Wahandisi Mkoani Tanga Wafundwa


Afisa Utumishi wa Halmashauri ya mji wa Korogwe Bi. Saada Malunde wakati wa ufunguzi wa kikao cha Wadau wa Maji kilichofanyika wilayani Korogwe mwishoni mwa wiki. Kushoto ni Mhandisi Ephraim Minde, Mhandisi wa Huduma za Maji Mkoa wa Tanga


  Mhandisi Ephraim Minde, Mhandisi wa Huduma za Maji Mkoa wa Tanga akitoa muongozo wa Kikao 
 
 Baadhi ya wajumbe wa kikao


Wahandisi wa maji kutoka Halmashauri zote zilizopo Mkoani Tanga wamepongezwa kwa jitihada zao za kuonyesha ubunifu wa kuanzishia utaratibu wa kuwakutanisha ili kujadiliana na kubadilishana uzoefu wa kiutendaji hatua iliyoelezwa kwamba itawezesha kusukuma mbele maendeleo kwenye sekta ya maji.

Pongezi hizo zilitolewa mwishoni mwa wiki na Afisa Utumishi wa Halmashauri ya mji wa Korogwe Saada Malunde aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wake Lewis Kalinjuna katika kufunga kikao cha wadau wa sekta ya maji kilichowahusisha wahandisi,mameneja mamlaka za maji na wasajili vyombo vya watumiaji maji
.
Akisoma hotuba yake ya ufungaji kwa niaba ya Mkurugenzi, Saada ambaye ni Afisa Utumishi alisema kitendo cha wahandisi kukutana ni kizuri ambapo kinasaidia kubadilishana uzoefu wa kazi lengo likiwa kuweza kuboresha mazingira ya kiutendaji hatua ambayo itaimarisha suala la upatikanaji wa huduma.

“Nimefurahi kusikia wahandisi mmeanzisha utaratibu wa kukutana kwenye kikao cha pamoja ni kitu kizuri,itasaidia kubadilishana uzoefu lengo likiwa kuboresha mazingira ya kiutendaji”. alisema Saada na kuwashauri wahandisi hao kuangalia uwezekano wa kushirikisha wadau wengine kwenye vikao vyao.

Aidha afisa utumishi huyo wakati alipokuwa akizungumzia suala la fedha aliwataka washiriki wa kikao hicho kuangalia uwezekano wa kuwabana kisheria baadhi ya wakandarasi ambao wamekuwa na tabia ya kuchelewesha kazi licha ya kuwepo taarifa za tatizo la uchelewaji wa fedha kutoka serikali kuu.

Awali akisoma maazimio ya kikao hicho kilichofanyika kwa siku nne kwenye ukumbi wa halmashauri ya mji Korogwe,msajili wa vyombo vya watumiaji maji wilayani Handeni Mwana Amina Mruma alisema kwa vile suala la utunzaji wa rasilimali maji ni mtambuka wadau wote wanatakiwa kushiriki kwenye utunzaji.

Maazimio mengine yaliyofikiwa kwenye kikao hicho yakilenga kuboresha maendeleo ya sekta ya maji ni juu ya miradi yote ya maji kuombewa fedha kulingana na mahitaji sambamba na hatua ya kuiombea hati za kutumia maji,kila halmashauri kupeleka mahitaji yake ya wataalam wa maji iliyopungukiwa wizarani.

Naye Katibu Tawala msaidizi huduma za maji mkoani Tanga, Mhandisi Ephraim Minde alimweleza mgeni rasmi wa ufungaji kikao hicho kwamba mada tano zimeweza kuwasilishwa akizitaja kuwa ni kuhusu sheria namba 11 na 12 ya mwaka 2012,utekelezaji miradi ya maji Tanga,mafanikio na changamoto.

Nyingine ni udhibiti na utunzaji wa rasilimali maji,utumishi wa umma na uwajibikaji pamoja na uendelevu wa huduma ya maji huku akisema ni kikao hicho cha kawaida kutathimini maendeleo ya sekta ya maji kwa halmashauri zote kutuma wawakilishi wakitilia mkazo kujua walipofikia ukamilishaji miradi ya vijiji kumi.

Mhandisi huyo alisema katika program ya vijiji kumi chini ya mradi wa maendeleo ya sekta ya maji mambo kadhaa yamejadiliwa kama vile kupitia taarifa za uendeshaji na matengenezo ya miundombinu na hali ya utoaji wa huduma ambapo pia waliweza kutembelea miradi inayoendelea kujengwa.

Mambo mengine yaliyojadiliwa ni utayarishaji wa taarifa ya maji ya robo mwaka na ya mwaka kwa kuziunganisha kimkoataarifa ambayo itatumwa wizara ya maji,kufanya tathimini ya upatikanaji wa maji katika wilaya na miji na kupitia taarifa ya utekelezaji miradi hususani program ya sekta ya maji WSDP. Habari na Fatna Mfalingundi-  Afisa Habari Halmashauri ya Wilaya Korogwe


Written by

0 comments: