Rc Tanga Aitaka Halmashauri Kuzalisha Ajira Kwa Vijana



MKUU wa Mkoa wa Tanga Luteni Mstaafu Mhe. Chiku Gallawa ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe kuzalisha ajira kwa vijana ili kuwapunguzia umasikini na kuwafanya waachane na vitendo vya uhalifu huku wakikuza uchumi wa taifa.
 Mhe.Gallawa ametoa agizo hilo mwishoni mwa wiki  alipohudhuria kikao cha baraza maalum la madiwani kupitia hoja za ukaguzi wa hesabu za serikali ambapo alisema jukumu kubwa la Serikali ni kuwaondolea umasikini wananchi wake na kusema kuwa nguvukazi ya taifa ni vijana.
Akifafanua njia za kuongeza ajira kwa vijana Mhe.Gallawa amesema kuwa hivi karibuni Shirika la Nyumba laTaifa (NHC) limetoa mashine za kufyatulia tofali maalum kwa kila Halmashauri na hivyo kuishauri  Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe kuchangamkia fursa hiyo kwa kuunda timu za ujenzi kwa kila kata na kuwapatia mafunzo vijana hao ambao mbali ya kufanya biashara  pia wangeweza kutumika kufyatua tofali za  majengo ya Serikali katika kata husika na kuongeza kipato.
Kadhalika amelitaka baraza  hilo la madiwani kuweka mazingira rafiki kwa uwekezaji kwa  kutowawekea vikwazo pindi wawekezaji watakapofika katika Halmashauri yao kwani uwekezaji ni njia endelevu ya kukuza uchumi itakayotoa ajira kwa vijana na kuongeza kuwa mkoa wa Tanga ulifungua milango ya uwekezaji kwa kufanya kongamano la kuuza fursa za uwekezaji kwa wadau mbalimbali Septemba mwaka jana.
Aidha amesisitiza kuwa ni lazima wataalamu na madiwani kushirikiana kwa pamoja kuhimiza uzalishaji endelevu na kuhakikisha pato la Mwananchi linaongezeka kufikia ml 1.5 mwaka 2015 kwani Korogwe ni Wilaya yenye utajiri wa mazao ya kila aina lakini bado hayajaweza kuwakwamua Wananchi wake kiuchumi inavyostahili.
Mhe.Gallawa ameongeza kuwa ni lazima fedha ya Serikali zifike chini kwa wananchi na kutoa matokeo yaliyokusudiwa na kusisitiza 20% ya mapato ya Halmashauri kupelekwa vijijini sambamba na 5% za wanawake na vijana ili Wananchi waone faida ya uzalishaji wao.
Mkuu huyo wa Mkoa ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kupata hati safi ya matumizi ya fedha za umma mwaka 2013/14 na kuwataka madiwani kuendelea kusimamia vyema fedha za umma huku akiwataka  watendaji kuongeza jitihada na ubunifu katika uzalishaj ili kuwaletea maendeleo Wananchi

Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani HWK akimkaribisha Mkuu wa Mkoa kuhutubia baraza hilo.Kushoto kwa RC ni Mbunge wa  Korogwe vijijini Mhe.Steven Mgonyani, Kulia kwa Mwnyekiti ni Mkurugenzi Mtendaji (W) Lukas Mweri na mwisho kabisa ni Mkaguzi Mkazi wa hesabu za Serikali Mkoa wa Tanga Dennis Kagashe. Stori & Picha na Fatna Mfalingundi, Afisa Habari wa Halmashauri ya Wilaya Korogwe.
 
 


Written by

0 comments: