Hotuba Ya Mkuu Wa Mkoa Wa Tanga Mheshimiwa Chiku A.S. Gallawa Katika Ufunguzi Wa Mkutano Wa Lishe Wa Wilaya Za Mkoa Wa Tanga Katika Ukumbi Wa Mikutano Wa Halmashauri Ya Jiji Tanga Tarehe 14 Julai, 2014
HOTUBA YA MKUU WA MKOA WA TANGA
MHESHIMIWA
CHIKU A.S. GALLAWA
KATIKA
UFUNGUZI WA MKUTANO WA
LISHE
WA WILAYA ZA MKOA WA TANGA
KATIKA
UKUMBI WA MIKUTANO WA HALMASHAURI
YA JIJI TANGA TAREHE 14 JULAI, 2014
·
Ndugu Naibu Katibu Mkuu
Afya – TAMISEMI,
·
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya,
·
Ndugu Katibu Tawala wa
Mkoa,
·
Ndugu Mganga Mkuu wa
Mkoa,
·
Waheshimiwa Wenyeviti wa Halmashauri,
·
Wakurugenzi wa Halmashauri,
·
Ndugu Mkurugenzi wa World Education/Pamoja Tuwalee,
·
Ndugu Mkurugenzi wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania
na Mwakilishi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,
·
Mabibi na Mabwana,
·
Wanahabari,
Kwanza,
napenda kulishukuru Shirika la World Education Inc. (WEI) linalotekeleza Mpango
wa Pamoja Tuwalee Kanda ya Kaskazini na waandaaji wengine wa mkutano huu kwa
kunipa heshima ya kuwa mgeni rasmi kwenye ufunguaji. Nikiwa mmoja wa wadau wakubwa wa masuala ya
Lishe, na hasa Lishe kwa Watoto na kina Mama, ninafarijika sana kujumuika na
viongozi wa Halmashauri za Mkoa wa Tanga kuzungumzia umuhimu
wa Lishe, hasa kwa watoto na kina Mama.
Pili,
natambua kwamba warsha hii isingeweza kufanyika bila ya Shirika la Misaada la
Marekani la USAID na Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupunguza Makali
ya UKIMWI (PEPFAR). Kwa hiyo, napenda kuwashukuru wafadhili wetu na wale wote
waliofanikisha warsha hii kwa njia moja ama nyingine.
Tatu, Jambo la muhimu
zaidi katika warsha hii ni uwepo wa Naibu Katibu Mkuu Afya-TAMISEMI, viongozi
wa mkoa, wilaya na Halmashauri zote za Tanga kwa nia ya kujikumbusha Sera, Miongozo na Mikakati
ya serikali juu ya Lishe na umuhimu wa
kuingiza maswala ya Lishe katika Mipango na Bajeti za kila mwaka za
Halmashauri. Napenda kuupongeza kwa dhati kabisa Mpango wa Pamoja Tuwalee Kanda
ya Kaskazini kwa kuandaa mkutano huu. Tunawashukuru
Sana.
Ndugu washiriki
Nimeelezwa
kwamba, shirika la WEI linatekeleza afua (interventions) za kitaifa za
kukabiliana na tatizo kubwa la utapiamlo, hasa utapiamlo wa udumavu unaoathiri
zaidi ya asilimia 42% ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano Tanzania.
Mpaka sasa WEI kwa ushirikiano na Halmashauri husika na Asasi 5 za Mkoa wa
Tanga (PASADIT, AFRIWAG, Muheza Hospice Care, TEWOREC na TALISDA) zilizopewa
dhamana ya kutekeleza Mpango wa Pamoja Tuwalee, limetekeleza zoezi la Upimaji Afya ya Watoto Shuleni na zoezi la Upimaji Hali
ya Lishe kwa Watoto ndani ya Jamii
katika Halmashauri 9 za Mkoa wa Tanga, ukiacha
wilaya za Kilindi na Mkinga.
Aidha,
matokeo ya Upimaji Afya za watoto Shuleni na matokeo ya Upimaji Hali ya Lishe
kwa watoto ndani ya Jamii yalitolewa katika Mikutano iliyoshirikisha Uongozi wa
Halmashauri husika na washiriki wakuu wa mazoezi haya. Dhumuni kubwa la
kushirikishana matokeo haya ni kuifanya Halmashauri iwe na umiliki wa zoezi na
matokeo yake, na kutafuta mbinu endelevu katika kuyatatua matatizo
yaliyobainishwa kwa kuhusisha Wadau muhimu wa Watoto na kwa kutumia raslimali
zilizopo ndani ya jamii.
Ndugu washiriki
Viwango vya utapiamlo
kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano vinavyotokana na Lishe Duni katika
Mkoa wa Tanga ukilinganisha na viwango vya kitaifa vinaonyesha kwamba:
Upungufu wa Wekundu wa Damu Kitaifa ni asilimia 58% na Tanga ni asilimia
53%
Udumavu Kitaifa ni 42% na Tanga ni 49%
Viwango vya utapiamlo
kwa kina mama katika umri wa kuzaa (miaka 15- 49) vinavyotokana na Lishe Duni
ukilinganisha na viwango vya kitaifa ni:
Upungufu wa Wekundu wa
Damu kitaifa ni 40% na Tanga ni 35%
Ndugu washiriki
Ni
dhahiri kwamba Halmashauri zote zinapaswa kuyapa kipaumbele maswala ya
Lishe ili kukabiliana na tatizo hili
kubwa la kitaifa. Hivyo basi, mkutano huu hauna budi kujadili na kuazimia kwa
pamoja namna ya kuboresha masuala ya Lishe katika Halmashauri zote 11 za Mkoa
wa Tanga.
Pamoja
na kukumbushana Sera, Mikakati na
Miongozi ya Kitaifa na afua za Lishe, mkutano huu pia utajadili mpango wa
uundaji/uhuishwaji wa Kamati za Lishe za Halmashauri pamoja na uanzishwaji wa
Dawati la Lishe katika Halmashauri zetu. Pia mkutano huu utajadili na kuandaa
Mikakati na mipango ya kuboresha utendaji wa Kamati za Lishe za Halmashauri na
uanzishwaji wa madawati ya lishe katika vituo vya tiba. Naomba mkumbuke kwamba tunafanya haya yote
ili kusaidia juhudi za Serikali za kupunguza viwango vya Utapiamlo katika Mkoa
wetu wa Tanga.
Ndugu washiriki,
Nimeelezwa
kwamba WEI inashirikiana na TFNC na serikali ya mkoa wa Tanga kufanya zoezi la
Lishe kwa Halmashauri zote 11 ili kusaidia juhudi za kupunguza viwango vya
Utapiamlo katika mkoa wetu. Zoezi hili litaanza na uundaji wa Kamati za Lishe
za Wilaya na uanzishaji wa Dawati la Lishe katika Halmashauri zetu.
Kwa
mujibu wa sera yetu ya ugatuzi wa madaraka ya mwaka 1998, ninyi Halmashauri
ndiyo watekelezaji wa Sheria, Sera, Miongozo na Mikakati ya Kitaifa ya
kuyasaidia makundi yaliyo katika hali hatarishi, wakiwamo Watoto na Kinamama,
hasa wakati wa ujauzito.
Kwa
hiyo basi, mkutano huu ni muhimu sana katika kusukuma mbele jitihada za Serikali,
siyo tu kuwasaidia Watoto na kina Mama kupata haki yao ya kupatiwa Lishe nzuri,
bali pia kusaidia serikali katika kupunguza viwango vya utapiamlo na vifo kwa
watoto na kina mama, hasa wakati wa kujifungua.
Ndugu washiriki,
Nimefarijika
zaidi kusikia kwamba pia mtajadili Mkakati wa Taifa wa Lishe uliozinduliwa na
Mheshimiwa Waziri Mkuu kule Musoma mnamo tarehe 21 Septemba, 2011. Kupitia
Mkakati huu, Wakurugenzi wa Halmashauri wanalazimika kuhakikisha uingizwaji wa
maswala ya Lishe katika Mipango ya kila mwaka ya Halmashauri zao na kusimamia
utekelezaji wake na kutoa taarifa za utekelezaji wake TAMISEMI na Wakuu wa
Mikoa kutoa taarifa kila robo kwa Waziri Mkuu. Kama nilivyosema awali, nyie
Halmashauri ndio watekelezaji wa majukumu haya ya serikali katika Mkakati wa
Taifa wa Lishe.
Ndugu washiriki,
Sasa
niulize, ni Halmashauri ngapi hapa zimetekeleza Mkakati wa Taifa wa Lishe kwa
kuhakikisha Idara za Mipango, Afya, Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Maendeleo ya
Jamii, na Elimu zinapanga bajeti na kutekeleza
miradi ya Lishe. Je, ni
Halmashauri ngapi hapa zina Mpango Kazi wa Lishe kwa mwaka huu wa fedha? Inawezekana
uelewa wa Mkakati wa Taifa wa Lishe ulikuwa bado haujaeleweka ama haujawafikia.
Lakini leo mtauelewa kwa undani ikiwemo mambo mnayoelekezwa kufanya.
Ni
mategemeo yangu kwamba baada ya mkutano huu, Idara zote zilizoelekezwa kuingiza
maswala ya Lishe kwenye bajeti zao zitafanya hivyo na taarifa za utekelezaji
zitatolewa kwa sehemu zote husika. Ni mategemeo yangu pia kwamba, viwango vya
vifo kwa watoto na kina mama vitapungua katika halmashauri zetu badala ya
kuongezeka.
Ndugu washiriki,
Mkitimiza
haya yaliyomo katika Mkakati wa Taifa wa Lishe, mtakuwa si tu kwamba mnajenga
ustawi na kuokoa maisha ya watoto na kina mama, bali pia mnachangia katika
juhudi za serikali kufikia malengo ya Milenia na kuondoa umaskini kama
ilivyoainishwa katika MKUKUTA na Visheni ya Taifa 2025.
Ndugu washiriki,
Pamoja
na hayo, ninaomba tuzingatie suala
moja muhimu. Ninapenda sote tuelewe kwamba mazingira yanayosababisha utapiamlo
na hata vifo kwa watoto na kina mama, hayaondoi ubinadamu wa watoto na
kina mama hawa. Naamini kabisa
kwamba wenzetu wahisani wanasukumwa kutupatia misaada kwa moyo wa ubinadamu
katika kusaidia watoto na kina mama kama ilivyo kwetu sote.
Tukiwa
na mtazamo huu, tutajenga imani kwamba pamoja na ukweli kwamba idadi ya watoto
na kina mama wanaofikiwa kwa huduma zetu inaongezeka,
haibaki kuwa takwimu tu katika kumbukumbu zetu, iwe kwa hawa wahisani au kwetu sisi wenyewe. Kila
huduma inayotolewa ina nafasi yake katika kuwaondolea mazingira magumu na
hatarishi na ninaamini umuhimu huu unatambuliwa,
hata na mtoto na mama mwenyewe.
Ndugu washiriki,
Napenda
kumalizia kwa kuwashukuru tena watekelezaji wa Mpango wa Pamoja Tuwalee na
Viongozi wote wa Mkoa kwa kufanikisha Mkutano huu. Wote tunaoguswa na masuala
ya Lishe tuhakikishe Sera, Mikakati na Miongozo ya kitaifa juu ya Lishe na Ustawi wa watoto na kina mama inatekelezwa
ipasavyo.
Baada ya kusema haya, sasa natamka kwamba warsha hii imefunguliwa rasmi.
ASANTENI
SANA KWA KUNISIKILIZA
0 comments: