Mashindano Ya SHIMUTA 2014 Yafunguliwa Rasmi Jijini Tanga
Mkuu wa Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga
Mhe.Subira Mgalu amezionya timu ambazo zinashiriki kwenye michuano ya
Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma na Kampuni Binafsi Nchini (SHIMUTA)
kuacha kuchukua wachezaji ambao sio wafanyakazi kwani kufanya hivyo kunapunguza
ladha ya mashindano hayo.
Mgalu aliyasema hayo mwishoni mwa
wiki wakati akizundua mashindano ya Shimuta yanayofanyika kwenye viwanja vya
Mkwakwani vilivyopo katika Jiji la Tanga na kushirikisha wanamichezo wapatao 500 kutoka mashirika
na makampuni mbalimbali hapa nchini.
Alisema kuwa michezo hujenga undugu
na furaha baina ya wanamichezo hivyo kuwaingiza wachezaji ambao sio wafanyakazi
kwenye mashindano hayo wataondoa maana halisi ya mashindano hayo jambo ambalo
linaweza kuwafanya kushindwa kufikia malengo yao waliojiwekea.
“Mashindano haya ni ya wanamichezo
wafanyakazi…kuna wale wanamichezo ambao sio wafanyakazi ambao wanajulikana kama
mamluki au wavamizi kwamba hapa sio mahala pao nawasihi tuchezeshe wafanyakazi
halisi ili mshindi apatikane kihalali na sio vyenginevyo….. kwa sababu ni
hatari sana kumleta mwanamichezo ambaye sio mfanyakazi kwenye michezo hii
anaweza kuvunjika mguu au akifa kwa mfano hatuombei itokee hiyo itakuwaje
“Alisema DC Mgalu.
Aidha alizitaka timu hizo kuacha
kuwatumia wachezaji wa aina hiyo kwani wana madhara makubwa hasa pale
yanapokuwa yakijitokeza kwa kuzitaka timu zenye utamaduni huo kuhakikisha
wanaondokana nao.
Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya
alionekana kukerekwa na baadhi ya menejimenti za Taasisi,Mashirika na makampuni
mbalimbali kuwa na utashi wa kutokupenda michezo na wengine kwa kisingizio cha
ukosefu wa fedha kuacha kufanya hivyo badala yake wamuunge mkono Rais Jakaya
Kikwete katika jitihada zake za kuinua na kuendeleza michezo hapa nchini.
Akizungumzia waamuzi wanaochezesha
mashindano hayo, Mgalu aliwataka kuchezesha kwa haki bila upendeleo kwa kufuata
sheria za mchezo husika ili mshindi aweze kupatikana kihalali kwa sababu
wakienda kunyume chake wanaweza kusababisha tafrani na manung’uniko kwa baadhi
ya timu shiriki.
Hali kadhalika aliwataka kuhakikisha
wanakuwa na nidhamu ya hali ya juu wakati wote wa mashindano ikiwemo
kukubaliana na matokeo pindi watakapojikuta wamefungwa wakati wa mashindano
hayo.
Awali akizungumza kabla ya
kumkaribisha Mkuu huyo wa Wilaya, Mwenyekiti wa Shimuta, Khamis Mkanachi alisema
kuwa mashindano hayo msimu huu yanashirikisha timu 20 pungufu ya 22
zilizoshiriki mwaka jana mkoani Dodoma ingawa walijiwekea lengo la kuwa na timu
25 hadi 30 mwaka huu .
Alisema kuwa kupungua kwa idadi ya
timu shiriki kunatokana na baadhi ya mashirika kubinafsishwa hali ambayo
imepelekea timu nyingi kushindwa kupata nafasi ya kupeleka washiriki wake
lakini pamoja na kuwepo hali hiyo shirikisho hilo limendelea na jitihada za
ziada kuhakikisha idadi ya timu hizo haipungui bali kuongezeka.
Aidha alizitaja timu hizo kuwa ni Shirika la
Utangazaji Tanzania (TBC),Chuo Kikuu Huria(OUT),Chuo cha Elimu ya
Biashara(CBE),Kampasi za Mbeya na Dar es Salaam na Mwanza,Shirika la Umeme
Tanzania(TANESCO),Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), ChuoKikuuchaArdhi.
Timu nyengine ambazo zinashiriki mashindano hayo ni Hifadhi ya Taifa Tanzania(TANAPA), Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini(IRDP),Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma(CDA),Chuo Kikuu cha Mzumbe,Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi(MOCU),Chuo kkikuu cha Muhimbili cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS),Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM).
Wengine ambao watashiriki kwenye mashindano hayo ni Baraza la Hifadhi na Usimamizi na Mazingira (NEMC),Shirika la Mzinga,Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Arusha (AICC), Wenyeji wa Mashindano hayo,TANGA CEMENT na Timu mpya kwenye shirikisho hilo ya Bohari ya Madawa(Medical Stores Department(MSD).
Mhe. Subira Mgalu akifungua rasmi mashindano hayo
Wakati Mhe. Mgalu akisalimiana na wachezaji wa timu shiriki
Mashindano yalifunguliwa kwa muziki wa kizazi kipya ujulikanao kama "Kwaito"
0 comments: