TANROADS Yalia na Wahujumu Barabara
Meneja wa TANROADS Eng.
Alfred Ndumbaro amewataka wakazi wa Tanga kuenzi barabara zilizojengwa katika Mkoa
wa Tanga kwa kuacha kuhujumu barabara hizo. Rai hiyo imetolewa wakati wa kikao
cha cha pili cha mwaka cha bodi ya barabara wakati akiwasilisha changamoto
zinazomkabili wakala wa barabara katika utekelezaji wa majukumu yake. Kikao cha
Bodi ya Barabara kinafanyika katika Ukumbi wa Ofisi za Mkuu wa
Mkoa leo hii na Mwenyekiti wake akiwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Chiku Gallawa.
Eng. Ndumbaro amebainisha kuwa
wananchi wamekuwa na tabia ya kuhujumu miundombinu ya barabara kwa wizi wa
alama za barabarani pamoja na ung’oaji wa makalvati ya chuma, ung’oaji wa mawe
yanayojengwa katika barabara kwa lengo la upimaji na kumbukumbu za kitaalamu,
ulimaji wa mashamba karibu sana na barabara unaosababisha mmomonyoko wa ardhi
na hivyo kusababisha mifereji ya barabara kujaa udongo na takataka kila wakati.
Akihoji mchango wa
wananchi katika kuenzi juhudi za Serikali katika kuboresha barabara, Eng
Ndumbaro amesema kuwa ni kawaida kuona mifugo ikipita katikati ya barabara kana
kwamba wananchi hawajali wala hawajui madhara ya tabia hiyo licha ya elimu na
maonyo mengi kutoka kwa Serikali.
Umefika wakati sasa
wananchi kujua kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inatumia fedha nyingi katika kujenga na kukarabati
barabara katika Mkoa wa Tanga.
Ni wito wa TANROADS kwa
wananchi kutunza barabara Mkoani Tanga ili ziweze kudumu kwa muda mrefu hasa
zilizojengwa kwa kiwango cha lami kwa kutozidisha uzito wa mizigo, kutojenga
kwenye eneo la hifadhi ya barabara, kutunza na kuheshimu alama za barabarani na
mwisho wananchi waelewe Barabara nzuri ni kwa maendeleo ya Mkoa na
Taifa kwa ujumla.
0 comments: