World Vision Waacha Wosia Ulinzi Kwa Watoto.


 
Shirika lisilo la Kiserikali la World vision Tanzania cluster ya Korogwe limeiomba jamii kuendeleza juhudi za shirika hilo walizozifanya kwa miaka kumi na tano katika tarafa ya Magoma wilayani Korogwe za kumlinda mtoto kwa kuhakikisha anapata huduma na haki zake zote za msingi.
Ombi hilo limetolewa jana na  mratibu wa mradi uliokuwa ukishughulikia maendeleo ya Magoma( Magoma ADP)  George Banyenza katika hafla ya kutia saini hati za makabidhiano iliyohudhuriwa na Watendaji wa World vision, watendaji wa halmashauri ya wilaya Korogwe,Diwani wa kata ya Magoma,Maafisa tarafa na Mtendaji wa kata hiyo, wenyeviti wa vijiji vya kata hiyo na wanufaika wa mradi huo iliyolenga  kukabidhi  rasmi majengo ya ofisi yaliyokuwa yakitumiwa na mradi huo kwa Serikali .
Banyenza alieleza kuwa kwa muda wa miaka kumi na tano World Vision kwa ufadhili wa watu wa ujerumani imekuwa ikiisaidia jamii ya tarafa ya Magoma kupitia watoto kupata huduma za elimu,afya na maji sambamba na kupinga ukatili dhidi ya watoto na kuhakikisha wanapata huduma zote za msingi.
“ADP Magoma imefikia tamati sasa lakini kwa kipindi chote tumekuwa tukiisaidia jamii  kupitia watoto hivyo tunaomba jengo na rasilimali zake tunazoacha ziwe chachu kwa jamii  kuendeleza ulinzi na usalama wa mtoto wa Magoma.” Alieleza Banyenza.
Katika hatua nyingine Meneja miradi Mwandamizi wa World vision  kanda ndogo ya Korogwe Sylvester Masanja, alimuomba Mkurugenzi Mtendaji kuwa mlezi wa asasi ya jamii ya UKIMAMA iliyokuwa ikilelewa na mradi huo sambamba na kuwapatia chumba kimoja katika jengo hilo kwa ajili ya shughuli za asasi hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Korogwe Lucas Mweri aliyepokea hati za makabidhiano ya jengo na rasilimali zake aliahidi kutunza rasilimali hizo na kuhakikisha zinatumika kwa matumizi yenye tija kwa jamii.
 Magoma ADP imeikabidhi Serikali jengo lenye thamani ya Tsh 68,480,000/- walilolijenga mwaka 2010 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kusaidia watoto na jamii tarafa ya Magoma ambayo imefikia mwisho wa utekelezwaji wake. Stori & picha na Fatna Mfalingundi-Afisa habari Halmashauri ya Wilaya Korogwe


Written by

0 comments: