Balozi Ombeni Awafunda Watumishi wa Umma Tanga , Asema Majukumu Yatekelezwe Kwa Uweledi


Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Y. Sefue amewataka watumishi wa Umma kufanya kazi  kwa kufuata kanuni na taratibu za utumishi wa umma ili kuzalisha huduma zenye tija kwa wananchi. Hayo ameyasema leo wakati akizungumza katika mkutano na watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa, Mashirika ya Umma, taasisi na wakala wa Serikali katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga.

Balozi Ombeni yuko katika ziara ya kikazi ya siku moja katika  Mkoa wa  Tanga yenye dhumuni la kusikiliza na kujionea hali ya utekelezaji wa majukumu ya Watumishi wa Umma ikiwa ni pamoja na kutolea ufafanuzi na miongozo ya masuala mbalimbali ya kiutumishi.  Ziara hii ni mwendelezo wa ziara za kikazi ambazo  Katibu Mkuu Kiongozi amekuwa akizifanya katika Wizara, Taasisi za Umma, Wakala za Serikali na Sekretarieti za Mikoa.

Akizungumza wakati wa hotuba yake, Balozi Ombeni amesisitiza kuwa ni wajibu wa kila mtumishi wa umma kuwa mwadilifu, mnyenyekevu na anayesikiliza kero za wananchi na si kuwanyongonyesha wananchi kwa lugha ambazo hazistahili.

“ Sisi ni watumishi wa Umma na tunaongozwa na kanuni na taratibu za utumishi, ni vyema kuzifahamu na kuzizingatia” amesisitiza Balozi Ombeni.

Akitoa taarifa ya utendaji wa watumishi wa Sekretarieti na Halmashauri za Mkoa wa Tanga kwa Katibu Mkuu Kiongozi muda mchache kabla ya hotuba ya Katibu Mkuu Kiongozi, Katibu Tawala Mkoa wa Tanga Bw. Salum Mohamed Chima ( Alhaji) amesema kuwa  hali ya usalama katika Mkoa ni tulivu na hakuna matukio yenye kuhatarisha uvunjifu wa amani.

Aidha Bw. Chima amemhakikishia Katibu Mkuu kiongozi kwamba Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa na Halmashauri zake hupata mishahara yao kwa kila mwezi  na kwamba taarifa za masuala ya ajira, kupandishwa vyeo na uthibitishwaji wa watumishi kazini  kufanyika kwa muda mfupi. Hii ni  kutokana na Sekretarieti ya Mkoa na Halmashauri kuunganishwa kwenye mfumo wa taaarifa za kiutumishi na mishahara.

Bw. Chima amebainisha baadhi ya changamoto zinazoikumba Sekretarieti ya Mkoa na Halmashauri zake kuwa ni Kupungua kwa raslimali fedha, athari za virusi vya  Ukimwi kupunguza nguvu kazi, Uhaba wa nyumba za watumishi ambapo amemwomba Katibu Mkuu Kiongozi kuona namna ya kuzitafutia majawabu ili utumishi wa umma uendelee kuwa chachu ya kuleta maendeleo.

Mara baada ya kuwasili Katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Katibu Mkuu Kiongozi na ujumbe wake wamepokelewa na Katibu Tawala wa Mkoa Bw. Salum Mohamed Chima, Mkuu wa Wilaya ya Tanga ,Viongozi Waandamizi wa Sekretarieti ya Mkoa, Wakuu wa Taasisi za Umma na Watendaji Wakuu wa Wakala za Serikali zilizopo Mkoani Tanga.

 Kabla ya kufanya mazungumzo na watumishi wa Umma, Katibu Mkuu Kiongozi amefanya mazungumzo na Viongozi wa Mkoa ambapo amewakumbusha umuhimu wa kuzingatia Sera, Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali ya Utumishi wa Umma katika kutoa huduma kwa Wananchi.
 
Katibu Tawala Mkoa wa Tanga Bw. Salum Mohamed Chima akiwasilisha taarifa  ya utendaji wa watumishi sekretarieti na Halmashauri za Mkoa wakati Katibu Mkuu kiongozi akizungumza na Viongozi wa Secretarieti ya Mkoa wa Tangakatika ukumbi mdogo wa mikutano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Sehemu ya wajumbe wa Mkutano katika ukumbi wa mikutano
 
 Barozi Ombeni na ujumbe wake pamoja na Wakuu wa Idara& Vitengo na Maafisa kutoka Secretarieti ya Mkoa wa Tanga
Barozi Ombeni na ujumbe wake pamoja na Makatibu Tawala Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za Tanga

 Barozi Ombeni na ujumbe wake pamoja na Makatibu Afya Halmashauri za Tanga
Barozi Ombeni na ujumbe wake pamoja na  Makatibu Elimu Mkoa na Halmashauri za Tanga

 Barozi Ombeni na ujumbe wake pamoja na Viongozi kutoka mashirika ya Serikali
Barozi Ombeni na ujumbe wake pamoja na Viongozi kutoka Wakala wa Serikali .Picha na Mwanahabari wa Ikulu
 


Written by

0 comments: