Hotuba Ya Mkuu Wa Mkoa Wa Tanga Mhe. Chiku A.S. Gallawa Katika Ufunguzi Wa Semina Ya Utoaji Wa Elimu Ya Sekta Ya Hifadhi Ya Jamii Kwa Viongozi Na Watendaji Wa Mkoa Wa Tanga; 23 Julai, 2014 Katika Ukumbi Wa Ofisi Ya Mkuu Wa Mkoa Tanga
HOTUBA YA MKUU WA MKOA WA TANGA MHE. CHIKU A.S. GALLAWA
KATIKA UFUNGUZI WA SEMINA YA UTOAJI WA ELIMU YA SEKTA YA HIFADHI YA JAMII KWA VIONGOZI
NA WATENDAJI WA MKOA WA TANGA; 23 JULAI, 2014 KATIKA UKUMBI WA OFISI YA MKUU WA MKOA TANGA.
Ø Ndugu Mwakilishi wa
mkurugenzi Mkuu wa SSRA.
Ø Ndugu wafanyakazi
wa SSRA.
Ø Ndugu washiriki,
Ø Ndugu waandishi
wa habari
Ø Ndugu wageni
waalikwa, mabbi na mabwana
Asalam aleykum.
Kwanza kabisa
naanza kwa kumshukuru mwenyezi Mungu kwa kutujaalia Uhai na Afya njema na kuweza kuhudhuria Mkutano huu muhimu kwa wadau wa Sekta ya Hifadhi
ya Jamii. Aidha nichukue fursa hii pia kuwakaribisha sana Jijini Tanga wageni wetu wote. Naelewa
kwamba washiriki wa Semina hii ni watendaji kutoka Ofisi yangu, Halmashauri za
Mkoa waTanga na ytaasisi nyingine ndaqni ya Mkoa wa Tanga hivyo ningependa
kuwakumbusha lengo na madhumuni ya Semina
hii kwa urahisi wa rejea zenu.
Ndugu mwenyekiti wa
mkutano na washiriki, lengo kubwa la
Semina hii ni kutoa uelewa wa kutosha kuhusiana na shughuli za Mamlaka ya usimamizi na udhibiti wa Sekta ya Hifadhi za Jamii (SSRA), pamoja na
uendeshwaji wa Sekta nzima ya Hifadhi ya Jamii kwa ujumla wake, hasa
ikizingatiwa kwamba watanzania wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusiana na
shughuli za (SSRA).
Ndugu Mwenyekiti na washiriki, Nimeona ni muhimu
kwa ufupi kujua maana ya SSRA na azima
yake katika kuboresha Sekta ya Hifadhi ya Jamii Tanzania kwani Hifadhi ya Jamii
ni kwa watanzania wote.
Mamlaka ya
Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi
ya Jamii iliundwa kwa Sheria Na. 8 ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2008 na kufanyiwa marekebisho kwa Sheria namba 5 ya mwaka 2012 kwa lengo la kusimamia na kudhibiti
Sekta ya Hifadhi ya Jamii kwa Manufaa ya
wanachama na Taifa kwa ujumla Mamlaka ilianza kazi rasmi mwishoni mwa mwaka
2010.
Hivyo kuundwa kwa
Mamlaka hii ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii ya
mwaka 2003 na malengo ya Milenia,
MKUKUTA pamoja na Dira ya Maendeleo 2025.
Mamlaka ina jukumu
la kusimamia shughuli zote za Hifadhi ya Jamii nchini ikiwa ni pamoja na Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii iliyoanzishwa
kwa Sheria ya Bunge. Mifuko hii ni pamoja na PPF, NSSF, PSPF, GEPF, NHIF na LAPF. Mamlaka inahakikisha kwamba
mifuko inakuwa endelevu, mifuko inaendeshwa kwa kufuata Kanuni na taratibu za
Kisheria, wanachama wanapata taarifa za
mifuko yao, mafao yanaboreshwa kwa maslahi ya Taifa kwa ujumla.
Ndugu mwenyekiti na wajumbe, Kuanzishwa kwa
SSRA kulifanywa ili kuhakikisha kwamba Sekta ya Hifadhi ya Jamii inaendeshwa
kwa Mujibu wa Sheria na Kanuni hii ikiwa ni pamoja na kulinda Haki za
wanachama, kuongeza upana na huduma za Hifadhi za Jamii na kuzifanya huduma hizi kuwa endelevu.
Ndugu Mwenyekiti na Washiriki, Kwa kifupi pia
nizungumzie Sera ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2003. Sera hii ilitungwa
kutokana na mabadiliko ya Kijamii,
Kiuchumi na Kisiasa hapa nchni, ili kuhakikisha kuwa wananchi wanafaidika
na mfumo mzima wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii, ambao utakuwa endelevu.
Hivyo basi, Sera ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii, imetokana
na majadiliano ya Wadau mbalimbali ambayo yalianza tangu mwaka 2001. Baada ya hapo Serikali iliridhia
na kupitisha Sera hiyo rasmi 2003.
Nia kubwa ya Sera
hii ni kutekeleza Dira na kuhakikisha kuwa kufikia mwaka 2025 Sekta ya Hifadhi ya Jamii ni kwa
watanzania walio wengi.
Ndugu Mwenyekiti na
Washiriki,
Lengo kubwa la Hifafhi ya Jamii ni kuwezesha
wananchi kuishi maisha yenye staha kwa
kuwawezesha kuapata huduma za msingi pale wanapopata majanga mbalimbali
kama vile Uzee,
Ugonjwa, Uzazi kwa Mujibu wa Mafao mbalimbali yanayotolewa na mifuko hiyo
hata kabla ya kustaafu mwananchama anaweza kupata fedha za kumsaidia kufanya
mambo mbalimbali kama vile kusomesha watoto, kujenga nyumba na kukabiliana na majanga mbalimbali.
Ndugu Mwenyekiti na washiriki, tunapozungumzia
dhana ya Hifadhi ya Jamii kwa wote
tunaona kuwa hapo awali mifuko ilipoanzishwa ililenga kuwahudumia
wafanyakazi na sio watumishi wote. Sera ya mwaka 2003 imeeleza mifuko ya Hifadhi ya Jamii ihudumie
watu wote wakulima wafanyakazi, wafanyabiashara, wajasiriamali watu
waliojiajiri wenyewe na wazee, hivyo basi inatoa fursa ya Hifadhi ya Jamii kwa wote. Kauli mbiu hii inaendana
sambamba na Sera ya Wigo wa
huduma ya Hifadhi ya Jamii ili iweze kumfikia
kila Mtanzania, Serikali inapenda kuona watanzania wengi iwezekanavyo
wanajiunga na Hifadhi ya Jamii nchini bila kujali anatoka kwenye Sekta rasmi au
isiyo rasmi.
Hivi sasa Sheria ya
SSRA inaruhusu mtu yeyote wa Sekta yoyote kuwa mwanachama wa Mifuko ya Hifadhi
ya Jamii. Hifadhi ya Jamii inahusisha wote walio katika sekta rasmi na isiyo
rasmi.
Ndugu Mwenyekiti na
washiriki, Mwisho nichukue fursa hii kuishukuru sana Mamlaka ya usimamizi wa
sekta ya Hifadhi ya Jamii kwa kuamua kuja kutoa elimu ya Hifadhi ya Jamii kwa Viongozi na
Watendaji wa Mkoa wa Tanga na pia kwa kunipa heshima ya kufungua Semina
hii muhimu ya utoaji wa Elimu juu ya Sekta ya Hifadhi za Jamii. Nawashukuru pia
washiriki Mliojitokeza kutoka Mkoa huu wa Tanga ambao ni muhimu kwetu sisi
kama wawakilishi na watendaji wa
wananchi wa Tanga. Niwaombe basi elimu
hii tutakayoipata hapa tuifikishe kwa wananchi wote ili nao waelewe namna ya
kujiwekea akiba iweze kuwasaidia kujikinga na majanga mbalimbali ya Kiuchumi na
Kijamii. Naomba tuwe wasikivu na tuchangie mada zitakazo tolewa.
Ndugu Mwenyekiti na
Washiriki, kwa haya machache, napenda kusema kuwa semina hii imefunguliwa
rasmi.
Asanteni kwa kunisikiliza
0 comments: