Utekelezaji Mradi wa Ujenzi Bandari ya Mwambani Matumaini Yaongezeka

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu ilipotembelea eneo  la Mwambani Wilayani Tanga ambalo limetengwa maalumu kwa ajili ya ujenzi wa Bandari ya Mwambani 

Wawekezaji wa Kimataifa 16 kati ya 22 waliowahi kujitokeza na kuonesha nia ya kuingia katika kinyang’anyiro cha kuwekeza katika ujenzi wa Bandari mpya ya kisasa ya Mwambani wameanza kujaza Zabuni.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Bandari (TPA) nchini, Madeni Kipande amesema hayo wakati akijibu swali la mwandishi wa habari aliyetaka kujua hatua iliyofikiwa kwenye mchakato wa ujenzi huo wakati wa mkutano na wadau wa Bandari uliofanyika jiji Tanga.

Alisema mchakato unaenda vizuri kwa kuwa hivi sasa wawekezaji hao wanaendelea kujaza zabuni zao na kuziwasilisha TPA ili kuruhusu kazi ya kumpata mwekezaji atakayetekeleza mradi huo kuendelea .

“Sasa hivi zabuni zinaendelea kujazwa hadi mwisho wa mwezi huu wa Novemba ili kuruhusu zoezi la kuzichambua liweze kufanywa mapema mwezi ujao”, alisema na kuongeza.

“Awali Kampuni 22 za kimataifa ndizo zilionesha nia ya kutaka kuwekeza kwenye ujenzi wa Bandari ya Mwambani lakini baadae serikali ikaona kwamba 16 ndizo zina uwezo mzuri wa kufanya kazi hiyo na ndizo zinazojaza Zabuni sasa”, alibainisha.

Aidha, Madeni aliwataka watendaji wa mamlaka hiyo mkoani Tanga kuendelea kujituma na kukubaliana na mabadiliko chanya yenye lengo la kuiwezesha bandari ya sasa ya Tanga kufanya kazi ki biashara zaidi kama ya Dar es salaam.

Awali Kaimu Meneja wa TPA Tanga, Freddy Liundi akizungumzia hali ya utendaji katika bandari hiyo alisema serikali imeendelea kuboresha mazingira ya utendajikazi ikiwemo ununuzi wa vifaa mbalimbali ili kuiongezea uwezo.

“Tunaendelea kujengewa uwezo na sasa tutarajia kupokea matishari matatu yenye uwezo wa kupakia tani 3,500 ya kichele na makasha 96 ya ukubwa wa futi 40 na makasha 192 ya futi 20 ifikapo katikati ya mwezi Disemaba mwaka huu”, alisema

Alibainisha kwamba matishari hayo pamoja na vifaa vingine yatasaidia sana kazi ya upakiaji na upakuaji wa mizigo gatini ambao awali ulikuwa ukisuasua.

Aidha, alisema pamoja na kuendelea kuboresha huduma kwa wateja wake kwa lengo la kuwavuta wengi zaidi ili waitumie bandari hiyo wamepokea krini kubwa moja yenye uwezo wa kubeba tani 63 hatua aliyowezesha bandari hiyo kuwa na krini tatu sasa.

“Kwa ujumla tija katika bandari ya Tanga sasa inaridhisha wastani wa tani kwa genge kwa shifti kwa shehena ya kichele imekuwa ya kiwango cha juu kiasi cha kupakua tani 8,000 kwa saa tofauti na awali”,alisema.

Na Anna Makange Habari Leo


Written by

0 comments: