Wamarekani Wafanya Upasuaji wa Ngiri Korogwe


Timu ya madaktari bingwa  saba kutoka nchini Marekani imefika  wilayani Korogwe katika hospitali ya wilaya ya Magunga kwa ajili ya kufanya upasuaji  maalumu wa ngiri kwa kutumia teknolojia ya  kisasa zaidi ya Mesh ambayo husababisha  ngiri kukoma na kutojirudia kabisa licha ya ugonjwa huo kuwa na tabia ya kujirudiarudia.

Akizungumza na waandishi  wa habari waliofika hospitalini hapo jana, Mganga Mkuu wa wilaya hiyo Dkt Rashid Said alisema kuwa zoezi hilo la upasuaji lililoanza mwishoni mwa wiki hii litadumu kwa muda wa wiki moja chini ya  madaktari bingwa toka Marekani  kwa ushirikiano na Madaktari wazawa.

Dkt Rashid alieleza kuwa  walipokea wagonjwa 150 waliofika kujiandikisha mwanzoni mwa wiki hata hivyo waliothibitika kuwa na ngiri kati yao ni Wagonjwa 95 wakiwemo wanawake 5 na watoto 8 na kuongeza kuwa mpaka siku hiyo wagonjwa 28 walikwishafanyiwa upasuaji  na zoezi lingeendelea mpaka Novemba Mosi na baadae kuendel;ezwa  na madaktari wazawa.
Aidha Dkt Rashid aliongeza kuwa  ujio huo wa madaktari hao bingwa umetokana na uhusiano mzuri uliojengwa na makanisa ya Anglikana ya Tanga na Zanzibar nchini Tanzania kupitia  Muungano wa vyuo vikuu vinavyotoa elimu ya afya nchini Marekani ambao ulituma Mwakilishi wao mapema mwezi mei mwaka huu ambapo matokeo ya safari yake ndiyo yamepelekea program ya zoezi hilo la upasuaji  linalofanywa na  taasisi   isiyo ya kiserikali ya nchini Marekani inayojishughulisha na upasuaji wa ngiri ya Global health Operation Hernia.

Naye Mwenyekiti wa kamati ya huduma za jamii wa Halmsahauri ya wilaya ya Korogwe na diwani wa kata ya Kerenge, Shebila Shebila  aliwasihi  Wananchi kuunga mkono jitihada hizo kwa kuachana na uvumi wa mitaani kuhusu upasuaji huo maalum na kujitokeza kwa wingi zaidi hata baada ya madaktari  hao kuondoka kwani pamoja na kuja kutoa huduma pia wamekuja kwa lengo la kuacha ujuzi  wa teknolojia ya kisasa na vifaa tiba vitakavyoendelea kutumika hospitalini hapo.

Wakati huohuo Abas Salehe mmoja wa wagonjwa waliofanyiwa upasuaji huo amesema kuwa  amehudumiwa vizuri sana  na imemshangaza jinsi upasuaji huo unavyofanyika  haraka na ndani ya muda mfupi Mgonjwa anaendelea na maisha yake ya kawaida kama ilivyomtokea yeye  tangu afanyiwe upasuaji huo juzi.

Naye Dkt Karl Moser ambaye ni kiongozi wa timu hiyo alisema kuwa wamefurahi sana kuwahudumia wananchi wa Korogwe kwani imempa nafasi ya kufurahia ukarimu wa Watanzania aliousikia miaka mingi na kuongeza kuwa Magunga ni hospitali iliyoongoza kwa kujipanga vizuri katika zoezi hilo akilinganisha na nchi za Gambia na Ghana alizotangulia kufanya zoezi hilo hapo awali.

Habari na  Fatna Mfalingundi-Afisa Habari wa Halmashauri ya Korogwe Vijijini


Written by

0 comments: