spika, napenda kutumia nafasi hii kumpongeza Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa mafanikio ya kihistoria waliyoyapata hivi majuzi dhidi ya waasi wa M23.  Tunamtakia yeye na wananchi wa Kongo kila la heri katika kazi ngumu iliyo mbele yao ya kujenga upya eneo hilo na kujenga mahusiano mapya miongoni mwa watu wa Kongo.  Pia nawapongeza sana wanajeshi wa Brigedi Maalum ya Umoja wa Mataifa kwa kazi nzuri waliyoifanya iliyowezesha mafanikio kupatikana.   Wanajeshi hao ni kutoka Afrika Kusini, Tanzania na Malawi wanaoongozwa na Brigedia Jenerali James Aloisi Mwakibolwa wa JWTZ.

Jumuiya ya Afrika Mashariki
Mheshimiwa Spika;
          Kama nilivyosema awali, haya mambo matatu siyo hasa makusudio yangu nilipoomba kuja kuzungumza na Waheshimiwa Wabunge wetu.  Nimeyachomekea tu kwa sababu ya umuhimu wake katika jamii kwa wakati tulio nao.  Jambo lililonileta hapa leo ni kuzungumzia hali ilivyo sasa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na nafasi ya Tanzania katika Jumuiya hiyo.  Nimeona nifanye hivyo kutokana na maswali mengi ambayo Watanzania wanajiuliza kufuatia matukio ya hivi karibuni ya viongozi wa nchi tatu wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaani Uganda, Rwanda na Kenya kukutana bila ya ushiriki wa viongozi wa Tanzania na Burundi.  Viongozi wenzangu hao wamefanya mikutano mitatu yaani: tarehe 24-25 Juni, 2013 mjini Entebbe, Uganda; tarehe 28 Agosti, 2013 mjini Mombasa, Kenya; na tarehe 28 Oktoba, 2013 mjini Kigali, Rwanda.

Mheshimiwa Spika;
          Naomba kwanza niweke wazi jambo moja, kwamba nchi mbili wanachama au zaidi hazikatazwi kuwa na makubaliano ya ushirikiano katika kufanya mambo mbalimbali.  Hata sisi Tanzania tunao ushirikiano wa namna hiyo na nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.  Lakini, nchi wanachama zinatakiwa kufanya hivyo kwa yale mambo ambayo hayako kwenye shughuli za Jumuiya kwa maana kwamba hayamo katika Mkataba au Itifaki au hakuna uamuzi wa msingi uliofanywa na vikao au taasisi za Jumuiya kuyashughulikia.  Pia, tunaweza kufanya hivyo kwa mambo ambayo yalishaamuliwa na Jumuiya yatekelezwe na ruhusa imetolewa kwa nchi yo yote iliyokuwa tayari kutekeleza ama peke yake au kwa kushirikiana na nchi nyingine.

Mheshimiwa Spika;
          Kwa mujibu wa matamko ya pamoja (Communique) yaliyotolewa baada ya mikutano hiyo, kuna mambo yapatayo manane ya msingi yaliyoamuliwa kufanywa na nchi hizo kwa lengo la kuendeleza utengamano wa nchi hizo wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.  Mambo hayo ni haya yafuatayo: 
(1)              Kujenga reli ya kisasa kutoka Mombasa hadi Kampala,  Kigali  na Bujumbura.
(2)             Ujenzi wa Bomba la Mafuta la kutoka Kenya hadi Uganda na Sudani ya Kusini.
(3)             Kujenga Kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda.
(4)             Kuanzisha Himaya Moja ya Ushuru  wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kutekeleza vipengele vyote;
(5)             Kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki na kwamba itaundwa Kamati ya kuandaa rasimu ya Katiba ya Shirikisho.
(6)             Kuharakisha uanzishwaji wa Visa ya pamoja ya Utalii ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (Single East African Community Tourist Visa); 
(7)             Kuandaa utaratibu wa kutumia vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria katika nchi zao; na
(8)             Kuongeza uzalishaji na usambazaji wa umeme.


Mheshimiwa Spika;
          Ni dhahiri kwamba orodha hiyo imechanganya mambo yale ambayo ni ya Jumuiya na yale yasiyo ya Jumuiya.  Kwa mfano, mambo manne kati ya hayo manane hayamo kwenye masharti ya kutokufanyika bila ya kuihusisha au kupata ridhaa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.  Jambo la kwanza ni uzalishaji na usambazaji wa umeme.  Ni kweli kwamba tunao mkakati wa kuwa na akiba ya pamoja ya nguvu ya umeme (East African Power Pool).  Hata hivyo, bado jukumu la kuzalisha na kusambaza umeme huo limeachiwa nchi wanachama zenyewe kuamua.  Lakini, hivi ndugu zetu hawa wanao muhali kuishirikisha Tanzania katika mpango ambao kimsingi umebuniwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo sote ni wanachama?    

Jambo la pili, ni ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda.  Hili si suala la Jumuiya bali la nchi ya Uganda kuamua yenyewe peke yake au kwa kushirikiana na wadau wengine.  Rais Yoweri Museveni alituarifu mpango huo na sote tuliupokea kwa furaha kwamba sasa tutapata mafuta karibu na nyumbani.   Alitualika kushiriki katika ujenzi wake sijui sasa amebadili mawazo kwamba Tanzania siyo muhimu.

Mheshimiwa Spika;
Jambo la tatu ni ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Kenya hadi Sudani ya Kusini na Uganda.  Hili si jambo linalobanwa na masharti ya Jumuiya. Ni juu ya nchi hizi tatu kuamua kufanya ili kuwezesha mafuta yao kufika kwenye masoko.  Hata hivyo, nimeambiwa kuwa Jumuiya imeshazungumzia bomba la mafuta kutoka Eldoret hadi Uganda, Rwanda na Burundi kuwa nalo lifike Tanzania kupitia upande wa Kaskazini Magharibi mwa Tanzania.  Inaelekea mpango huo sasa haupo maana hatujausikia kutajwa katika ujenzi wa bomba hilo. 
Mheshimiwa Spika;
Jambo la nne ni ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Mombasa – Kampala – Kigali – Bujumbura.  Hili nalo hatuna tatizo nalo.  Si mradi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ni jambo lililo chini ya mamlaka ya nchi wanachama husika.  Hata hivyo, ni vyema kutambua ujenzi wa miundombinu ya reli, barabara na usafiri wa anga na majini kuunganisha nchi za Afrika Mashariki ni miongoni mwa mambo ya kipaumbele cha juu yanayoshughulikiwa na Jumuiya yetu.  Jumuiya hutengeneza mikakati ya pamoja na ndiyo maana tuna East African Railway Masterplan, tuna East African Road Network, na tuna Lake Victoria Development Programme kwa ziwa Victoria. 
Kwa ajili hiyo, nilitegemea kuwa reli ya kutoka Mombasa hadi Kigali na Juba ingekuwa na tawi linalounganisha reli hiyo na reli ya Tanzania kama ilivyo reli ya Moshi – Voi – Taveta aliyotuachia mkoloni. Tulitegemea hivyo kwa minajili ya kuunganisha soko la Afrika Mashariki ambapo naamini Tanzania ni mdau muhimu.  Lakini inaelekea kwa maoni ya wenzetu hivyo sivyo. 

Mheshimiwa Spika;
Lazima nikiri kuwa inashangaza na tunayo kila sababu ya kuuliza kwa nini wenzetu wameamua kufanya hivi.  Kumetokea nini toka tukutane pale Arusha Aprili 28, 2013 na Juni 24, 2013 walipokutana kuamua kufanya mambo ya kujenga na kuimarisha utengamano wa Afrika Mashariki kwa kubaguana,  Haijawahi kuwa hivi kabla.   

Mheshimiwa Spika;
          Katika mambo manne yaliyosalia ambayo yaliamuliwa na kuwekewa utaratibu wake wa utekelezaji na Jumuiya ya Afrika Mashariki mawili hatuna maneno nayo.  Mambo hayo ni matumizi ya vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria na Visa ya Pamoja ya Utalii kwani tuliamua kwa pamoja kuwa nchi wanachama zilizokuwa tayari waanze.  Lakini, kwa upande wa kuanzishwa kwa Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha (Single Customs Territory) na Shirikisho la Afrika Mashariki tunadhani wenzetu wamekiuka uamuzi wetu wa pamoja.

Mheshimiwa Spika;
          Katika Mkutano Maalum wa 11 wa Wakuu wa Nchi wanachama uliofanyika tarehe 28 Aprili, 2012 Jijini Arusha, tulipokea na kuridhia mapendekezo ya kuanzisha Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha (Single Customs Territory).  Kwa mujibu wa mapendekezo hayo kila nchi mwanachama itasimamia shughuli zake za kiforodha na kukusanya mapato yake kama ilivyo sasa.  Hata hivyo, kwa bidhaa zinazopitia nchi moja kwenda nchi nyingine mwanachama, ukaguzi na ukusanyaji wa mapato utafanyika katika kituo cha kwanza bidhaa hizo zinapoingilia.  Mapato hayo yatawasilishwa kwa nchi husika baada ya kuthibitisha kuwa bidhaa zilivuka mpaka. 

Mheshimiwa Spika;
Kutokana na uamuzi huo, Wakuu wa Nchi waliagiza Baraza la Mawaziri kuunda Kikosi Kazi cha kujadiliana na kuandaa utaratibu wa utekelezaji wa mfumo huo.  Taarifa ya kikosi kazi inatakiwa kutolewa katika Mkutano wa 15 wa Wakuu wa Nchi utakaofanyika Kampala, Uganda tarehe 30 Novemba, 2013.  Iweje leo nchi tatu wanachama ziamue peke yao kuanza kutekeleza?  Wanatekeleza nini na kwa nini wafanye hivyo? 



Mheshimiwa Spika;
          Kuhusu Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki hadithi yake inafanana na hii ya Himaya ya Forodha.  Katika Mkutano wa 14  wa Wakuu wa Nchi wanachama uliofanyika tarehe 30 Novemba, 2012, Nairobi, tulipokea taarifa ya hatua iliyofikiwa kuhusu mchakato wa kutaka kuanzishwa kwa Shirikisho.   Mkutano huo uliagiza nchi wanachama kujadiliana zaidi kuhusu mpango kazi wa kufikia Shirikisho la Kisiasa na mpango wa kutekeleza mapendekezo mengine yaliyotolewa na Timu ya Wataalamu.  Inategemewa kuwa Baraza la Mawaziri litawasilisha mapendekezo ya majadiliano hayo katika Mkutano wa 15 wa Wakuu wa Nchi mwezi Novemba, 2013.  Iweje leo wenzetu hawa waamue kuanzisha mchakato wao wa kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki.   

Mheshimiwa Spika;
     Kwa kweli huwa najiuliza maswali mengi na kukosa majibu kuhusu nini kinachoendelea kufanywa na viongozi wenzangu watatu na kwa nini!  Nakosa majibu ya uhakika.  Je wenzetu wamekosa imani na Jumuiya ya Afrika Mashariki na je wanataka kuunda yao?  Je wanaichukia nchi yetu na hivyo wameamua kutufanyia vitimbi tutoke!  Au sijui wanachuki na mimi!  Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kuwa hatuna mpango wa kutoka (kama vijana wasemavyo hatoki mtu hapa).  Tupo na tutaendelea kuwepo!  

Mheshimiwa Spika;
          Tanzania haijafanya jambo lo lote baya dhidi ya Jumuiya au nchi yo yote mwanachama.  Na ukweli ni kwamba ni mwanachama mvumilivu, mtiifu na mwaminifu kwa Jumuiya.  Tunatimiza ipasavyo wajibu wetu kwa Jumuiya na kushiriki kwa ukamilifu katika ujenzi wake na utengamano ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.  Sabahu ya wenzetu watatu kuamua kufanya mambo yahusuyo Jumuiya yetu peke yao kwa kweli haieleweki.   

Mheshimiwa Spika;
Tunasikia eti kuwa baadhi yao walipoulizwa kwa nini wengine hatupo wakasema kuwa wao wametangulia na sisi tutakapokuwa tayari tutajiunga.  Yaani wana Umoja wa Waliokuwa Tayari (Coalition of the Willing).  Hivi ni nani hayuko tayari (who is not willing?)  Haiwezekani watu waitane wenyewe bila ya kutualika halafu wadai kuwa wao ndiyo wako tayari na kujenga dhana kuwa sisi wasiotualika ndiyo ambao hatuko tayari.  Madai hayo hayana ukweli.  Ni vyema waseme ukweli.  Kama walitualika tukakataa ndiyo wanaweza kusema hayo.        

Mheshimiwa Spika;
Kumekuwepo na madai kutoka kwa baadhi ya wenzetu, eti kwamba Tanzania haina moyo wala dhamira ya dhati ya kuendeleza  utengamano wa Afrika Mashariki.  Kwa sababu hiyo inasemekana eti nchi yetu imekuwa kikwazo kwa maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwamba Tanzania tunawachelewesha wengine kupiga hatua za haraka.  Wanadai kama siyo hivyo Jumuiya ya Afrika Mashariki ingekuwa mbali kwa maendeleo. Maneno hayo yamekuwa yanarudiwa au kujirudia mara nyingi kiasi cha kuwafanya baadhi ya watu wa Afrika Mashariki na hata kwingineko duniani waamini hivyo.    

Mheshimiwa Spika;
Napenda kusema kwa dhati ya moyo wangu kwamba madai hayo hayana ukweli wo wote.  Isitoshe hata sababu zinazotolewa kuthibitisha ukweli wake hazina mashiko.  Hazifanani na ukweli kuhusu Tanzania na Watanzania walivyo.  Tanzania ni muumini wa dhati wa umoja na utengamano wa nchi za Afrika Mashariki na Afrika.  Tumethibitisha hivyo kwa vitendo kwa kuunganisha nchi zetu mbili huru yaani Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika na kuwa taifa moja liitwalo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Muungano wa nchi zetu mbili ndio pekee uliodumu kwa muda mrefu kuliko yote Afrika.  

Mheshimiwa Spika; 
 Tanzania ni mwanachama mwaminifu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa maana ya kutekeleza Mkataba ulioanzisha Jumuiya hiyo, kwa Itifaki zake na maamuzi halali ya vikao na taasisi za Jumuiya.  Kama lipo jambo ambalo hatujalifanya ilivyotakiwa itakuwa ni kwa sababu za msingi na siyo kwa sababu ya kupuuza Jumuiya. Tunaithamini sana Jumuiya na tumeipa kipaumbele cha juu.  Hatuwezi kuhangaika kwa gharama kubwa ya muda wetu, fedha zetu na kutoa mchango wa hali na mali kuianzisha, kujenga na kuifikisha Jumuiya hapa ilipo halafu tuwe ni watu tunaoongoza kutokuipenda na kudhoofisha maendeleo na ustawi wake. Ni maneno ya kushangaza na wala hayaingii akilini.  Ama kweli akutukanae hakuchagulii tusi.

Mheshimiwa Spika;
          Nionavyo mimi msimamo wetu kuhusu kuharakisha Shirikisho na masuala ya ardhi, ajira, uhamiaji, pengine ndiyo yanayotuletea hisia zisizokuwa sahihi juu yetu.  Mimi siamini kama kuna mengine.  Hata hivyo, napata taabu kuamini kwamba kutofautiana kwa mawazo katika mambo hayo kutapelekea baadhi ya wenzetu wasipende hata kushirikiana nasi kwa mambo ambayo hayana matatizo na tumekuwa tunashirikiana vizuri. 


Mheshimiwa Spika;
Tanzania imekuwa inawasihi wanachama wenzetu kuwa tujenge Jumuiya yetu hatua moja baada ya nyingine kama ilivyo kwenye Mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki.  Hatuna tatizo la kuongeza kasi ya ujenzi wa Jumuiya lakini tusivuke hatua yo yote.  Tusiende kasi ya kupindukia. Mkataba unaelekeza tunaanza na Umoja wa Forodha, inafuatia Soko la Pamoja kisha Umoja wa Kifedha na hatimaye Shirikisho la Kisiasa. 

Mheshimiwa Spika;
          Ni kweli kabisa hatukuunga mkono kuharakisha Shirikisho la Kisasa kabla ya kukamilisha baadhi ya hatua.  Na, tulifanya hivyo kwa nia njema ya kutaka Shirikisho lijengwe juu ya msingi imara.  Na, msingi huo si mwingine bali utengamano wa kiuchumi kwa maana ya Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja na Umoja wa Kifedha zilizojengeka vizuri na kufanya kazi ipasavyo na kunufaisha wanachama wote sawia.

Mheshimiwa Spika;

          Lazima tutambue ukweli kuwa kunufaika kiuchumi ndicho kichocheo kikubwa cha nchi kujiunga na kuendelea kuwa mwanachama wa Jumuiya yetu.  Kama mambo ya kiuchumi yakipangika vizuri na kila nchi ikanufaika sawia, unajenga msingi imara kwa Shirikisho la Kisiasa kustawi na kudumu.  Kama ngazi hizi tatu za awali hazitashughulikiwa vizuri na nchi wanachama zikahisi hazinufaiki ipasavyo, Shirikisho litayumba au kuyumbishwa hivyo kudumu kwake kutakuwa kwa mashaka.



Mheshimiwa Spika;
          Tanzania ni kati ya zile nchi zinazotaka ngazi zote za mchakato wa utengamano zitekelezwe moja baada ya nyingine bila kuruka hata moja.  Kwa msimamo na mtazamo wetu,  Shirikisho iwe ndiyo hatua ya mwisho.  Na huo siyo msimamo wangu au wa Serikali peke yake, ndiyo msimamo wa Watanzania walio wengi.
          Bila ya shaka sote tutakumbuka kuwa mwaka 2006 Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya waliunda Kamati Maalum katika kila nchi kukusanya maoni ya wananchi kuhusu kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki.  Kwa hapa nchini Kamati hiyo iliongozwa na Profesa Samwel Wangwe na katika taarifa yake,  Kamati ilieleza kuwa asilimia 74.4 ya Watanzania wanaunga mkono kuwepo kwa Shirikisho lakini ni asilimia 25.4 tu ndiyo waliunga mkono kuharakishwa kwake. 

Mheshimiwa Spika;
          Takwimu hizi zinaelezea ukweli kuhusu hisia za Watanzania, kuhusu kuwepo kwa Shirikisho na kasi ya utekelezaji wake.  Watanzania wengi sana wanaunga mkono kuwepo kwa Shirikisho la Afrika Mashariki lakini wanataka jambo hilo lisifanywe haraka haraka.  Wanataka lifanywe kwa umakini mkubwa na tuende hatua kwa hatua kama ilivyoainishwa katika Mkataba uliounda Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Spika;
          Sera na msimamo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakwenda sambamba na ile ya wananchi wa Tanzania.  Ndiyo maana tumeafiki mapendekezo ya Kamati ile ya mwaka 2004 iliyoongozwa na Mheshimiwa Amos Wako wakati ule akiwa Mwanasheria Mkuu wa Kenya.  Kamati hiyo iliundwa kupendekeza namna ya kuharakisha utekelezaji wa mchakato wa utengamano wa Afrika Mashariki.
          Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umetamka muda wa kutekeleza ngazi ya Umoja wa Forodha lakini uko kimya kuhusu ngazi zilizofuata.  Ili kuondoa kasoro hiyo na kwa nia ya kuharakisha Shirikisho Kamati ilipewa jukumu la kutoa maoni na mapendekezo juu ya namna ya kufanya hivyo.  Kamati ilifanya kazi nzuri ya kupata maoni na hisia za watu wa makundi mbalimbali katika nchi wanachama kuhusu ujenzi wa Jumuiya na utengamano.

Mheshimiwa Spika;
          Kwa upande wa Tanzania kwa mfano, Kamati ya Mheshimiwa Amos Wako ilitambua hisia za Watanzania kuhusu ardhi na ajira na kupendekezwa kuwa masuala hayo yabaki kwenye mamlaka ya nchi wanachama kuamua.  Kuhusu mchakato wa utengamano Kamati ilipendekeza kwanza kwamba mchakato wa ujenzi wa Umoja wa Forodha uachwe mpaka ufike ukomo wake wa miaka mitano.  Baada ya hapo muda wa kutekelezwa ngazi zinazofuata unaweza kupunguzwa.  Kwa mfano walipendekeza kuwa matayarisho ya kuunda Soko la Pamoja yaanze hata kabla ya mchakato wa Umoja wa Forodha kufika mwisho ili mara wakati huo ukifikiwa Soko la Pamoja linaanze.  Hivyo hivyo mara baada ya ngazi hiyo kuanza matayarisho ya kuanza ngazi ya Umoja wa Kifedha yanaanza.  Ngazi hiyo nayo ikianza matayarisho ya kuunda Shirikisho yanaanza.  Kamati pia imetoa mapendekezo ya namna ya kufikia uamuzi kuhusu Shirikisho kwamba wananchi wa nchi wanachama wataamua kwa kura.  Tukifuata mapendekezo ya Kamati ya Mheshimiwa Amos Wako na wenzake kama tufanyavyo sasa Tanzania haina matatizo nayo.

Mheshimiwa Spika;
          Baada ya kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na wana-Afrika Mashariki kuhusu ujenzi wa Jumuiya yao inasikitisha kuona vinafanyika vitendo vinavyoanzisha mivutano kuhusu mambo yaliyokwisha fanyiwa kazi na kuamuliwa.  Tunapata taabu zaidi pale watu wanapobagua wenzao na wanapofanya mambo yanayopingana na Mkataba wa Jumuiya na Itifaki zake.  Kwa kweli kama mwenendo huu hautabadilika sijui mambo yatakuwaje mbele ya safari. 

Mheshimiwa Spika;
Nchi yetu inapenda kuona kuwa tunakuwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyo imara na iliyo endelevu.  Jumuiya ambayo inaendeshwa vizuri, mambo yake ni mazuri na nchi zote wanachama na watu wake wananufaika nayo, na hivyo wanaifurahia.  Tanzania haina tatizo na kuharakisha mchakato wa utengamano, lakini tunapata taabu kuruka baadhi ya hatua kabla hazijakamilika.   Tunawaomba wenzetu kuwa makini katika kila hatua tunayochukua.  Bila ya kufanya hivyo,  Jumuiya yetu itakuwa imejengeka katika msingi dhaifu hivyo ustawi na uhai wake utakuwa na changamoto nyingi.  Hatupendi ya mwaka 1977 yatokee tena.

Mheshimiwa Spika;
          Napenda kuwahakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushiriki katika shughuli za Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuimarisha utengamano wa Afrika Mashariki kwa kuzingatia matakwa ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Itifaki zake.   Tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa Jumuiya haidhoofiki wala kufa.  Na iwapo itadhoofika au kufa kamwe hatutaki Tanzania inyooshewe kidole kuwa chanzo wala kichocheo chake.  Ndiyo maana, hatutachoka kuzungumza na wenzetu kuhakikisha kuwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki inaendelea kustawi. 
Tutaendelea kukumbushana umuhimu wa kufanya mambo yanayojenga na kuepuka yale yanayoweza kubomoa.  Tutakumbushana umuhimu wa kuheshimu matakwa na masharti ya Mkataba ulioanzisha Jumuiya, Itifaki zake na maamuzi halali ya vikao rasmi na asasi za Jumuiya.  Tukifanya hivyo Jumuiya ya Afrika ya Mashariki itadumu, itazidi kustawi na kunufaisha nchi wanachama na watu wake kama yalivyo malengo na madhumuni ya kuundwa kwake.   
Mungu Ibariki Afrika
Mungu Ibariki Tanzania
Idumu Jumuiya ya Afrika Mashariki

Mheshimiwa Spika na
Waheshimiwa Wabunge;

                   Asanteni sana kwa kunisikiliza
Hotuba kutoka Ikulu Blog

Written by

0 comments: