Hotuba ya Mhe. Chiku Gallawa, Mkuu Wa Mkoa Wa Tanga Kwenye Mkutano Wa Nne wa Baraza La Wafanyakazi Wa TANROADS



HOTUBA YA MHESHIMIWA CHIKU GALLAWA, MKUU WA MKOA WA TANGA KWENYE MKUTANO WA NNE WA BARAZA LA WAFANYAKAZI WA TANROADS KWENYE UKUMBI WA HOTELI YA TANGA BEACH RESORT – JIJINI TANGA
TAREHE 17.6.2014

·       Mheshimiwa Bi. Hawa Mmanga – Mwenyekiti Bodi ya TANROADS
·       Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi;
·       Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza,
·       Wageni Waalikwa,
·       Mabibi na mabwana.

1.  Awali ya yote nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutukutanisha hapa tukiwa ni wenye afya njema, aidha  niwashukuru sana hasa Mtendaji Mkuu kwa  kunialika kujumuika nanyi leo kufungua rasmi mkutano wenu wa nne wa Baraza la Wafanyakazi wa TANROADS. Kwa nafasi niliyo nayo niseme karibuni sana Tanga na mjisikie mko katika Mkoa unaokuwa kwa kasi na rafiki katika kujiletea maendeleo.

2.  Napenda kuchukua nafasi hii pia kuwapongeza na kuwashukuru kwa kazi nzuri ambayo mnaendelea kuifanya katika kuratibu na kusimamia matengenezo, ukarabati na ujenzi wa barabara kuu na za mikoa, kusimamia na kudhibiti uzito wa magari pamoja na kulinda maeneo ya hifadhi ya barabara. Hizo kwa hakika ndizo shughuli zinazohitaji ushirikishwaji wafanyakazi wote wa Wakala katika kuzipanga na kuzitekeleza.

3.  Sekta ya ujenzi hasa wa barabara inahitaji uaminifu wa kweli na moyo wa kujituma ili kuweza kuleta tija na ufanisi katika ujenzi wa Taifa letu. Ubora wa miundombinu ya barabara unatupa fursa ya kujiletea maendeleo kwani usafirishaji wa bidhaa na malighafi mbali mbali unarahisishwa.

4.  Ninatambua kazi kubwa zinazofanywa na TANROADS na msingi wa utekelezaji wa kazi hizo ni kuwa na chombo ambacho kitawakutanisha Menejimenti na Wafanyakazi kuweza kukaa pamoja kupanga na kujadili namna iliyo bora ya utekelezaji wake. Njia iliyo bora ya kukaa na kupanga pamoja ni kupitia mikutano kama hii ya Baraza kwani kwenye mkutano kama huu, Wafanyakazi wanayo nafasi kubwa ya kuzungumza kwa uwazi na Menejimenti juu ya mambo ambayo yanaweza kwa kiasi fulani kukwamisha utekelezaji wa mipango hiyo. Ninayaongea haya kwa sababu ni ukweli usio pingika kwamba majadiliano na ushirikishwaji ndio dhana na njia pekee yenye kuleta tija hasa mahali pa kazi. Tunahitaji kujenga moyo wa kushirikishana katika kila jambo ili kujenga utamaduni wa kufanya kazi kwa uwazi pasipo kificho na kuondoa kabisa dhana  iliyozoeleka ya Menejimenti kufanya mambo yao peke yao na Wafanyakazi kuamua kufanya mambo yao peke yao katika mfumo wa kutoa maagizo toka juu yaani TOP DOWN APPROACH.
5.  Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi ni wawakilishi wa Wafanyakazi wenzao ambao ndio watendaji na watekelezaji wa majukumu ya kila siku ya kazi za Wakala, Wajumbe mnatakiwa kutambua jukumu kubwa mlilopewa na Wafanyakazi wenzenu katika kupanga mipango na kuandaa njia bora na mikakati ya namna ya kutekeleza pasipo kwenda kinyume na Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma. Hakika tunapaswa kila mmoja wetu kutambua jukumu hilo na liwe chachu ya kuendelea kujituma na kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kuleta tija kwa Taifa letu.

6.  Sisi Serikali tunatambua jukumu kubwa mlilokabidhiwa katika kuratibu, kusimamia matengenezo na ujenzi wa barabara hapa nchini, tunapaswa kutekeleza jukumu hilo kwa kuzingatia miiko tuliyojiwekea na kuhakikisha kwamba hakuna hata mmoja wetu anajaribu kwa njia yoyote ile kutaka kuharibu taswira nzuri ya Wakala. Tunatambua umuhimu wa kazi zenu na kila mtu anasifu utendaji kazi ulio bora wa Wakala, sifa hizo ziendelee kwa kuongeza kasi ya utendaji na kufikia malengo na mipango mliyojipangia. Kwa kufanya hivyo kutasaidia kujenga Wakala ulio bora nchini, Afrika na Dunia na hata kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa pamoja na malengo ya Millenia kwa kupunguza umaskini kwa Nusu.

7.  Yapo mambo ambayo ni muhimu tuendelee kukumbushana kila wakati, uadilifu katika utendaji wa kazi ni jambo la muhimu sana kulizingatia kwa kila mmoja wetu, tukiwa waadilifu basi hata kazi zetu zitakuwa zinazingatia ubora kwa thamani ya fedha tunazolipa kwa Makandarasi. Hili ni jambo la msingi kabisa kulizingatia ili kujenga taswira iliyo bora kwa jamii  inayotunguzuka. Nalisema hili kwa dhati kabisa kwani tusije tukaharibu sura nzuri ambayo tayari imeanza kujengeka na kuaminiwa miongoni mwa Wananchi. Aidha, sambamba na uadilifu, ubora wa kazi zetu nao ni msingi ambao lazima tuuangalie kwa umakini sana kwani nayo ni sehemu muhimu ambayo kila mwananchi anatamani kuona inafanywa kwa kiwango cha juu sana.

8.  Aidha, naendelea kukumbusha kuendelea kufanya kazi na Makandarasi waliosajiliwa na ambao wanafanya kazi kwa kuzingatia thamani ya fedha inayolipwa. Wakala usiwape kazi Makandarasi ambao hawajasajiliwa na Bodi husika kwani kwa kufanya hivyo kutachangia kupata matokeo yasiyo bora na yasiyolingana na thamani halisi ya fedha tunazolipa.

9.  Sekta ya ujenzi hasa wa miundombinu ya barabara ni kiungo muhimu sana katika kuchangia maendeleo ya uchumi wa nchi na ustawi wa wananchi wake katika nchi yetu, hivyo tutambue kwamba tunajukumu la kuhakikisha sekta hii nyeti inaendelea kuwa kielelezo cha kweli katika kufanikisha ustawi wa nchi yetu. Kwa hakika tunalo jukumu kubwa sana katika kuendelea kujenga uchumi wa taifa hili kwa manufaa ya wananchi wa nchi hii.

Kwa furaha kubwa sasa nachukua nafasi hii kutamka kuwa mkutano wa nne wa Baraza la Wafanyakazi wa TANROADS umefunguliwa rasmi.

AHSANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA.








Written by

0 comments: