Watanzania Hawawezi kuipata Katiba Mpya Kwa kumwaga Damu





Serikali imesema haiko tayari kufanya maamuzi ya kusitisha mchakato wa Katiba Mpya unaoendelea  sasa kwa sababu ya vitisho vya Viongozi wa UKAWA ambao Wametangaza kufanya maandamano nchi nzima ili  kushinikiza kuvunja Bunge la Katiba.
Hayo yamesema na Kiongozi wa  mbio za Mwenge wa Uhuru Bi Rachel Stephen Kassanda wakati akitoa ujumbe wa Mwenge  kwa Wakazi wa Negero, Kata ya Kimbe Wilaya ya Kilindi .
Kassanda amesisitiza kuwa Serikali ya Tanzania haiwezi kukubali damu ya Watanzania kumwagika kwa masilahi binafsi ya viongozi wa kisiasa. Ni historia ya Tanzania kutatua tofauti zinazojitokeza kwa vikao na mazungumzo ya amani ili kufikia mwaafaka akitolea mfano wa Baba wa taifa Mwl. Julius K. Nyerere alivyoongoza  mapambano kwa njia ya mazungumzo na hatimaye tukajipatia Uhuru.  Amewaomba wanaUKAWA kurudi bungeni ili kufanikisha  mchakato wa kuipata Katiba Mpya.
Akiwakilisha taarifa ya Mkoa wakati wa mapokezi ya Mwenge Bw. S M.Chima , Katibu Tawala Mkoa wa Tanga alisema Mkoa wa Tanga umejipanga kuona Katiba Mpya inapatikana kwa amani.
 “Mkoa  wa  Tanga  ni  miongoni  mwa  Mikoa  ambayo  imejipanga  kuhakikisha mchakato wa kupata Katiba Mpya unakwenda vizuri kuanzia ngazi ya chini, na kwa kujivunia Mkoa wa Tanga wabunge wote wapo kwa ajili ya kuwawakilisha wananchi na hakuna aliyegoma, na kwa maneno mengine Tanga hatuna UKAWA” alisisitiza Chima.
Pia  Kassanda ameendelea kuonya baadhi ya wanasiasa ambao wana nia ya kuvuruga mchakato wa Katiba Mpya kwa kusema kuwa watu wa namna hiyo hawana nia nzuri na Nchi ya Tanzania na kuwataka wananchi kuwapuuza watu wa namna hiyo.
Mwenge wa Uhuru Wilayani Kilindi umefanikiwa kutembelea miradi 6 yenye thamani ya Shilingi za Kitanzania Bilioni 9.4 ambayo ni kuzindua mradi wa maji Negero, kuweka jiwe la msingi mradi wa soko,nyumba  za watumishi na mradi wa chuo cha ufundi Mafisi, kukagua Hifadhi ya Msitu wa Asili Pinguli na ufunguzi wa mradi wa maabara Mafisi siku ya Alhamisi Agosti 14.
Sehemu ya Wananchi kutoka Kilindi wakati wa ujumbe wa Mwenge wa Uhuru Wilayani humo
 Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2014, Bi Rachel Kassanda akiwa katika Hifadhi ya Msitu wa Pinguli Wilayani Kilindi mara baada ya kuukagua
 Mkimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2014, Bw. Wito Jaston Mlemelwa kutoka  Mbeya akitoa pongezi kwa wakuliwa wakati akitembelea mabanda ya Wajasiliamali ,PCCB na Afya
 Moja kati ya Nyumba 3 za Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi zilizowekewa jiwe la Msingi wakati Mwenge wa Uhuru ulipotembelea miradi ya Maendeleo wilayani humo. Nyumba hizo ni jitihada ya Serikali katika kupunguza kero ya makazi kwa watumishi nchini.
Mbunge wa Jimbo la Kilindi Mhe. Beatrice Shelukindo akisalimia wananchi muda mchache kabla ya Salamu za utii kutolewa kwa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mlisho Kikwete jioni ya Mkesha wa Mwenge katika wilaya ya Kilindi
 


Written by

0 comments: