Blog ya Mkoa wa Tanga, itakupatia habari mbalimbali, kuhusu Mkoa wetu
Makao Makuu ya Mkoa wa Tanga

Tangazo Ukosefu Wa Muda Wa Maji Jijini Tanga


TANGAZO
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Tanga (TANGA UWASA) inawatangazia wakazi wa jiji la Tanga kuwa kutakuwa na ukosefu wa maji siku ya Alhamisi ya Tarehe 16/4/2015. Hii inatokana na TANESCO kufanya ukarabati wa nguzo katika maeneo ya mitambo ya maji Pande.

Wananchi mnashauriwa kuhifadhi maji ya kutosha. Huduma inatarajiwa kurejea kama kawaida siku ya Ijumaa tarehe 17/4/2015.

Mamlaka inaomba radhi kwa usumbufu utakaojitokeza.


Imetolewa na ofisi ya uhusiano
Tanga uwasa
14/04/2015


Read more

Mkuu Wa Mkoa Wa Tanga Azindua Mpango Mkakati Wa Miaka Mitano Wa Ukimwi Katika Mkoa Wa Tanga Wakati Wa Kikao Cha RCC


Mhe. Magalula Said Magalula , Mkuu wa Mkoa wa Tanga akikata utepe uliofungwa kwenye kitabu kuashiria  uzinduzi wa Mpango wa Miaka mitano wa Ukimwi katika Mkoa wa Tanga wakati wa kikao cha Ushauri cha Mkoa wa Tanga (RCC) kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga mwishoni mwa wiki.

Mada mbalimbali ziliwasilishwa na kujadiliwa katika kikao hicho zikiwemo mada juu ya Taarifa ya upatikananji maji katika Mkoa wa Tanga, taarifa ya Bima ya Afya, taarifa ya hali ya bandari ya Tanga, taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya 2014/2015 na mapenekezo ya bajeti ya mwaka 2015/2016.

Wajumbe walipata nafasi ya kujadiliana jinsi ya kuboresha huduma na vilevile mikakati juu ya kukabiliana na baadhi ya changamoto. Naye Mkuu wa mkoa ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kikao alitoa maelekezo juu ya nini kifanyike ili huduma za wananchi ziweze kuboreshwa. 

    Baadhi ya Wajumbe na waalikwa wakisikiliza mijadala mbalimbali



      Baadhi ya waandishi wa habari wakisikiliza kwa makini



Read more

Jikumbushe Wiki Ya Utepe Mweupe Iliyofanyika Kitaifa Mkoani Tanga

Mkoa wa Tanga umekuwa mwenyeji wa maadhimisho ya Kitaifa ya Utepe Mweupe wa Uzazi salama  yaliyofanyika Machi 15 mwaka huu. Wiki ya Utepe mweupe ilianza tarehe 10 ambapo iliambatana na shughuli mbalimbali zilizolenga kuhakikisha vifo vya mama na mtoto vinavyozuilika vinatokomezwa.

Katika Kupata sauti za Wananchi, Wakazi wa Wilaya tano za Mkoa wa Tanga ambazo ni Kilindi, Handeni, Korogwe, Muheza na Jiji la Tanga walipata fursa ya kutoa maoni yao wakiwawakilisha Watanzania  jinsi gani huduma za afya ziboreshwe  kwa lengo la kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Uhamasishaji wa wananchi ulifanyika kupitia vyombo mbalimbali ya habari. Pichani Bi. Agness Mbwana ambaye ni Mratibu wa Utepe Mweupe Mkoa wa Tanga akizungumza  na wananchi juu ya ushiriki wao katika maadhimisho hayo kupitia radio ya Breeze Fm iliyoko Tanga 
Dr Herriet Mwakilishi kutokaChama cha madaktari Wanawake Tanzania  ( MEWATA )  akifafanua kuhusu dalili za awali za ugonjwa wa saratani ya matiti  na huduma za upimaji wakati wa wiki ya  maadhimisho ya Utepe Mweupe Mkoani kupitia radio ya Breeze Fm
 Vikao vya maandalizi ya Utepe Mweupe viliendelea katika ukumbi mdogo wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga ili kufanikisha zoezi  la maadhimisho kitaifa. Wa pili kulia ni Mganga Mkuu wa mkoa wa Tanga Dr Asha Mahita akifafanua jambo wakati wa kikao
Baadhi ya wajumbe wa vikao vya maandalizi
 Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Magalula Said Magalula akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini  kwake siku mbili kabla ya Kilele cha Maadhimsho  ili kuutaarifu umma kuwa Mkoa ulijiandaa vyema na maandalizi yalikamilika tayari kwa maadhimisho ya siku ya Utepe Mweupe kitaifa Mkoani Tanga
Baadhi ya waandishi wakati wa mkutano
Zoezi la Upimaji wa dalili za awali ya saratani ya matiti liliiendelea . Pichani akinamama wakisubiri kumwona mtalaamu


Read more

Bodi Ya Barabara Mkoa wa Tanga Yaonya Uharibifu Wa Barabara


Wajumbe wa Bodi ya Barabara Mkoa wa Tanga  wamesikitiswa na baadhi ya tabia za Wakazi wa Tanga ambao kwa makusudi kabisa wamekuwa wakifanya uharibifu katika barabara hasa zile zenye lami. Hayo yamebainika katika kikao cha pili  cha bodi ya barabara kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mku wa Tanga siku ya alhamisi ya Machi 2015 kuanzia saa tatu asubuhi.

Akifungua kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Tanga, magalula Said Magalula amesema lengo la kikao cha bodi ya barabaraa ni wadau kupata habari sahihi ya uboreshaji wa barabara katika kupunguza umaskini na kuleta maendeleo kwa wananchi.

“ Tukiweka maazimio mazuri yanayotekelezeka  barabara zetu zinaweza kuwa katika mazingira mazuri na kuhudumia ipasavyo “alisisitiza Magalula

Pia Mhe. Magalula alielekeza Wakurugenzi wa Halmashauri za tanga kuhakikisha wanatoa  elimu kwa wananchi juu ya kutumia vivuko vilivyowekwa barabarani rasmi kwa ajili ya kuvusha mifugo.


Kikao kiliazimia  kuhakikisha uboreshaji katika kudhibiti uzito na mifugo kutembea barabarani.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga , Mhe Magalula Said Magalula akifungua rasmi kikao cha Bodi ya barabara
Meneja wa TANROADS Mhandisi Alfred Ndumbaro Akitoa taarifa ya hali ya barabara katika Mkoa wa Tanga
 Mbunge wa jimbo la  Tanga Mhe Omari Nundu akichangia mada wakati wa Kikao
Baadhi ya wajumbe wa bodi ya Barabara na waalikwa




Read more

Mahakama Tanga Yazindua Bodi Mpya Ya Parole


 Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Magalula Said Magalula amewataka wajumbe wa Bodi ya Paroli Mkoa  kutenda kazi kwa kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa ili kutenda haki na kuepuka ushawishi wa namna yeyote katika kupokea na kuomba rushwa.

Hayo yamesemwa mapema siku ya alhamisi ya machi 12 mwaka huu wakati wa uzindua rasmi Bodi ya Parole Mkoa tukio lililofanyika katika ofisi za Magereza Mkoa.

 Lengo la Bodi hii ni  kuwajadili  wafungwa wenye sifa  za kuweza kuachiliwa huru baada ya kutimiza vigezo ambavyo vimeainishwa kwenye  sheria namba 25  ya Paroli ya mwaka 1994 na kufanyiwa mabadiliko mwaka 2002.

Sheria husika imeweza kuanisha ni aina gani ya makosa ambayo mfungwa anaweza kupata fursa ya kuingia kwenye mpango wa Paroli . Pamoja na makosa hayo mfungwa hawezi kuingizwa kwenye utaratibu wa Paroli endapo amepatikana na kosa la unyanyanyi wa siraha, madawa ya kulevya, kulawiti, kubaka na mauaji ya kukusudia.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa sheria ya parole tangu utekelezaji wake mwaka 2003, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tanga Kamishina Agustino Mboje amesema tayari wafungwa 331 wameshaachiliwa huru kwa utaratibu wa parole, wafungwa 305 wamemaliza vifungo vyao salama na wafungwa 26 bado wanaendelea na vifungo vyao kwa utaratibu huu.

Licha ya kuwepo na mpango huu wa kupunguza msongamano wa wafungwa gerezani lakini bado wafungwa wengi wameshindwa kunufaika na utaratibu wa Paroli kutokana na kutotimiza masharti ya parole.

Sababu kubwa ni ukosefu wa nakala za hukumu kwa wakati na ukosefu wa elimu ya kutosha  kwa wanajamii kuhusu sheria hii na hivyo kupelekea maafisa wa Paroli  kuwa na ugumu wa kupata taarifa muhimu zinazowahusu wafungwa wananotarajiwa kunufaika na mpango huu.

 Maafisa wa Magereza wakimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Magalula Said Magalula
Mkuu wa Mkoa wa Tanga akisaini kitabu cha wageni
Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tanga Kam. Augostino Mboje akitoa taarifa ya utekelezaji wa sheria ya Parole katika Mkoa wa Tanga
Baadhi ya wajumbe na Maafisa wa magereza wakati wa uzinduzi



Read more

Mkoa Wa Tanga Kuwa Mwenyeji Wa Maadhimisho Ya Siku Ya Utepe Mweupe Kitaifa Machi 15

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Magalula S. Magalula akizungumza  na Waandishi wa Habari  Leo Ofisini kwake 
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Tanga Bw. Ramadhani Kaswa  (Kushoto ) na baadhi ya Waandishi wakati wa mkutano
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakati wa mkutano

Taarifa zaidi

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga kwa niaba ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Muungano wa Utepe Mweupe wa Uzazi Salama Tanzania inapenda kuwatangazia Wananchi  kuwa Mkoa wa Tanga unatarajia kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya Siku ya Utepe Mweupe Kitaifa itakayofanyika Machi 15, Mwaka huu.

Siku ya Utepe Mweupe ni mwendelezo wa juhudi za Serikali katika kupunguza  na kutokomeza kabisa vifo vya akina mama na watoto wachanga.Maadhimisho haya ambayo hufanyika  Machi 15 kila mwaka yana lengo la kuwakumbuka na kuwaenzi wanawake waliopoteza maisha kutokana na matatizo ya uzazi.

Siku hii pia hutumika kujadili mikakati ya kuzuia vifo vingine visitokee. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “WAJIBIKA MAMA NA MTOTO MCHANGA AISHI”.  Kauli mbiu hii inalenga kuhamasisha uwajibikaji wa kila mmoja wetu kuanzia mama mjamzito nwenyewe na familia yake,  jamii na uongozi katika kuhakikisha kuwa hakuna mama wala mtoto mchanga anayepoteza maisha kutokana na sababau ambazo zingeweza kuzuilika.

Aidha, kutakuwepo na shughuli mbalimbali ambazo zitaambatana na maadhimisho haya katika wiki ya kuelekea siku yenyewe ambazo ni pamoja na uchangiaji damu salama, kushiriki katika zoezi la sauti ya jamii,kushiriki katika matembezi ya mshikamano na mkutano siku ya kilele.

 Asilimia 75 ya vifo vingi nchini vinatokana na kutoka damu kwa wingi, maambukizi, shinikizo la damu na utoaji mimba. Wanawake 24 wanafariki kila siku na wengine hupata ulemavu wa kudumu.

Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kuweka mikakati madhubuti ili kupunguza vifo vya mama na mtoto. Kwanza imeelekeza nguvu zake katika kutoa elimu ya uzazi salama na pia imeelekeza Halmashauri zote Mkoani kuwa na kipengele mahususi cha bajeti kinacholenga kuhakikisha kuwa huduma za dharura za uzazi zinapatikana karibu na akina mama na watoto.

Kutokana na juhudi za serikali na wadau mbalimbali, matunda yameshaanza kuonekana miongoni mwetu. Kwa mfano katika Mkoa wa Tanga vifo vya mama na mtoto vimepungua kutoka idadi ya akina mama 101 kati ya wakina mama 45,256 waliojifungua kwa mwaka 2013 hadi kufikia idadi ya akinamama 69 kati ya wakina mama 47,692 waliojifungua kwa mwaka 2014 na idadi ya watoto 429 kati ya watoto 44,852 waliozaliwa  kwa mwaka 2013.   Serikali inaendelea na mapambano kuhakikisha afya ya mama na mtoto iko salama.

Kupunguza vifo vya mama na mtoto vinavyotokana na matatizo wakati wa kujifungua ni  moja ya malengo 8 ya Milenia. Hili ni lengo namba tano ambalo linalenga kupunguza vifo vya akina mama vinavyoyokana na matatizo wakati wa kujifungua kwa asilimia sabini na tano (75%) ifikapo mwaka 2015.

Nawashukuru na kuwapongeza wenzetu wa Utepe Mweupe na wadau wengine kwa kujikita katika kampeni ya uhamasishaji ili kupunguza na kutokomeza vifo vya mama na mtoto.

Napenda kutoa wito kwa wananchi kuhakikisha kuwa kila mmoja anatekeleza wajibu wake ili kuokoa maisha ya mama na mtoto. Pia naviomba vyombo vya habari kuungana na makundi mengine katika jamii kuwa sauti ya akina mama ili kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Kwa pamoja tunaweza kuzuia vifo vya mama na watoto wachanga

“Wajibika Mama na Mtoto Mchanga Waishi”





Read more

Wakuu Wapya Wa Wilaya Mkoani Tanga Waapishwa Leo

Mhe. Magalula Said Magalula akimwapisha Mhe. Husna Rajab Msangi kuwa  Mkuu wa Wilaya ya Handeni .


Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Magalula Said Magalula amewaapishwa leo Wakuu Wapya wa Wilaya ambao ni Mhe. Husna Rajab Msangi, Mkuu wa Wilaya ya Handeni na Mhe. Mariam M. Juma , Mkuu wa Wilaya ya Lushoto wakati wa hafla fupi iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga .

Mhe. Magalula ameonya tabia ya umangimeza na kuwaasa Wakuu hao wapya kuwa njia pekee ya kumwahakikishia Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete ,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa hajakosea kuwateua ni kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii.

Aidha kwa upande wao, Wakuu hao wameomba ushirikiano kutoka kwa viongozi wa Wilaya wanakotoka na Mkoa ili waweze kutekeleza majukumu yao vizuri.

               Mhe Magalula Said Magalula akimwapisha Mhe. Mariam M. Juma kuwa  Mkuu wa Wilaya ya Lushoto .
Baadhi  ya waalikwa wakati wa kiapo

Picha ya pamoja ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Katibu Tawala wa Mkoa Bw. Mohamed Chima ( wa kwanza kushoto kwa waliokaa), wakuu wa Wilaya Wapya , Viongozi Maalumu na  Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Wilaya




Read more

Utepe Mweupe Wakutana Na Waandishi Wa Habari Mkoani Tanga

Bi Rose Mlay, Mratibu wa Muungano wa Utepe Mweupe akitoa mada . Kulia ni Bw. Kenneth Simbaya , Mmoja wa wakufunzi kwenye warsha.


“Mama akiwa salama Taifa liko salama, Mama anapokufa na Taifa linakufa” Hayo ni baadhi ya maneno ambayo waliaswa waandishi wa habari kwenye warsha ya Waandishi wa habari iliyoandaliwa na Muungano wa Utepe Mweupe iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa  Kituo cha Walemavu ( YDCP)

Waandishi  wa Habari kutoka vyombo vya Habari Mkoani Tanga walipata wasaa wa  kuongeza uelewa wa masuala ya Vifo vya Mama na Mtoto. Akizungumza kwa hisia kali, Bi Rose Mlay  ambaye ni Mratibu wa Muungano wa Utepe Mweupe aliwaomba waandishi wa habari kuungana na makundi mengine katika jamii kupaza sauti  kwa niaba ya akina mama ili kupunguza vifo vya mama na mtoto.

“Sababu za vifo vya mama na mtoto hazichagui zinaweza kutokea kwa mama yeyote awe tajiri ama maskini. Mama anahitaji kituo cha afya kilichokaribu na chenye huduma nzuri , vifaa na wataalamu. Jamani Tuwajibike ili mama aishi”

Naye Bw. Kenneth Simbaya , mmoja wa wakufunzi kwenye warsha hiyo alitoa wito kwa waandishi  wa habari kuona umuhimu wa kuandika makala na habari za vifo vya akina mama na watoto ili jamii husika na serikali ilichukulie suala hilo kwa uzito mkubwa.

Warsha ya waandishi wa habari iliyoamdaliwa na Muungano wa Utepe Mweupe ni maandalizi ya maadhimisho ya siku ya Utepe Mweupe yenye kauli mbiu “Wajibika  Mama Aishi”yatakayofanyika kitaifa Machi 15 katika Mkoa wa Tanga.

 Bw. Hassan Hashim, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Tanga  ambaye pia ni Mwakilishi wa Channel Ten akichangia mada wakati wa Warsha
Bw.  John Semkande, mwakilishi kutoka Pangani Fm akitoa ushuhuda ni kwa jinsi gani amekuwa akitimiza wajibu wake ili kuhakikisha anaokoa maisha ya mama na mtoto 



Read more

Mabadiliko Ya Wakuu Wa Wilaya Katika Mkoa Wa Tanga


Kitaifa ,   Rais  Jakaya Mrisho Kikwete ameteua  Wakuu wa Wilaya wapya 12, waliobadilishwa vituo vya kazi 64 na waliobaki kwenye vituo vya zamani 42. Katika Mkoa wa Tanga yafuatayo ni mabadiliko ya Wakuu wa Wilaya.

Wakuu wa Wilaya Wapya.
1      Wilaya ya Tanga
Mhe. Abdula Suleiman Lutavi anayetokea Wilaya Namtumbo

2    Wilaya ya Muheza
 Mhe. Esterina Julio Kilas akitokea  Wilaya ya Wanging’ombe

3    Wilaya ya Pangani
Mhe. Regina Regnald Chonjo akitokea Wilaya ya  Nachingwea

4   Wilaya ya Lushoto
     Mhe. Mariam M. Juma ambaye ni uteuzi mpya 

5    Wilaya ya Handeni
Mhe. Husna Rajab Msangi ambaye ni uteuzi mpya

Wakuu wa Wilaya waliohamishwa vituo vya kazi ndani ya Mkoa
1   Mhe.Hafsa Mahinya Mtasiwa ambaye amehamishiwa Wilaya ya Korogwe akitokea Wilaya ya Pangani.

Wakuu wa Wilaya waliobaki kwenye vituo vyao vya zamani ndani ya Mkoa
1     Mhe.Mboni Mwanahamis Mgaza, Mkuu wa Wilaya ya Mkinga
2     Mhe. Suleman Salum Liwowa, Mkuu wa Wilaya ya Kilindi

Wakuu wa Wilaya ambao uteuzi wao umetenguliwa na kupangiwa kazi nyingine
1.      Mhe. Mrisho Gambo, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe

Waliokuwa Wakuu wa Wilaya za Tanga na kuhamishiwa Wilaya zingine Nchini
1. Mhe. Subira Hamis Mgalu aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Muheza amehamishiwa Wilaya ya             Kisarawe
2. Mhe. Magid Hemed Mwanga alieykuwa Mkuu wa Wilaya ya Lushoto amehamishiwa Wilaya ya         Bagamoyo
3. Mhe.  Muhingo Rweyemamu aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni amehamishiwa Wilaya ya         Makete


Read more

Taswira Ya Maadhimisho Ya Miaka 38 Ya CCM Yaliyofanyika KiMkoa Wilayani Muheza

    Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Magalula S. Magalula akielezea utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Mkoa wa Tanga wakati wa Maadhimisho ya 38 ya CCM yaliyofanyika Kimkoa katika Wilaya ya Handeni. Miongoni mwa mafanikio ni  Uongezekaji wa Shule za Msingi na za Sekondari, ujenzi wa Maabara na Zahanati kwa kila kijiji, Umeme wa REA Vijijini, Barabara za Lami na pia amekipongeza chama cha mapinduzi kwa  ushindi wa Kishindo wakati wa chaguzi za serikali za Mitaa.


   Jumla ya wananchama wapya 200 wamejiunga na Chama cha Mapinduzi kutoka vyama pinzani. Pichani mmoja wa wanachama wapya akipokea kadi yake ya CCM kutoka kwa Katibu wa CCM Mkoa Bw. Shija Othuman
Baadhi ya Washiriki kwenye Maadhimisho



Read more

Waganga Wakuu Wa Hospitali Za Wilaya Wakumbushwa Kuendelea Kutoa Elimu Ya Mfuko Wa Bima Ya Afya



Wakurugenzi  na Waganga wakuu wa hospitali za Wilaya Mkoani Tanga,  wametakiwa kupita kila  kijiji na kitongoji kutoa elimu ya  kujiunga  na mfuko wa bima ya afya ili kuiwezesha Serikali kufikia  malengo iliyojiwekea.

 Akifungua kikao cha  kujadili mpango  wa mfuko wa Afya ya jamii na kusaini mkataba wa uhamasishaji  wa CHF kwa Wilaya  ya Lushoto na Muheza jana, Katibu Tawala  Mkoa wa Tanga,  Salim Mohammed Chima  alisema elimu ya mfuko wa afya ya jamii inahitajika na  kuwataka viongozi wenye  dhamana kuacha  kujifungia  maofisini.

 Alisema viongozi  wengi wamekuwa  wakishindwa kutekeleza wajibu wao wakiwemo watu wenye  dhamana kushindwa  kuhamasisha jamii kujiunga  na mifuko wa bima  ya afya ya jamii.  

 “Leo nawafungulia  kikao chenu wenyewe  cha kujadili na kuweka mikakati ya jamii kujiunga na mfuko  wa afya ya  jamii---baada ya hapa kila mmoja ahakikishe anatimiza wajibu  wake” alisisitiza Chima

  “Tumekuwa  tukikemea tabia ya wakuu wa  idara na viongozi wenye dhamana kujifungia maofisini na  kushindwa kutekeleza  wajibu wao kwa mujibu wa mikataba ya utumishi wa umma”  alisema

 Alisema tabia ya  viongozi kujifungia  maofisini na kuacha kutekeleza wajibu wao ataikomesha   ikiwemo utoro   pamoja  na muda wa kuingia na kutoka kazini na hivyo kutoa agizo la  kila mmoja kujua  wajibu wake katika kazi.

 Awali akizungumza  katika kikao hicho,  Mganga Mkuu wa Mkoa, Asha Mahita, alipinga vikali ukosefu wa  madawa katika  hospitali zake na kuwabebesha mzigo waganga wa hospitali za  Wilaya kwa uzembe  wa kuacha kuagizia dawa.

 Alisema malalamiko  yanayotoka kwa  wananchi juu ya ukosefu wa madawa ni uzembe wa waganga wakuu  wa hospitali na  hivyo kutoa wito kwa kila mmoja kuhakikisha kituo chake   kinakuwa na dawa za  kutosha ili kuondosha malalamiko kutoka kwa  wananchi.

 “Hakuna ukosefu  wa madawa hospitalini  na ikotokea ni waganga wakuu wa hospitali kufanya uzembe wa  kuacha  kuagizia-----dawa zipo za kutosha na hili nitalishughulikia  mimi mwenyewe”  alisema na kuongeza  

 “Tena natoa wito  kwa wananchi popote  katika Mkoa huu mgonjwa aendapo hospitali na kuelezwa kuwa  hakuna dawa  awasiliane na ofisi yangu au mimi mwenyewe nitalivalia njuga  ” alisema Mahita  

 Kwa kauli hiyo,  Mahita aliwataka  waganga wakuu wa hospitali za Wilaya  kuhakikisha vituo vyao  havipungukiwi na  madawa na kudai kuwa hakuna upungufu huo na yoyote ambaye  atafanya uzembe  atamchukulia hatua. Habari & picha na  Salim Mohammed, Mwananchi 



Read more

Serikali Yasema Zoezi La Kupigia Kura Katiba inayopendekezwa Liko Pale Pale

Serikali imewahikikishia watanzania kuwa zoezi la uandikishwaji wa wapiga kura katika daftari la kudumu kwa mfumo wa kieletroniki BVR litafanyika kwa ufanisi na ndani ya wakati uliopangwa.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda Bungeni leo wakati akijibu  swali la kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani Bungeni Mhe. Freeman Mbowe kuhusu uhakika wa zoezi hilo na pia ameuhakikishia umma kuwa vifaa vinavyotarajiwa  kuletwa vina ubora mara ya mbili ya vilivyoletwa mwanzo kwa ajili ya zoezi la majaribio hilo.

Mhe. Pinda amewataka wananchi wasiwe na wasiwasi bali wajiandaa vyema kwa   kuwa zoezi la upigaji kura kwa ajili ya katiba mpya litafanyika katika tarehe iliyopangwa .
  
Vile vile Mhe. Pinda amesisitiza kuwa  endapo tume itaona kuwa zoezi hilo haliwezekani kwa sababu yoyote ile, itatoa taarifa serikalini na serikali iko tayari kubadili maamuzi.
  
Zoezi la kupiga kura ya maoni linatarajiwa kufanyika April 30 mwaka huu .




Read more

Kamati Ya Bunge Ya Kilimo, Maji Na Mifugo Yaonya Uharibifu Wa Mazingira katika Vyanzo vya Maji


 Uchimbaji wa madini katika chanzo cha maji cha mto Zigi uliopo eneo la Amani Wilaya ya Muheza umeendelea kuleta madhara  makubwa kwa kusababisha kupungua kwa maji ambayo awali yamekuwa msaada mkubwa kwa wakazi wa Tanga.

Hayo yamebainika wakati wa ziara ya siku moja ya Kamati  ndogo ya Bunge ya Kilimo, Maji na Mifugo ilipotembelea katika eneo hilo  mwanzoni mwa wiki  ikiwa ni sehemu ya ukaguzi wa miradi ya maji katika Mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara

Akizungumza mara baada ya kusomewa taarifa ya maendeleo ya chanzo cha maji ya mto Zigi, Mwenyekiti wa Kamati ndogo ya Bunge Mhe. Moshi Selemani Kakoso ameutahadharisha umma kuwa muda uliobaki si wa kulalamikia madhara bali  kila mwananchi ana jukumu la  kuchukua hatua katika utunzaji wa mazingira.

“Wafichueni waharifu wa mazingira kwani waharibifu sio wageni bali ni miongoni mwa wakazi wa eneo husika” alisisitiza Mhe. Kakoso

Vile vile wito umetolewa kwa Uongozi wa Mamlaka ya Maji Tanga kuhakikisha kuwa wanabuni miradi ya maendeleo ambayo ni endelevu ili kuwawezesha wananchi kuachana na uchimbaji wa madini katika eneo la chanzo cha maji.

Wakijibu hoja ya Miradi ya mendeleo, Mamlaka ya maji Tanga imesema tayari ipo miradi mbalimbali ambayo inaendeshwa na Mamlaka hiyo na kiasi cha shilingi millioni 100 zimeshatengwa kwa mwaka 2014/15 kwa ajili ya kuboresha maisha ya wakazi ambao wanaishi eneo karibu na chanzo cha maji cha mti Zigi.

Nao wananchi wakizungumza wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha  Sangarawe ambacho kipo karibu na hifadhi ya taifa ya Amani, wameiomba serikali kuona uwezekano wa kuboresha  barabara ili kusaidia usafirishaji wa mazao kwenda muheza mjini.

Naye mwenyekiti wa Halmashauri ya Muheza amewakumbusha wananchi kuwa tayari serikali imeshaanza mchakato wa kuendeleza barabara hiyo na kwa sasa iko katika kiwango cha changalawe na jitihada zinafanyika ili barabara hiyo iweze kuwekwa katika kiwango cha lami katika siku za usoni.
Katibu Tawala Msaidizi  kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tanga Eng. Ephraim Minde akifafanua jambo mara baada ya Kamati ya Bunge na wawakilishi kutoka Wizara ya Kilimo kuwasili ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Muheza 

 Mjumbe wa Kamati ya Bunge Mhe Subira K. Mgalu  ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Muheza akitoa ufafanuzi na kuonyesha uharibifu unaoendelea katika eneo la Chanzo cha maji cha mto Zigi eneo la Amani Wilaya ya muheza mara baada ya kutembelea eneo la Sangarawe. Kulia kwake ni mjumbe wa Kamati  Vrajlal Son.

 Taswira ya sasa ya baadhi ya   eneo la Sangarawe  baada ya uchimbaji wa madini usio rasmi unaofanywa na vijana wa eneo hilo




 Bw. Shaban Hamis Mzava- Meneja wa Mamlaka ya Maji Wilaya ya Muheza akisoma taarifa ya mradi wa Maji  Kijiji cha Ubembe Wilaya ya Muheza mara baada ya Kamati ya Bunge ya kilimo, Maji na Mifugo kutembelea Mradi huo.

 Kamati ikitembelea mradi huo
Mradi wa maji Kijiji cha  Ubembe Wilaya ya Muheza


Read more