Waziri Mkuu Atoa Suluhu Kiwanda Cha Chai Mponde



WazirI Mkuu Mizengo Pinda amewataka Wakala wa  Wakulima Wadogo wa Chai pamoja na Bodi ya Chai nchini  waangalie uwezekano wa kuunda timu ya watu wawili au watatu  itakayosimamia mwenendo wa kiwanda cha chai Mponde,  kilichopo wilayani Lushoto mkoani Tanga. 
 Waziri Mkuu ambaye aliwasili jijini Tanga jana  asubuhi (Jumamosi, Septemba 13, 2014) akitokea Dodoma,  alipokea taarifa fupi ya mgogoro wa kiwanda hicho kabla ya  kuzungumza na wakulima, wadau wa zao la chai na viongozi wa  mkoa na wizara kadhaa kwenye mkutano uliofanyika kwenye  ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga. 
 “Wakala wa Wakulima pamoja na Bodi ya Chai  itabidi watusaidie kuunda timu kwa sababu tunahitaji kuwa na  jicho la Serikali ndani ya kiwanda... tunahitaji watu wenye  uzoefu mkubwa na mambo ya chai ili wasimamie uendeshaji wa  kiwanda pindi kitakapoanza kazi,” alisema. 
 “Vilevile mwekezaji itabidi akubali kufanya  kazi na timu ya Serikali ili tuweze kujua kwa leo kiwanda  kiko katika hali gani na tukitaka kukifungua ni lazima  tufanye nini,”  aliongeza. 
 Waziri Mkuu alisema timu hiyo kwa kushirikiana  na mwekezaji hawana budi kuandaa mpango-kazi wa miaka miwili  hadi mitatu wa kufufua kiwanda ili uzalishaji wa chai ufikie  pazuri. “Kiwanda wakati kinabinafsishwa kilikuwa na uwezo  wa kusindika kilo 20,000 za majani ya chai lakini  kilikarabatiwa na kufikisha uwezo wa kusindika kilo 120,000  kwa siku. Sasa tuangalie uwezekano wa kuongeza uzalishaji  kwani hapo tutaweza pia kuongeza mavuno kwa wakulima  wetu,” alisema. 
 Alisema ili kuweza kusonga mbele, itabidi  Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) aende  kufanya ukaguzi kwenye kiwanda hicho ili kuweza kutoa picha  halisi ya kiwanda hicho kwa sababu Serikali ina hisa.  
 Kiwanda cha Chai cha Mponde kinamilikiwa na  Chama cha Wakulima wa Chai cha UTEGA (Usambara Tea Growers  Association) ambacho kilitafuta mwekezaji ambayo ni Kampuni  ya Chai ya Lushoto (Lushoto Tea Company). Wakulima wa Chai  walikifungia kiwanda hicho kisifanye kazi kwa madai kuwa  walikuwa hawalipwi walipo kwa wakati, wamiliki kutumia lugha  chafu.
 Baada ya kusikiliza pande zote, Waziri Mkuu  alikubaliana na rai iliyotolewa na pande hizo kwamba kuna  haja ya kufungua kiwanda hicho ambacho kilifungwa tangu Mei  26, 2013 ili kuwasadia wakulima wapate soko la chai lakini  pia waweze kujikimu mahitaji yao.
 Mapema, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Bibi  Chiku Gallawa alisema mkoa wa Tanga ulijipanga kukuza  kiwango cha ukusanyaji mapato ili kuendana na mpango wa  Serikali wa matokeo makubwa sasa lakini kufungwa kwa kiwanda  hicho, kumeshusha pato la mtu mmoja mmoja, pato la mkoa na  pato la Taifa kwa ujumla. 
 “Changamoto kubwa ambayo tumekabiliana nayo  kwa kipindi chote hiki ambacho kiwanda kilikuwa kimefungwa, ni kwa wananchi kushindwa kuuza chai yao,” aliongeza.  
 Naye, Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Bw.  Majjid Mwanga akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu alisema  kiwanda cha Mponde kilikuwa na uwezo wa kusindika kilo  70,000 za majani mabichi ya chai kwa siku lakini hadi  kinafungwa uwezo huo ulishuka na kufikia kilo 25,000 kwa  siku. 
 Alisema idadi ya wakulima walioathirika  kutokana na kufungwa kwa kiwanda hicho ni 3,908 ambao  walikuwa wakilima hekta 1,951. “Bei ya kilo moja ya chai  ilikuwa ni sh. 225/- wakati wastani wa pato la mkulima kwa  nusu hekta ilikuwa ni sh. 180,000/- kwa mwezi lakini kwa  sasa limeshuka na kufikia sh. 90,000/- kwa mwezi kwa nusu  hekta hiyo hiyo,” alisema. 
 Alisema zaidi ya tani 1,800 zimeshindikana  kusindikwa na hivyo kuikosesha Halmashauri yao kiasi cha sh.  milioni 21.6/- ambazo zilikuwa zikilipwa kama ushuru kwa  kila kilo moja iliyokuwa ikiuzwa. “Wakulima kwa ujumla wao  wamepata hasara ya sh. milioni 370.8/-” alisema. 
 Mkutano huo pia ulihudhuriwa pia na Mawaziri wa  OWM-TAMISEMI; Kilimo, Chakula na Ushirika; Viwanda na  Biashara, Wabunge wa Mlalo, Bumbuli na Lushoto; viongozi wa  Mkoa na Halmashauri za Korogwe, Lushoto na Bumbuli, viongozi  wa UTEGA na mwekezaji, ambaye ni mmiliki wa kiwanda cha  Lushoto Tea Company. 

 Stori na Irene Bwire , Ofisi ya Waziri Mkuu.

 


Written by

0 comments: