Maonesho ya biashara na uwekezaji kujumuisha mataifa 30 mei 2014 Mkoani Tanga .
Maonesho ya biashara ya
kimataifa yaliyofanyika mwaka jana kwa mara ya kwanza jijini Tanga ambayo yaliandaliwa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Tanga kwa ushirikiano na Tantrade mwaka huu yanatarajiwa kufana zaidi kwa kuwa
yatajumuisha mataifa 30 tofauti na mwaka jana ambapo ni mataifa 8 tu
yalishiriki.
Hayo
yamesemwa na Mwenyekiti wa TCIAA mkoa wa Tanga
Paulo Bisoki wakati wa kikao kazi kati ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga na
maafisa Uwekezaji Viungo “Focal persons” wa Halmashauri zote za Mkoa kilichofanyika jana katika ukumbi wa mikutano
wa ofisi ya Mkuu wa mkoa.
Bisoki aliongeza kuwa
maonesho hayo yatakayofanyika kwa siku kumi mwezi Mei katika viwanja vya
Tangamano mwaka huu yameboreshwa zaidi kwa kuwa yatakuwa ni maonesho ya
biashara na uwekezaji ambayo yatawakutanisha kwa pamoja wajasiriamali wadogo na
wawekezaji wanaotafuta fursa za kuwekeza katika mkoa wa Tanga na hivyo kuwataka
maafisa viungo wa uwekezaji kujiandaa kikamilifu.
“Katika siku hizo kumi
kutakuwa na siku maalumu za kukutana kati ya wawekezaji na maafisa viungo wa uwekezaji ili kufafanua zaidi fursa zilizopo
katika maeneo yenu,mtapanga siku watembelea hayo maeneo na kujionea wao wenyewe
hivyo mjiandae vilivyo”alisema Bisoki.
Kwa upande wake Mkuu wa
Mkoa wa Tanga Mh.Chiku Gallawa aliwataka mafisa hao kutambua kuwa nafasi
waliyoipata ni nyeti na ina changamoto kwani kazi kubwa waliyonayo ni
kuwakwamua kiuchumi wananchi wa mkoa wa Tanga kutoka hali duni walizonazo kupitia uwekezaji.
“Kazi mliyopewa
inahitaji umakini na unadhifu hasa katika suala la mawasiliano ambayo yanapaswa
kufanyika kwa wakati na kumvutia Mwekezaji hadi kivutio kimoja kinapopata
Mwekezaji,jukumu lenu ni kuwatoa Wananchi katika lindi la umasikini kwa kuingia
ubia na wawekezaji na si kugeuzwa manamba.” Aliongeza Gallawa.
Kadhalika Mh.Gallawa
aliziagiza Halmashauri zote kutenga maeneo maalum na kuyaweka tayari kwa ajili
ya uwekezaji wa viwanda na kuongeza kuwa msukumo wa uwekeaji unaelekezwa zaidi
katika ujenzi wa viwanda ili kuwakwamua vijana wengi wasio na ajira na tayari
balozi tatu nchini zipo tayari kusaidia katika uwekezaji huo wa viwanda.
Maonesho hayo
yatakayofanyika mwezi Mei itakuwa ni mwendelezo wa jitihada za kuinua pato la
mkaazi wa Tanga kufikia Tsh 1,500,000/-ambapo Septemba 2013 lilifanyika
kongamano la uwekezaji ambalo lilijumuisha mikoa ya kanda ya Kaskazini ya
Kilimanjaro,Arusha,Manyara na Tanga waliokuwa wenyeji wa kongamano hilo.
Maafisa uwekezaji wa
Halmashauri za Mkoa wa Tanga wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa kabla ya kuanza
kuwasilisha mipango kazi yao.
Afisa uwekezaji
Halmashauri ya wilaya ya Korogwe Lameck Kajala akiwasilisha mpangokazi wa
Halmashauri yake
0 comments: