RC awafunda Maafisa uwekezaji wa Halmashauri.


Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mh. Chiku Gallawa amewataka maafisa uwekezaji viungo wa Halmashauri zote mkoani hapa kuwa wabunifu wa kuibua vivutio vitakavyowavutia wawekezaji na hatimaye waweze kubadilisha kipato cha Mwananchi wa Tanga na kufikia Tsh.1,500,000/- kwa mwaka.

Gallawa ameyasema hayo juzi katika kikao kazi na maafisa hao kilicholenga kuwatambulisha maafisa uwekezaji wa wilaya na kufanya tathmini ya maendeleo ya hali ya uwekezaji baada ya kongamano lililofanyika Septemba 2013 likijumuisha mikoa ya kanda ya kaskazini kwa lengo la kutangaza fursa ilizonazo.
Alisema kuwa kipaumbele cha mkoa kufikia 2015 ni kuongeza pato la Mwananchi hivyo amewaita maafisa hao ili waweze kueleza wamefanya nini mara baada ya kumalizika kwa kongamano la Septemba na mikakati yao ya kuendeleza uwekezaji katika mkoa wa Tanga.

“Nimewaita hapa ili  mpate kufahamiana,kubadilishana uzoefu na kuweza kushirikiana katika kukuza uwekezaji ndani ya mkoa na hatimae muweze kuongeza kipato cha Mwanatanga kwani hicho ndiyo kipaumbele chetu kufikia 2015.” Aliongeza Gallawa.

Aidha aliongeza kuwa maafisa uwekezaji wanapaswa kuwa wabunifu,waaminifu na wenye uwezo wa kutambua fursa zilizopo pamoja na taasisi wanazoweza kushirikiana nazo katika maswala ya uwekezaji kama MUVI na SIDO waliokuwa washiriki wa kikao hicho na kueleza kuwa Mkoa unajipanga kuwajengea uwezo wa kitaalamu maafisa hao ili waweze kutimiza lengo.

Kwa upande wake afisa uwekezaji wa mkoa Mussa Mlawilo aliwataka maafisa hao kuongeza ufanisi katika kushughulika na mpango wa ubia wa sekta binafsi na sekta ya umma katika uwekezaji (PPP) ili kujenga uchumi hai na endelevu wa mkoa.

Kadhalika aliongeza kuwa maafisa hao wanapaswa kuwa wakarimu na wenye kujali zaidi huduma kwa mteja, kuepukana na migogoro na hatimae kuvuta wawekezaji wapya kwani wawekezaji hao wakichukua 75% ya fursa zilizopo mkoani Wananchi wa Tanga wataondoka katika hali ya umasikini,kuongeza pato la taifa na maafisa hao watakuwa ni mfano wa kuigwa kwa kuwajibika ipasavyo .
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mh.Chiku Gallawa akiwahutubia maafisa wawekezaji wa Halmashauri.

 




Written by

0 comments: