Tunafikiria Kufuta Ada Sekondari – Rais Kikwete


 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametangaza rasmi kuwa Serikali inaangalia uwezekano wa kufuta ada katika shule zake za sekondari, kama namna ya kuboresha Sera ya Elimu na kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi anayeanza darasa kwanza anamaliza kidato cha nne.

Aidha, Rais Kikwete amesema kwamba Serikali yake iliibua mpango wa ujenzi wa sekondari za kata kwa sababu nafasi za wanafunzi kuingia sekondari zilikuwa zimekuwa finyu kiasi cha kwamba ni asilimia kati ya sita na 10 ya watoto wote waliokuwa wanamaliza shule za msingi mwaka 2005 walikuwa wanaingia sekondari wakati anaingia madarakani.

Rais Kikwete pia amesema kuwa pamoja na kejeli nyingi zilizoelekezwa kwa shule za sekondari za kata kiasi cha kuitwa Yeboyebo katika miaka ya mwanzoni ya shule hizo, bado zimekuwa na mafanikio makubwa, ambayo ni sehemu ya mafanikio makubwa ya jumla ya Sekta ya Elimu katika miaka karibu tisa ya uongozi wake.

Rais Kikwete alikuwa anazungumza jioni ya leo, Jumatano, Agosti 25, 2014, na wanajumuia ya Chuo Kikuu cha Mzumbe cha Morogoro na wakazi wa vijiji vya jirani na chuo hicho ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Morogoro iliyoanza Agosti 20.

Katika hotuba yake ya kusisimua, Rais Kikwete ametumia muda wa kutosha kuelezea historia ya maendeleo ya elimu nchini, mabadiliko ya mwelekeo wa elimu na sera ambazo zimeongoza mageuzi makubwa katika elimu chini ya uongozi wake.

Rais Kikwete amewaambia mamia kwa mamia ya wanazuoni hao na watumishi wengine wa Chuo hicho pamoja na wanavijiji wa jirani kuwa Serikali wakati wote imekuwa inasaka kubuni sera za kuendeleza elimu nchini na wakati wote kuboresha sera hizo.

“Kwa mfano sasa hivi tunaangalia jinsi gani ya kufuta karo katika shule zetu zote za sekondari za Serikali kama namna ya kuhakikisha kuwa kila mtoto anayeanza darasa la kwanza anakuwa na nafasi ya kumaliza sekondari kwa maana ya kidato cha nne bila kulazimika kuacha shule kwa sababu ya ada,”amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Tunaangalia kuondoa ada hii ambako wazazi wanalipa Sh. elfu ishirini kwa shule za kutwa na Sh. elfu sabini kwa shule za bweni, ili watoto wetu waingie darasa la kwanza na kwenda moja kwa moja hadi kidato cha nne bila ya wasiwasi wa kukwamishwa na ada.”

Akielezea historia ya kuanzishwa kwa Shule za Sekondari za Kata, Rais Kikwete amesema kuwa wakati Serikali yake inaingia madarakani, hali ya watoto kuingia sekondari kutoka shule za msingi ilikuwa mbaya kiasi cha kwamba ni asilimia kati ya sita na 10 iliyokuwa inasonga mbele kwa sababu shule za sekondari zilikuwa chache.

“Kwa miaka mingi, tulikuwa hatukujenga shule mpya za sekondari, na kama mnavyojua wakoloni wa Kiingereza ndio kabisa hawakujenga shule. Kazi hiyo waliwaachia Wamisionari. Kwa hiyo wakati tunaingia madarakani, hali ilikuwa mbaya ndiyo maana tukaja na Sera ya Shule za Kata.”

Kwa mujibu wa takwimu rasmi, zilikuwepo jumla ya shule za sekondari 1,745 mwaka 2005 zikiwemo shule 1202 za Serikali na sasa ziko jumla ya shule za sekondari 4,576 zikiwemo shule 3,528 za Serikali.

Kuhusu maendeleo ya shule za sekondari za kata, Rais Kikwete amesema kuwa zimekuwa na mafanikio makubwa kama ambavyo Sekta ya Elimu nzima imekuwa na mafanikio makubwa.

Rais Kikwete ameelezea baadhi ya mafanikio hayo kama vile upanuzi mkubwa wa elimu ya msingi na uandikishaji wa watoto kuingia shule, upanuzi wa elimu ya sekondari, ongezeko kubwa la wanafunzi wa shule za sekondari, upanuzi wa elimu ya juu ambako sasa kuna vyuo vikuu 51, vikiwemo 15 vya umma, ongezeko la fedha za mikopo ya elimu kutoka sh bilioni 16 mwaka 2005 na kufikia bilioni 345 kwa sasa, kuongezeka kwa wakopaji kutoka wanafunzi 16,000 mwaka 2005 hadi kufikia 95,000 kwa sasa.
 

Rais Kikwete amesema kuwa kwa sasa Serikali yake inapambana na changamoto zilizojitokeza kutokana na kupanuka sana kwa elimu nchini na kuwa moja ya changamoto hizo ni ukosefu wa walimu wa masomo ya sayansi ambapo sasa imefikia kikomo kwa sababu, sasa wapo karibu wa kutosha wa masomo hayo kwa shule za sekondari zote nchini.

Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
25 Agosti , 2014


 
 


Written by

0 comments: